Namtambulisha kwenu msanii huyu anaitwa Kadija



MSANII Kadija ni moja kati ya wasanii ambao wameanza kusikika hivi karibuni katika medani ya muziki hapa nchini.


Ni msanii ambae kwa sasa wimbo wake wa Maumivu ndio unatamba katika vituo mbalimbali vya radio.


Msanii huyu mwanadada mweupe,mrefu na mchangamfu alianza kujihusisha na masuala ya muziki tangia mwaka 2011 akiwa kama mwanafunzi wa shule ya muziki ya Tanzania House of Talent(THT).


Kadija akizungumzia safari yake ya muziki anasema kuwa alianza kuimba tangia akiwa anasoma shule ya msingi.


Anasema kuwa enzi hizo wasanii waliokuwa wakitamba ni pamoja na Rehema Chalamila, Ray C ambae ni msanii mfano mkubwa kwake kwa sasa.


Anasema kuwa Ray C alikuwa akimvutia kwa uwezo wake wa kuimba na kukata mauno hasa akiwa jukwaani.


Anasema kuwa kwa upande wake aliamua kuingia rasmi katika darasa la muziki la THT ili kukuza kipaji chake cha muziki akiwa na imani kuwa siku moja atakuja kuwa msanii mkubwa.


Anaongeza kuwa alijiunga na darasa la THT na kujifunza kuimba, kucheza na kujihusisha na masuala yote yahusuyo muziki.


Alipomaliza aliendelea kujihusisha na muziki kwa ukaribu zaidi akiwa na kundi la The Trio lililoshirikisha wasanii kama vile Angela Karashani na Alice.


Kadija akiwa na kundi hilo walijitaidi kufanya nyimbo mbalimbali kabla ya kila mmoja kuamua kufanya nyimbo zake mwenyewe tena.


Kwa sasa Angela ambae aliwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya uimbaji ya Tusker Project Fame msimu uliopita na Alice na anaendelea na nyimbo zake kama msanii wa muziki wa kizazi kipya.


Kadija wimbo wake huo wa Maumizu aliurekodia katika studio ya Surround Sound chini ya mtayarishaji wa muziki Nash Designer.


"Najua unaweza kusukwa katika muziki kwa muda mrefu na kisha kujikuta ukaja siku moja kutoa wimbo ambao ndio ukakutambulisha rasmi katika medani ya muziki"alisema Kadija.


Aliongeza kuwa "Wimbo huu nilikuwa najua kuwa ni mzuri lakini sikujua kabisa kama ni wimbo ambao ungekuja kupendwa kiasi hiki kama ilivyo kwa sasa".


Wimbo huo wa Maumivu anasema kuwa umeandikwa na msanii Ditto wa hapo hapo THT na kuongeza kuwa amemsaidia kwa kila kitu katika wimbo huo.


Anasema kuwa Ditto katika wimbo huo aliandika kuanzia maneno na kuweka kila kionjo ambapo kwake yeye alikuwa na jukumu la kuweka sauti yake tu.


Anaongeza kuwa Ditto amekuwa ni msaada mkubwa kwake kwa kuwa ni katika wimbo huo ndio nyota yake ya muziki imeonekana.


Kadija ameshafanya video ya wimbo huo ambayo ameifanyia katika kampuni ya Legendary ambayo imesimamia kazi zake za kutayarisha video hiyo.


Anaongeza kuwa ilikuwa ni kama bahati kwake kujikuta akiambiwa kuwa inabidi kuimba wimbo huo.


"Nilijiskia furaha sana hasa pale nilipoombwa na Ditto kuuimba wimbo huu ambao awali aliuimba yeye lakini akaja kugundua kuwa ni wimbo ambao unataka mtu mwenye kuweza kuuimba kwa hisia zaidi na ndipo nilipopatikana mimi"anasema Kadija.


Msanii huyo mbali na wimbo huo lakini pia anao wimbo mwengine uitwao Nzogo ambao ameurekodia katika studio ya Legendary. 


Anasema kuwa katika wimbo huo ameimba na kucheza na amecheza sana ikilinganishwa na nyimbo zake nyingine.


Anaongeza kuwa kwa kuwa pia anao uwezo wa kucheza muziki akiwa kama mcheza muziki mwenye cheti ameonesha pia kipaji chake cha pili katika wimbo huo.


Anasema kuwa ni wimbo ambao utaingia sokoni hivi karibuni na utakuwa wimbo wenye mashiko.


Lakini hata hivyo anaongeza kuwa kwake kuimba sio lazima ziwe nyimbo za mapenzi tu ila hata nyimbo za kawaida za kimaisha anaweza kuziimba.


Akifafanua hilo anasema kuwa anataka kuanza kuimba nyimbo kama vile za masuala ya jamii kuhusiana na magonjwa, mazingira, kutoa wito kwa jamii kupitia muziki na mengineo muhimu.


Anaongeza kuwa anapenda kuimba nyimbo za kila aina na kusisitiza kuwa hata kushirikishwa nyimbo za watu wengine kwake anaweza kuzitendea kazi.


Kwa sasa msanii huyo anasema kuwa anashukuru Mungu kwa kuwa ameshaanza kupata mialiko kadhaa ya kufanya shoo.


Anasema kuwa yupo tayari kufanya shoo sehemu yoyote na muda wowote ule kulingana na makubaliano ya kazi zake.


Anaongeza kuwa pia kwa sasa ameanza kujadiliana na kampuni zinazonunua miito ya simu ili kununua nyimbo zake kuanzia wimbo huo wa Maumivu na nyimbo nyingine zinazokuja.


Aliekuwa msanii mwenzake katika kundi la la The TRio,  Alice anasema kuwa Kadija amefungua njia na katika kuendeleza muziki kwa wanawake.


Anasema kuwa anajisikia furaha kuona msanii huyo ameanza kazi yake ya kwanza na imekubalika haraka na kuitaka jamii kumuunga mkono.


Kadija ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto wanne ambapo ana dada yake aitwae Zakia, anafuata yeye Kadija na kisha kuna Salum na Zaharath.

Katika familia yake ni yeye peke yake anaejishughulisha na masuala ya muziki huku ndugu zake wengine wakiwa ni wanajishughulisha na shughuli nyingine mbali na za sanaa.
   

Related

Sticky 8913736524879429527

Post a Comment

emo-but-icon

item