Alichomaanisha Profesa J katika wimbo wa Kipi Sijaskia


   
MOJA kati ya nyimbo ambazo kwa sasa zinasikika zaidi kwenye vituo mbalimbali vya radio ni wimbo wa msanii Joseph Haule, Profesa J uitwao Kipi Sijaskia.

Wimbo huo ni wimbo ambao unazungumzia masuala mbalimbali yaliyowahi kusemwa kuhusiana na msanii huyo.


Wimbo huo ambao ameshirikishwa msanii Nasib Abdul, Diamond ambapo Prof J anasikika akisononeshwa na watu ambao wamekuwa wakimshutumu mengi kuanzia maisha yake binafsi hadi kazi zake za muziki.


Wimbo huo umekuwa ukitumiwa kwa sasa kama wimbo wa ushauri kwa watu wenye kusemwa vibaya au kupakaziwa masuala mengi katika jamii.


Akizungumza na gazeti hili msanii huyo alieanza kujishughulisha na  fani ya muziki tangia miaka ya 1995 alisema kuwa aliutunga wimbo huo tangia mwaka 2011.


Profesa J akiwa kama mmoja kati ya wahasisi wakubwa wa muziki huo alienza muziki akiwa na kundi la Hard Blasters ni mmoja kati ya wasanii waliochangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha fikra za muziki wa Bongo Fleva hapa nchini.


Kupitia wimbo wake wa Chemsha Bongo wa mwaka 1998 alitoa elimu kuhusiana na vijana ambao wanategemea wazazi wao na kushindwa kujishughulisha kutafuta vipato vyao wenyewe.


Akaendelea kutamba zaidi hadi kwenye mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipotoa nyimbo zake kama vile Bongo Dar es salaam, Ndio Mzee na nyinginezo na kuwa mmoja kati ya wasanii wachache wa zamani ambao wanatamba hadi sasa.


Kupitia wimbo huu ambao umetoka sasa katika vyombo vya habari amegusa tena nyoyo za watu wengi hasa kwa kuzungumzia maisha yake.
Profesa J aliliambia gazeti hili kuwa moja kati ya vitu vikubwa vilivyokuwa vikimsumbua kwa muda mrefu ni kuambiwa kuwa ameathirika na uogonjwa wa Ukimwi.


Anasema kuwa hali hiyo ilimfanya akose amani kwa muda mrefu tangia miaka alipokuwa akiambia mambo hayo.


  Anasema kuwa ikiwa ni kwenye mwisho mwa miaka ya 2000 ilipoanza kutolewa kwa tuhuma hizo alijikuta akinyooshewa vidole na watu.


Anasema kuwa mwaka 2011 aliamua kutunga wimbo kuhusiana na yale mengine mengi aliyosikia akiambiwa kujihusisha nayo.


"Najua kuna kipindi nilianza kuambiwa kuwa nimeambukizwa virusi vya ukimwi huku hali hiyo ikielezwa kabisa waziwazi kutoka kwa watu wengine walikuwa marafiki zangu kabisa wa karibu"alisema Profesa J.


Anaongeza kuwa katika wimbo huo amegusia hilo hasa kwa kusema kuwa "Mlisema nimeathirika kutokana na kukonda ghafla lakini wale mlionipakazia wengi wenu tumeshawazika".


Anasema kuwa kauli hiyo katiak wimbo wake ni kweli kabisa inawagusia baadhi ya watu anaowafahamu kuwa walimtangaza kuathirika na wengi wao wamefariki kwa ugonjwa huo huo au matatizo mengine.


Anaongeza kuwa inasikitisha katika jamii kuona kuwa wapo watu ambao kazi yao ni kuwasema wengine kwa mabaya.


Anasema kuwa mbali na kuwatangazi wenzao kuathirika ila wanawatangazia ubaya zaidi kuhusiana na mengi.


Anasema kuwa hali hiyo imepelekea watu wengina kushindwa kuendelea na kazi zao za kawaida za kila siku kutokana na kunyanyapaliwa na watu katika jamii.


