Makala ya wiki: Tuzo za muziki za Kilimanjaro 2014
https://habari5.blogspot.com/2014/04/makala-ya-wiki-tuzo-za-muziki-za.html
KWA sasa moja kati ya habari kubwa za sanaa hapa nchini ni kuhusiana na Tuzo za Muziki Tanzania za Kilimanjaro kwa mwaka 2014.
Tuzo hizo zinazofanyika kila mwaka kwa mwaka huu zitafanyika mwezi ujao huku kwa sasa tayari mchakato wa upigaji wa kura ukiwa tayari umeshafunguliwa.
Upigaji wa kura ulianza mapema mwezi huu na wasanii mbalimbali wakiwa wameshaanza kujipigia chapuo kuomba kupiwa kura.
Lakini pia wapo wasanii ambao wamekuwa na malalamiko kadhaa kuhusiana na tuzo hizo huku kubwa zaidi ikiwa ni kutolewa kwenye ushiriki wao kwenye tuzo hizo.
Wasani wengine wametolewa kushiriki kwenye tuzo hizo kutokana na nyimbo zao kuwa hazina maadili hasa suala zima la Video za wasanii wenyewe.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) likiwa kama ndio waratibu wa tuzo hizo chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) katika kufafanua kero mbalimbali zilizotolewa na wasanii walikutana nao katika semina elekezi.
Godfrey Mngereza ni kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA anawasihi wasanii wa muziki hapa nchini kuwa na utaratibu wa kutengeneza nyimbo zitakazoishi miaka zaidi ya 50 ijayo bila ya kuathiri haiba zao.
Mngereza anasema kuwa wasanii wa muziki wengi wa sasa wanashindwa kubuni aina ya nyimbo na hata video ambazo zinatunza na kutetea maadili ya kitanzania.
Anasema kuwa wasanii wanatakiwa kutambua kuwa majukumu yao sio kuburudisha peke yake bali kusimama kama kioo katika jamii na kuendeleza maandili ya kitanzania .
Akiongeza hatua za BASATA katika kuwaendeleza wasanii na kuhakikisha kuwa wanabakia katika mstari anasema kuwa kuzuia wasanii waliotengeza video za nyimbo zao zisizokuwa na maadili kushiriki katika tuzo za Kili ni moja kati ya njia muafaka za kuwarejesha kwenye mstari wasanii hao.
Anaongeza kuwa kwa upande nyimbo kama vile Tema Mate Tuwachape wa msanii Madee au ule wa Snura Mushi wa Nimevurugwa zimezuiliwa kutokana na kutozingatia maadili hayo.
Lakini hata hivyo hoja hiyo inakumba na upinzani kutoka kwa baadhi ya wasanii ambao wanasisitiza kuwa sio haki kuwatoa kwenye ushiriki wa kugombea tuzo kwa kuwa hata nyimbo za ulaya zinaoneshwa na wasanii wamevaa nusu uchi.
Ni semina ambayo inaonekana kuwa imegusa wasanii pamoja na wadau wa Basata kwa kuwa wasanii waliwabana watu wa Baraza hilo kuwa uamuzi wao huo hauna mantiki kwa kuwa vituo hivyo hivyo vya luninga bado vinaonesha Video za wasanii wengine wa nje wakiwa wakifanya mambo machafu zaidi.
Msanii Khamis Mwinjuma ni mmoja kati ya wasanii ambao waliwakumbusha BASATA kuwa uwepo wa mitandao ya kijami unaweza pia kuendeleza kuonesha Video hizo na hivyo inakuwa haijasaidia lolote.
Lakini hata hivyo Mngereza anafafanua zaidi kuwa maadili ya Ulaya sio kigezo cha kuyaleta hapa nchini kupitia video hizo na msimamo wa Baraza kama msimamizi wa tuzo hizo ni kuhakikisha kuwa wasanii wanarejea kwenye mstari kwa namna yoyote ile.
"Lakini najua kuwa hoja yangu kubwa hapa nataka kusema kuwa kuna umuhimu wa wasanii wenyewe kuwekeza kwenye elimu ili angalau kuwa na mwanga katika kusimamia kazi zenu za sanaa"anasema Mngereza.
Katika semina hiyo ya takribani saa tano iliyoshirikisha takribani wasanii 50 kutoka katika bendi mbalimbali za muziki, ngoma za asili,nyimbo za taarab,nyimbo za muziki wa kizazi kipya pamoja na watayarishaji wa muziki.
Mbali na wasanii wengine kulalamikia nyimbo zao kutolewa lakini pia wapo ambao wamelalamikia nyimbo zao kutoingizwa kabisa kwenye tuzo hizo.
