Walimu wa muziki wa "Kikwete" watumiwe vema
https://habari5.blogspot.com/2014/07/walimu-wa-muziki-wa-kikwete-watumiwe.html
Na Evance Ng'ingo
HIVI majuzi walianza kuingia kutoka Marekani wakufunzi wa muziki ambao ni moja kati ya matokeo ya Rais Kikwete katika kuendeleza sekta ya sanaa hapa nchini.
Wakufunzi hao wa muziki ni matokeo ya ziara aliyoifanya Kikwete Marekani ambapo alienda kwa ziara ya kikazi na kuamua kuwaleta hapa nchini wataalamu hao wa masuala ya muziki kuja kuwanoa wasanii wa hapa Tanzania.
Ujio huo umekuja wakati mzuri ambapo kwa sasa wasanii wa Tanzania wamejikuta wakiiweka nchi vema kwenye ramani ya muziki hasa pale wasanii kama akina Nasib Abdul, Diamond wakiwa wameenda katika viwango vya kimataifa katika masuala ya muziki.
Ujio huo wa wataalamu hao wa muziki ambao ni Mtangazaji wa Kipindi cha burudani cha E, kilichopo chini ya Channel ya BET Terence J, Meneja wa msanii Luda Chriss, Shaka Zulu, Meneja aliefanya kazi na akina Lil Whyne, na wengine wakubwa Marekani David Banner
Kwa kuwa wataalamu hao wamekuja hapa nchini kutoa elimu ya muziki hivyo ni wakati sasa kwa wataalamu wetu wa muziki hapa nchini kutumia weledi wa wataalamu hao.
Binafsi ningependekeza kuwa moja kati ya namna bora ya kuvuna weledi wa wataalamu hao wa muziki ni kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo wa Training to trainers, nikiwa ninamaana ya kuwa wawafundishe wataalamu wa muziki ambao nao wawafundishe wasanii wa hapa nchini.
Kwa kufanya hivyo itasaidia kuwepo kwa mfumo endelevu wa kutoa elimu ya sanaa kwa kuwa watakaofundishwa na wao watawafundisha wengine pia.
Haina maana kuwa kwa Tanzania hakuna wataalamu wa muziki wanaoweza kuwafundisha wasanii wa hapa nyumbani kuimba ila kinachotakiwa kutambulika hapa ni kuwa wataalamu hawa wao wana uelewa mkubwa katika soko la muziki la kimataifa.
Soko hilo ndio ambalo leo wasanii kama akina Diamond ndio wanalikimbilia na ndio soko ambalo inatakiwa ndani ya miaka mitano ijayo kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na wasanii wakubwa wengi ambao wanaweza kufika anga la kimataifa.
Hivyo ninaposema kuwa wataalamu hao watumiwe kuendeleza muzii wa Tanzania nina maana kuwa nimfumo wa kuangalia zaidi sio tu namna ya kuimba kama njia ya pekee ya kuendeleza muziki ila kuangalia na mengine yanayotokana na muziki na ni kwa namna gani yanaweza kuendelezwa.
Kwa biashara ya muziki peke yake inahusiana na masuala mengine mengi kama vile matumizi ya mitandao ya kijamii katika kujitangaza, utengenezaji wa video bora pamoja na usambazaji wake, uimarishaji wa haiba ya msanii, soko la muziki la kimataifa pamoja hata na namna gani soko la muziki wa Bongo Fleva linavyoweza kwenda kimataifa zaidi.
Iwapo wataalamu hao wkaitumiwa vema hasa sio tu kwa kuzungumza na wasanii peke yao lakini wakawekewa mfumo mzuri wa kuzungumza na wataalamu wengine wa sanaa hasa walimu wa sanaa, itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa kwa watu hawa ambao nao ndio wanafanya kazi na wasanii kila siku.
Ni wakati sasa wa kuhakikisha kuwa sekta ya muziki kwa hapa nchi sio tu inakuwa bali pia inaimarika na kuwakilisha vema nje ya nchi kwa kuzalisha wasanii wengi watakaovuka mipaka na kuvuna mafanikio ya maisha nje ya nchi kupitia sekta ya sanaa.
Nchi nyingi kwa Afrika Mashariki na Kati wanatumia lugha hii ya kiswahili huku kukiwa hamasa kubwa ya wakazi wa nchi hizo wakishabikia aina hii ya muziki.
Hivyo kukiwa na elimu nzuri ya muziki pamoja na soko lake ni dhahiri kuwa kutazaliwa akina Diamond wengi ambao watatoka nje ya nchi wakienda kuimba na kuvuna hela kupitia muziki na kisha kuja kusaidia jamii zao za kitanzania.
Ni imani yangu kuwa wale ambao wamepewa jukumu la kuratibu ratiba ya wataalamu hao wa muziki wa Marekani kwa hapa nchini wataandaa mfumo mzuri wa kuhakikisha kuwa elimu ya wataaalamu hao inakuwa na matunda mazuri kwa maendeleo ya sanaa kwa hapa nchini.
====================