Makala: Jisomee kuhusiana na tuzo za Kili
https://habari5.blogspot.com/2014/05/makala-jisomee-kuhusiana-na-tuzo-za-kili.html
Diamond na Wema |
HIVI majuzi zilifanyika tuzo za muziki za Kilimanjaro Tanzania Music Award 2014 (KTMA) ambapo zilifana na kushuhudiwa wasanii wengi wakichukua tuzo zao.
Ilikuwa ni katika ukumbi wa Mlimani ambapo sherehe za utoaji tuzo hizo zilipambwa na burudani safi kutoka kwa wasanii mbalimbali.
Ikilinganishwa na miaka ya nyuma mwaka huu shughuli nzima ya tuzo hizo imekuwa nzuri zaidi.
Aina ya burudani iliyokuwa ikitolewa na wasanii ilikuwa ni ya kuvutia na yenye vionjo vya asili, mfano mzuri ni msanii Hamis Mwinjuma aliekuwa akiimba huku akiwa amezungukwa na wamasai na pia hata wasanii wa kundi la weusi nao waliimba huku wakiwa wamevalia mavazi ya asili na hivyo kuweka kuitekeleza dhana ya kikwetukwetu vema zaidi.
Muziki ulikuwa mzuri kwa maana ya kwamba wasanii walifanikiwa kutumi avema vyombo vya muziki bila ya kuwepo kwa aina yoyote ya vyombo kugoma.
Watumiaji wa vyombo vya muziki inaonekana kuwa walifanya mazoezi ya kutosha kwa maana walikuwa wakijua ni wapi na namna gani ya kuanza na kumalizia kupiga vyombo vya muziki kwa kila msanii.
Moja kati ya vivutio vikubwa katika setka nzima ya sanaa siku hiyo ilikuwa ni uimbaji wa pamoja uliofanywa na wasanii mbalimbali wa kike.
Wasanii hao walikuwa ni Vanesa Mdee maarufu kama V Money, Angela Karashani maarufu kama Angels, Menina Atick na Alice.
Wasanii hao waliimba pamoja na kisha baadae kila mmoja kuimba kivyake vyake huku wakisindikizwa na muziki wa Live.
Akizungumzia hatua hiyo Angels anasema kuwa walitumia wiki tatu kujifua wakiwa katika usimamizi wa wataalamu wa muziki kutoka Tanzania House of Talent (THT).
Anaongeza kuwa tuzo hizo za muziki zilitoa nafasi kubwa kwa wasanii wa aina zote kuanzia wasanii wakubwa wa sasa, wasanii wa zamani na hata wasanii chipukizi.
Burudani nyingine safi ilikuwa ni ushindani wa uchezaji na uimbaji uliofanywa na makundi mawili ambapo kundi la Makomandoo pamoja na kundi jingine lililokuwa chini ya dansa na mwimbaji msanii anaetamba na wimbo wa Sound Track.
Walishindana kucheza na kuimba huku kila kundi likitumia ubunifu zaidi wa kucheza kuzunguka jukwaa na hivyo kuongeza furaha zaidi kwa wageni waliohudhuria.
Tukio kama hilo lilifanywa na bendi ya Twanga Pepeta na ile ya Extra Bongo ambapo Kalala Junior aliongoza kwa upande wa Extra Bongo huku Super Nyamwela.
Mbali na burudani hizo na nyingine za aina mbalimbali kupendezesha siku hiyo, lakini pia kulikuwa na aina nyingine ya burudani kutoka kwa aliekuwa akiendesha shughuli hiyo (MC) aliekuwa Mpoki ambae ni mmoja kati ya wachekeshaji wakubwa hapa nchini.
Mpoki inaweza kuwa alikuwa akiongoza kwa kufurahisha lakini pia kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni kero kwa wengine.
Alifanikiwa kuwafanya watu wafuatilie kiundani zaidi hafla hizo kwa kuwa mbali na kuburudika wageni walipata aina ya vichekesho kutoka kwa Mpoki.
Tofauti na ilivyokuwa mwaka jana au hata mwaka juzi ambapo kulikuwa na MC na kisha akimaliza kutaja wanaotakiwa kuchukua tuzo anakuja mchekeshaji anakaribisha burudani na kwa aina ya uchekeshaji pia.
Kwa mwaka huu Mpoki akisaidiana na mtangazaji mwengine aitwae Shadee aliendelea moja kwa moja na ukaribishaji wa burudani na utangazaji wa vipengele vilivyokuwa vikifuata.
Mpoki kuna wakati alizidisha utani na kuangalia zaidi kuwachekesha watu waliohudhuria hafla hiyo bila ya kujali kuwa kuna wakati alikuwa akiwakosesha amani wengine.