George Kavishe ambae ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro anasema kuwa wasanii wanatakiwa kujua njia mbadala za kuingiza nyimbo zao sokoni.
Anasema kuwa ili kuweza kuchaguliwa kwenye tuzo hizo ni vema wasani wakatambua kuwa ni nyimbo zilizotoka kuanzia mwezi wa kwanza hadi kabla ya mwezi wa 11 ndio zinakuwa kwenye nafasi ya kushirikishwa kwenye kinyang'anyiro hicho.
"Najua kwa sasa mitaani kumekuwa na baadhi ya wasanii wanasema kuwa nyimbo zao zilikubalika mitaani lakini hazijachukuliwa kwenye kushiriki katika tuzo za mwaka huu, ni vema wakajua ni muda gani wa kuachia nyimbo zao na ziweze kuchukuliwa kwenye tuzo hizi"anasema Kavishe.
Kavishe anaongeza kuwa lengo la tuzo hizo sio kutoa fedha kwa washindi isipokuwa ni kuonesha kwa kiasi gani wanapongeza na kutambua kazi nzuri iliyofanywa na wasanii watakaoshinda.
Anafafanua kuwa wapo wasanii ambao wamekuwa wakidhania kuwa fedha wanazopewa kwenye bahasha ni kutambua ushindi wao lakini ukweli ni kwamba hizo ni fedha za matumizi madogomadogo tu.
"Tunatambua hali halisi ya maisha yetu watanzania tunatakiwa katika hafla kama hiyo pengine kupitia dukani kupendeza na sasa kwa kuwakatia fedha kidogo ni kurudisha kwenye zile zilizotumika katika maandalizi yenu binafsi ya kuja kwenye tuzo"anasema Kavishe.
Anaongeza kuwa TBL imejipanga kuhakikisha kuwa wasanii wananufaika na tuzo hizo kwa namna nyingine kama vile kwa njia ya ushiriki kwenye matamasha ya muziki ambayo yatakuwa yakifanywa na TBL kwa ajili ya washiriki wa tuzo hizo mahiri kama Kili Tour.
Katika hilo wasanii wa muziki wa dansi walilalamikia kuachwa katika ziara hizo ambapo walielezea kuwa kwao wanaona kuwa ni sawa na wametengwa.
Rapa wa bendi ya Mapacha Watatu, Kharid Chokoraa anasema kuwa suala la bendi kusafiri kwa pamoja kama inakuwa inahusisha msafara mkubwa zaidi ambapo kunakuwa na vifaa mbalimbali, wasanii wenyewe hadi wachezaji wa muziki (wacheza shoo).
"Ni kweli kuwa hii inakuwa na gharama lakini kwa upande wetu sisi hakuna shida kama Mapacha Watatu tunaweza kutumia CD na kuendelea kuimba kama kawaida"anasema Chokoraa.
Hoja ya uhalali wa wasanii kushinda tuzo hizo nayo imeibuka kati ya wasanii hasa ikingatiwa na mfumo wa upigaji wa kura ulivyo kwa sasa.
Mfumo unaotumiwa ni kura moja kwa msanii mmoja katika kila kipengele kinachoshindaniwa na namba ya simu iliyotimiwa kwenye upigaji wa kura katika kipengele husika haiwezi kutumiwa mara mbili.
Pia wasanii wanaweza kuomba kwa njia zao wenyewe kama vile kwa kutumia mitandao ya kijamii kama vile Twitter, Facebook, Instragram na njia nyingine.
Hoja hiyo ilimgusa msanii wa kundi la Weusi Asili, Niki wa Pili ambae ni msemaji wa kundi hili kuonesha wasiwasi wake kuwa wasanii wasiokuwa na marafiki wengine kwenye mitandao hiyo au wasiokuwa na uelewa kabisa wa matumizi ya mitandao hiyo kujikuta wakikosa kura.
"Mimi ninaona kuwa hiyo sio sahihi kwa kuwa wapo wasanii ambao hawana kabisa hiyo mitandao au hata kama wanatumia lakini sio waelewa sasa hapa inaama kwa wale wenye marafiki zaidi ya 500 wakipigiwa kura wanajikuta wamejiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kushinda"anasema Niki wa Pili.
Kavishe anatumia mwanya huo kuwataka wasanii kujikita zaidi katika matumizi ya mitandao hiyo ikiwa kama wanataka kujitangaza sio tu kwa ajili ya kupata kura za kushinda tuzo za Kili ila hata katika maisha yao ya kila siku kama wasanii.