"Mimi nakwambia kuwa yupo mwanamama mmoja aliamua kujiua hivihivi kutokana na kuambiwa kuathirika sasa ndugu yangu hata kama iwe ni kweli sasa inakuwaje mtu anasakamwa kwa kiasi cha mwenyewe kuamua kujiua?"alihoji Profesa J.


Anasisitiza kuwa kutokana na hali kama hizo aliwahi kutunga wimbo uitwao Usinitenge ambapo ndani yake aligusia masuala nyeti kuhusiana na kunyanyapaliwa kunavyofanyiwa na waathirika katika jamii.


Katika wimbo huo Profesa J ameendelea kugusia mengi katika maisha ya kawaida ya kila siku kuna Verse anasema "kuna washkaji wengine feki wakipata dili hawakujui wamekalili kuwa kila jogoo akiwika ni asubuhi".


Akifafanua kuhusiana na ujumbe alioulenga katika wimbo wake huo anasema kuwa wapo hata wasanii wengine ambao wakialikwa kwenye shoo nje ya nchi au hata hapa hapa nchini wakiombwa namba za simu za wasanii wengine ili nao waitwe inakuwa ngumu kutoa.


Anasema kuwa hali hiyo ndio iliyomfanya kuwasema kuwa ni marafiki feki wakipata dili hawakujui na wanaona kuwa kila jogoo akiwika kwao ni asubuhi.


Anawasihi wasanii hao kuona kuwa sio wakisikia kuwa wamepata dili la kazi za kulipwa na wao wakiona kuwa nyota imefunguka kwao basi ndio inakuwa hivyo hivyo na kwa wengine wao pia ni asubuhi.


Anasema kuwa hiyo ni moja kati ya vitu vinavyosababisha kushuka kwa muziki wa hapa nchini kwa kuwa wasanii wengi ni wanafiki ambao wanalenga kuangushana.


Anafafanua zaidi kuwa hiyo ni tofauti na wasanii wa Nigeria ambao kwa upande wao wanaungana mkono kwa kuoneshana mahala palipo na dili za muziki.


"Ukiona wasanii kama akina Dovido wakija Tanzania wakaziona fursa basi wakirejea tu makwao wanakuwa mstari wa mbele katika kuwalezea wasanii wenzao pa kwenda kuchuma"anasema Profesa J.


Anawataka wasanii kujua kuwa Mungu ndio anatoa riziki na hakuna kwa namna yoyote ile mwanadamu kuzuia riziki hiyo.
Pia gwiji huyo aliedumu katika muziki kwa zaidi ya miaka 20 anasema kuwa pia amewagusia watu ambao wanatumia jina lake kujiingizia fedha.


Anasema kuwa wapo mapromota wanatangaza kwa wananchi kuwa Profesa J atakuwapo katika shoo zao lakini inatokea kuwa kumbe hata kumwalika hawajamwalika.


Anaongeza kuwa hali hiyo imekuwa mbaya na inamtesa kwa kuwa wananchi wanatokea kumchukia  kwa kudhani kuwa amewadharau na kwa upande mwengine promota anakuwa ameshajiingizia fedha.


    Wimbo huo umerekodiwa katika studio ya Bongo Record na amemshirikisha Diamond kutokana na umahiri wake katika kuimba nyimbo za ina hiyo.


"Nimezushiwa mara nne kuwa nimekufa yani ilikuwa ni taarifa rasmi kabisa ambazo watu walinisema na iliniathiri pamojana familia yangu yote na sasa utaona kuwa ni kwa kiasi gani hali ilivyokuwa mbaya"alisema Profesa J.


Akizungumzia ushirikishwaji wake katika wimbo huo Diamond anasema kuwa ni wimbo wenye ujumbe mzito na unahusiana na maisha ya kila siku ya wanadamu.


"Sisi tunaimba muziki wa mapenzi zaidi lakini wapo wanaoimba muziki wa kijamii kabisa na yale muhimu katika jamii na hapa Profesa amewakilisha rasmi Hip Hop na amekuwa akifanya hivyo kwa miaka mingi sasa"anasema Diamond.
=======================

Related

Sticky 906465968598239662

Post a Comment

emo-but-icon

item