Hatuiogopi Al Ahly

WAWAKILISHI  wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, Yanga imejipanga kikamilifu kuing'oa Al Ahly kwenye michuano hiyo.

Yanga inatarajia kucheza na Al Ahly mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao baada ya kuiondoa Komorozine ya Comoro kwa jumla ya mabao 12-2 kwenye mechi za awali katika michuano hiyo.

Yanga imesema itabadili mbinu za kujiandaa kabla ya kukabiliana na Al Ahly.

Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu aliliambia gazeti hili jana kuwa kama uongozi wanajua ugumu uliopo mbele yao baada ya kuwatoa Komorozine, watahakikisha wanaipa maandalizi mazuri timu yao kulingana na timu ambayo watacheza nayo.

“Tunacheza na mabingwa watetezi Al Ahly, tunajua ni timu kubwa Afrika na sisi tumejipanga kuhakikisha tunabadili mbinu tulizotumia kuiandaa timu yetu kwa ajili ya mechi ya Komorozine na tutatumia mbinu nyingine kulingana na timu tunayokwenda kupambana nayo, lengo ni kuhakikisha tunashinda,” alisema Njovu.

Njovu alisema baada ya kuwa na uhakika wa kuvuka raundi ya kwanza tayari walishaandaa mikakati ya kufanya, ikiwa ni kuboresha kambi ya timu yao, kuwajenga wachezaji wao kisaikolojia na benchi la ufundi kuwapa mbinu ambazo zinaweza kuifanya Yanga ikafuta uteja na Waarabu mwaka huu na kusonga mbele.

“Kama uongozi hatuna wasiwasi kwa sababu tunaiamini timu yetu na tumekamilisha kila kitu katika mambo ya kuiandaa timu kuelekea kwenye mchezo huo, lakini hata kocha ametuhakikishia kwamba Yanga itafanya vizuri kutokana na kuwajua vizuri Al Ahly, mbinu zao na pia ni timu ambayo ina wachezaji wengi wenye umri mkubwa,”alisema Njovu.

Njovu alisema Yanga itaendelea na kambi yake ya Bagamoyo kujiandaa na mchezo huo pamoja na ule wa Ligi Kuu utakaochezwa Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting, lengo likiwa ni kuwapa utulivu wachezaji wao ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mchezo huo ambao unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Taifa kati ya Februari 28 au Machi 2, mwaka huu.

Yanga ndiyo wawakilishi pekee waliosalia kwenye michuano ya kimataifa kwa timu za Tanzania bara na Visiwani baada ya timu za Azam, KMKM na Chuoni kutolewa kwenye hatua ya awali ya michuno hiyo ya kimataifa.


Wakati huohuo, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limeipongeza Yanga na timu nyingine za ukanda wake kwa kusonga mbele kwenye michuano ya kimataifa.

Taarifa ya Cecafa kwa vyombo vya habari jana ilizitakia timu hizo mafanikio mema katika raundi inayofuata.

Huku ikizitaka timu zilizotolewa mapema kujiuliza na kurekebisha makosa ili zifanye vizuri zitakapopata nafasi hiyo mwakani.

Mbali na Yanga, timu nyingine za ukanda wa Cecafa zilizosonga mbele kwenye michuano ya CAF ni  KCC (Uganda)  iliyoiondoa Merreikh (Sudan) kwa jumla ya mabao 3-2.


Gor Mahia ya Kenya iliyoiondoa US Bitam ya Gabon kwa mikwaju ya penalti, Flambeau de I’EST FC (Burundi) iliyoiondoa  Diables Noir ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa jumla ya mabao  2-1.

Dedebit ya Ethiopia iliyoiondoa KMKM ya Zanzibar kwa jumla ya mabao  3-2, AFC Leopards ya Kenya iliyoiondoa Defence ya Ethiopia, AS Kigali ya Rwanda na Al-Hilal ya Sudan.
Mwisho.

Related

Sticky 4502588630757262951

Post a Comment

emo-but-icon

item