Utani kama ule wa kusifia zaidi kabila lake la Kihaya na kisha kuonesha dharau kwa kabila ya kizaramo.
"Ukisikia jina la Rweyemamu basi ujue kuwa anasoma ulaya au marekani lakini ukisikia sijui Mwajuma basi ujue huyo mzalamo anauza uji nje ya nyumba yao"anasema Mpoki.
Kauli kama hizi sio nzuri hasa kwa tukio kubwa kama hilo la sanaa ambalo linatazamwa na watu mbalimbali kupitia Luninga zao.
Suala kama hilo la ukabila au utani wa aina yoyote ambao unaonekana kuwagusa wakina dada inatoa maana halisi ya tukio kubwa kama lile na hivyo utani wa kusema kuwa wakinadada wamekuja wamevalia nguo ndefu sababu miguu yao ina mabaka sio utani mzuri.
Mbali na kasoro kama hizo bado Mpoki anaonesha ni kwa kiasi gani alivyo na kipaji cha uchekeshaji hasa pale alipokuwa akitoa utani wa hapo kwa hapo.
Kivutio kingine cha burudani ilikuwa ni aina ya upigaji wa Saxaphone uliofanywa na mkongwe King Maluu ambae alitumia kifaa hivyo kupigia nyimbo za wasanii wakubwa wa Bongo Fleva kama Diamond (My Number One) na Ommy Dimpozi (Tupogo).
Alitumia takribani dakika 15 kupendezesha siku hiyo ambapo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa aina hiyo ya burudani kuonekana katika tuzo hizo.
Katika utoaji wenyewe wa tuzo msanii Nasib Abdul, Diamond aliechukua tuzo sana zikiwa ni kama vile Video Bora, Wimbo Bora,Wimbo wa kushirikishwa,msanii mtumbuizaji,msani bora bongo fleva wa kiume, mtunzi bora, Wimbo bora wa Afro Pop.
Usiku hup ulionekana kuwa ni wa msanii huyo kutokana na kuchukua tuzo nyingine lakini pia ni kutokana na namna alivyopambwa na mpenzi wake Wema Sepetu.
Akizungumza na gazeto anasema kuwa kwa sasa amebakiza kupewa tuzo za MTV ambazo anawania kipengele cha wimbo bora wa kushirikishwa ambao ni wimbo wa My Number One alioimba na msanii kutoka Nigeria Dovido.
"Kwa sasa nimepata tuzo saba za MTV lakini ninaona kuwa kuna changamoto kubwa mbele yangu ambayo ni kushinda tuzo za MTV na ninaomba kuwa wananchi wasiniangushe"anasema Diamond.
Siku hiyo pia kulikuwa na upekee wa aina yake baada ya msanii Farid Kubanda, Feed Q kutunukiwa tuzo mbili kama msanii bora wa Hip Hop pamoja na wimbo bora wa Hip Hop.
Akizungumzia hatua hiyo anasema kuwa ni imani yake kuwa kwa sasa watu wamejua uwezo wake wa muziki na wamelionesha hilo kwa kumchagua.
"Hii ni hatua kubwa kwangu na kwa wapenzi wa muziki wangu kwa kuwa wamekuwa nami kwa halinamali na kila mwaka kunipigia kura hatimae nimepata tuzo mbili"anasema Feed Q.
Hoja hiyo ya Feed Q inaungana na hoja nyingine kutoka kwa wasanii mbalimbali kuwa wamekuwa matokeo yao yakichakachuliwa na kushindwa kutajwa kama washindi wa tuzo hizo.
Lakini pia wapo ambao wanalalamikia ni kwa nini wametolewa kwenye kuwania tuzo hizo kwa sababu mbalimbali ambazo wanasema kuwa kwa asilimia kubwa ni uonevu.
Lakini pia kwa mwaka huu imekuwa ni tofauti kidogo kwa kuwa wale wasanii walioonekana kuwa nyimbo zao hazina maadili walizuiliwa kugombania tuzo hizo.
Godfrey Mwingereza ni Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), baraza lenye dhamana ya kusimamia na kuendesha tuzo hizo anasema kuwa hatua hiyo ni kuwakumbusha wasanii umuhimu wa maadili.
"Kuwazuia kushiriki katika tuzo hizi ni kuhakikisha kuwa wasanii wanakumbuka na kuzingatia maadili katika utengenezaji wa Video na Nyimbo zao"anasema Mwingereza.
Kwa upande wake meneja wa kinywaji cha Kilimanjaro ambao ni wadhamini wa tuzo hizo, George Kavishe anasema kwa wasanii ambao wanaona kuwa tuzo za mwaka huu hazijawatendea haki wanaweza kumuona na kupewa mwelekeo gani wa kufuata ili wajue hatma yao.