Tumuenzi Gurumo kwa kuendeleza muziki wa dansi
https://habari5.blogspot.com/2014/04/tumuenzi-gurumo-kwa-kuendeleza-muziki.html
Jembe lenyewe ndio hilo |
WIKI iliyopita tasnia ya muziki wa dansi na sanaa nzima kwa ujumla ilipata piga la kuondokewa na msanii nguli wa muziki wa dansi nchini Muhdin Gurumo.
Gurumo alifariki akiwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili baada ya kuuguza maradhi yake ya moyo kwa siku tatu.
Kifo cha Gurumo kimewagusa watu wengi kuanzia wazee, vijana na watoto ambapo pia hata wanasiasa wanamkumbuka mzee huyo kutokana na umahiri wake katika kuimba.
Gurumo alianza kuimba mwaka 1960 atakumbukwa na nyimbo zake zenye kubeba ujumbe kulingana na mazingira husika iwe siasa, uchumi na masuala ya kijamii.
Aliwahi kutamba na bendi ya Sikinde kabla ya kuhamia Msondo na baadhi ya nyimbo zake alizowahi kutamba nazo ni pamoja na Usimchezee chatu, selina piga moyo konde na nyinginezo nyingi.
Aliacha rasmi kuimba muziki mwaka jana baada ya kuwa ameimba kwa miaka 53.
Gurumo aliefariki akiwa na miaka Wakati 74 moja kati ya sababu nyingine iliyomfanya achane na muziki ni kutokana na umri wake kuwa mkubwa na hivyo kuona kuwa kwake ni fursa kuwaachia vijana wengine na wang'ae kupitia muziki.
“Muziki kwangu umekuwa kama asili yangu na kazi yangu lakini nimeamua kustaafu kutokana na umri wangu na nitabaki kuwa mshauri tu kwa mwanamuziki yeyote atakayetaka ushauri wangu,”alivyosema wakati akitangaza kuachana na muziki.
Vilevile Mzee Gurumo amewaasa vijana kuwa wabunifu na kuupenda mziki wa zamani kwani ndio chimbuko la bongofleva na kuwashauri wanamuziki wa sasa kuwa wavumilivu kukaa muda mrefu kwenye bendi moja ili hata wanapoondoka mchango wao uthaminiwe.
Mwanamuziki huyo mkongwe alianza kufahamika katika tasnia ya muziki wa dansi kwenye miaka ya 1960 ambapo mwaka 1964 alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa bendi ya ya Nuta Jazz mwaka 1964 na kudumu na bendi hiyo mpaka mwaka 1978 alipotimkia bendi ya DDC Mlimani Park.
Alidumu na Mlimani Park mpaka mwaka 1985 na kuhamia Safari Sound aliyofanya nayo kazi mpaka mwaka 1990 na kujiunga na Msondo Ngoma mpaka sasa anaamua kustaafu Muziki.
MSANII wa muziki wa Zouk, Hafsa Kazinja anamzungumzi marehemu Muhidin Gurumo kuwa ni mwanamuziki ambae hakuwa na uchoyo kwenye kukukuza vipaji vya wanamuziki wengine.
Anasema kuwa katika kuhakikisha hilo aliurekodi upya wimbo wa Gurumo uitwao Nimuokoe Nani ambao Gurumo aliuimba wakati akiwa na bendi ya Nukta Jazz miaka ya 1960.
Anasema kuwa mbali na wimbo huo kutopewa nguvu zaidi na vyombo vya habari kwa maana ya hauchezwi mara kwa mara kwenye Radio na Luninga mbalimbali.
Anaongeza kuwa hali hiyo imepelekea Mzee Gurumo kufariki akiwa kabla hata hajala matunda ya kazi hiyo kwa kuwa lengo lilikuwa ni kumsaidia baadhi ya fedha zingezopatikana kwenye wimbo huo kusaidia shughuli zake mbalimbali.
"Yani nimeumia sana kwa kuwa mzee huyu alikuwa ni mwenye uwezo sana na wimbo huo wa Nimuokoe Nani ni wimbo wake wa miaka hiyo ya 1960 na mimi nimeuweka katika hali ya upya tayari kwa kufanya kazi"alisema Hafsa.
Hafsa anavitaka vyombo vya habari kuendelea kuhamasisha wanamuziki wa sasa wakamuenzi Gurumo kwa kumba nyimbo zenye maadili na elimu kama alivyofanya Gurumo.
Ni vema mzee huyo nguri wa muziki wa dansi akaenziwa kwa kupigania maendeleo ya muziki wa dansi hapa nchini.
Maana yake ni kuhakikisha kuwa kama mzee huyo aliishi miaka yake yote akiwa kama mwasisi wa muziki huo huku akipigania kupatikana kwa muziki wa Tanzania.
Kwa sasa muziki huo unaonekana kuwa unasuasua kutokana na kukosekana kwa hamasa yake.
Kuna hali ya kurushiana mpira katika kusuasua huko kwa maendeleo ya muziki wa dansi wa sasa, wapo wanaodai kuwa vyombo vya habari vinahusika kwa ukaribu zaidi katika kuuporomosha huku waandishi wa masuala ya sanaa nao wanasema kuwa kusuasua kwa maendeleo ya muziki huo kunatokana na kushindwa kwa wanamuziki hao kutunga nyimbo mpya kila siku.
