Makala: Kifo cha Gurumo

GWIJI wa muziki wa dansi nchini Muhidin Gurumo  amefariki dunia jana baada ya kuuguza maradhi yake ya moyo kwa siku tatu.

Gurumo alifariki jana mchana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa siku tatu akiuguza maradhi yake hayo ya ugonjwa wa moyo.


 Akizungumza na gazeti hili jana mtoto wa kwanza wa marehemu, Abdala Gurumo alisema kuwa kwa sasa msiba upo katika eneo la Makuburi Ubungo.


Alisema kuwa wanasubiria baadhi ya ndugu wengine ili kupanga taratibu za maziko.


Aliongeza kuwa familia imepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa baba yao huyo kwa kuwa alikuwa nguzo na kila kitu katika familia.


"Msiba huu ni mkubwa kwa kuwa baba ametuacha watoto wake sita tukiwa katika hali ya huzuni na tunamuombea kwa Mungu kila heri huko aliko na ampumzishe kwa amani"alisema Abdala.


Gwiji huyo wa muziki alieanza kuimba mwaka 1960 atakumbukwa na nyimbo zake zenye kubeba ujumbe kulingana na mazingira husika iwe siasa, uchumi na masuala ya kijamii.


Aliwahi kutamba na bendi ya Sikinde kabla ya kuhamia Msondo na baadhi ya nyimbo zake alizowahi kutamba nazo ni pamoja na Usimchezee chatu, selina piga moyo konde na nyinginezo nyingi.


Aliacha rasmi kuimba muziki mwaka jana baada ya kusumbuliwa na maradhi hayo ya moyo ambayo ndio yamepoteza maisha yake. 


Alianza kuimbia bendi ya Juwata kwenye miaka ya 1960 na kisha akajiunga na bendi ya Nuta mwaka 1964 akiwa mmoja ya waanzilishi na kisha mwaka mwaka 1978 alijiunga na bendi ya Sikinde Orchestra Safari Sound (OSS) kuanzia 1985 hadi 1990.


pia aliwahi kuimbia bendi za  Nuta   Mlimani Park na hadi anafariki alikuwa ameshatunga nyimbo zaidi ya 200.
 

Wimbo mwingine uliompa sifa Gurumo ni Celina aliouimba akiwa na Mlimani Park. 

Gurumo alizaliwa 1940 katika kijiji cha Masaki, Kisarawe mkoani Pwani. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Sungwi na kumaliza darasa la saba 1956. Pia alipata mafunzo ya dini ya Kiislamu katika madrasa ya kijiji alichokuwa akiishi.

Baada ya kumaliza shule, aliamua kujiunga na bendi ya Kilimanjaro Chacha iliyokuwa na maskani Ilala, Dar es Salaam. Alifanya kazi na bendi hiyo hadi 1961 alipojiunga na Rufiji Jazz pia ya Dar es Salaam.

Alidumu na bendi hiyo hadi 1963 alipojiunga na Kilwa Jazz, iliyokuwa maarufu enzi hizo chini ya uongozi wa marehemu Ahmed Kipande. Bendi hiyo ilikuwa na makundi mawili, Kilwa A na B, Gurumo alikuwa kundi B.

Kwa upande wake msanii wa bendi ya Msondo, Edo Sanga alisema kuwa marehemu alikuwa mwalimu wake na msaada wake wa karibu katika sanaa.


Alisema kuwa anaona kuwa marehemu amefariki katika kipindi ambacho alikuwa bado anahitajika.


Aliongeza kuwa kwa upande wake amefundishwa muziki na Gurumo kwa muda mrefu na kwa  sasa anaona kuwa alikuwa akiendelea kumhitaji kwa hali na mali.


Kwa upande wake mdau wa muziki Juma Mbizo ambae amekuwa akifanya kazi kwa ukaribu zaidi na Gurumo hadi kipindi cha mwisho alisema kuwa kwake upande wake anauona kuwa ni msiba mkubwa kwa kuwa umegusa tasnia nzima ya muziki.


Alisema kuwa mara ya mwisho aliwasiliana nae jana asubuhi kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno na alikuwa akiendelea vema.


"Mimi kama mnavyokumbuka kuwa hata ile shoo yake  ya mwisho pale Sigara tulikuwa pamoja na alikuwa akiniamini katika kuandaa shoo hiyo na tulimaliza na kupata angalau fedha zake za kama kiinua mgongo"alisema Mbizo.


Alisema kuwa mbali na kuwa alikuwa mwanamuziki aliekwisha acha hata kuimba lakini alikuwa anaendelea na ushauri katika tasnia hiyo ya muziki.


Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nasib Abdul, Diamond kwa upande wake alisema kuwa kifo hicho kimemgusa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa alikuwa rafiki yake wa karibu.


Alisema kuwa alikuwa tangia mdogo akisikiliza nyimbo zake na kuwa alikuwa msanii wa aina  yake na ndio maana hata alipoacha kuimba alimzawadia zawadi ya gari.


"Huyu mzee kwanza yeye mwenyewe alikuwa akiupenda sana  muziki wangu na aliwahi kusema hadharani sasa hata mimi nilikuwa nikimchukulia kama mfano kwa kuwa alikuwa msanii mkubwa sana"alisema Diamond.


Related

Sticky 1569107203663844279

Post a Comment

emo-but-icon

item