Wakati ambapo wasanii kama akina Gurumo, Malijani Rajabu, Baraka Mwinshehe kulikuwa hakuna sana ushindani katika muziki kwa maana ya kwamba kulikuwa kuna bendi za muziki za hapa hapa nyumbani zaidi zilizokuwa zikipiga miziki ya yenye maadhi ya hapa nyumbani.
Lakini hali hiyo ilikuja kubadilika baada ya kuwepo kwa wanamuziki walioanza kupiga nyimbo zenye asili ya Congo.
Hiyo ilileta ushabiki wa kundi fulani la wapenzi wa muziki wa dansi kupenda nyimbo hizo kwa maana ya nyimbo zinazopigwa na bendi kama Twanga Pepeta, Fm Academia, Extra Bongo na nyinginezo.
Uwepo wa bendi hizo zenye kupiga nyimbo kwa maadhi ya kikongo umeongeza ajira kwa wanamuziki waliokuwapo enzi hizo na hata kusaidia pia kuibua vipaji vipya vya waimbaji ambavyo ndio vinatamba hadi sasa.
Lakini hata hivyo haijaathiri kabisa muziki wa unaopigwa na bendi zenye miondoko ya akina Msondo au Sikinde.
Hii kwa maana ya kwamba hata ukienda kwenye kumbi zao za burudani utakuta wanawapenzi wengi zaidi pia.
Lakini katika vyombo vingi vya habari hasa radio na Luninga vimekuwa vikitoa kipaumbele katika aina ile ya muziki wenye maadhi ya Congo na ule wenye maadhi ya akina Sikinde na Msondo haupewi kipaumbele sana.
Hali hiyo imepelekea wanamuziki wa muziki wa dansi wameanzisha umoja wao wa kutetea haki ya muziki huo.
Juma Jao ambae ni mwalimu wa kujitegemea wa muziki anasema kuwa umoja huo utakuwa na majukumu mengi katika kuhakikisha kuwa muziki huo unazidi kukua.
Anaongeza kuwa muziki wa dansi kwa sasa umekuwa ukionekana kutopewa msaada unaotakiwa kutoka kwa wadau wa muziki.
Anaongeza kuwa kuwa vipo baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikitoa kauli kuwa muziki huo umekufa kauli ambayo inahatarisha maendeleo yake.
"Kutokana na hali hii kwa sasa wanamuziki wengi wametokea kutokuwa na imani ya kuwa wanaweza kupata msaada wa kweli kutoka kwa baadhi ya vyombo vya habari"anasema Jao.
Akizungumzia majukumu zaidi ya kamati hiyo anasema kuwa kitakuwa na majukumu ya kufuatilia masuala mbalimbali nyeti yahusuyo muziki wa dansi na namna ambavyo vyombo vya habari vinaweza kusaidia.
Anaongeza kuwa msimamo wao ni kwamba sio kweli muziki huo unakufa kwa sababu wanamuziki hawatoi nyimbo mpya ila ni kwa sababu wahusika katika vyombo hivyo vya habari hawatoi kipaumbele katika kusaidia muziki wa dansi.
"Utakuta mwanamuziki anapeleka wimbo wake mpya lakini wimbo huo hauchezwei kabisa kwenye vyombo vya habari hasa hizo radio na wanatoa kipaumbele kwa nyimbo za Bongo Fleva na hata za Kinaijeria kabisa"alisema Jao.
Lakini bado changamoto kubwa inabakia kwa wanamuziki wa muziki huo wa dansi wa staili za akina Msondo na Sikinde kujipanga ili kuendelea kuongeza hamasa ya aina hiyo ya muziki.
Kwa kuwa watu wengi hasa vijana kwa sasa wanapenda nyimbo zenye maadhi kama zile za Bongo Fleva, Muziki wa Kikongo na hata muziki wa Nigeria.
Hiyo inapelekea hata baadhi ya vyombo vya habari hasa Radio na Luninga kujikuta vikipenda zaidi kupiga nyimbo za aina hiyo kwa maana ya Bongo Fleva Nigerian Flavor au bendi kama hizo za wanamuziki wa aina ya Twanga Pepeta na Mashujaa.
Kinachotakiwa kwa wanamuziki wanaoimba aina ya muziki wa akina Msondo kujipanga pengine hata kwa kuhakikisha kuwa wanatengeneza basi Video nzuri za miziki yao.
Kwa wanamuziki ambao walisaidia kuufikisha muziki huo wa dansi yenye maadhi ya kitanzania hapa tulipo ndio hao hao wanatakiwa kusaidiwa kuuendeleza na kuupeleka mbele zaidi.
Hivyo nguvu za akina Gurumo walizotumia kuufikisha muziki huo hapa ulipo ni vema zikaendelezwa kwa kuuweka kwenye soko la kisasa zaidi kwa maana ya kujiweka hata kwenye mitandao ya kijamii ambapo humo kuna Face book, Twitter na hata mitandao mingine.
Nyimbo zao ziwekwe na zifanyiwe matangazo zaidi miito ya simu na zitumiwe kama miito kwenye simu mbalimbali kwa maana ya kuwa ziuzwe kwenye makampuni hayo.
Hivyo ili kuendeleza harakati zilizofanywa na wanamuziki waasisi wa muziki wa dansi hapa nchini akina Gurumo, Baraka Mwinshehe ni vema walipo wakawa na mkakati wa kuukuza muziki huo kisasa zaidi.