Ziara ya wakongwe wa Real Madrid ilete faida endelevu.
https://habari5.blogspot.com/2014/05/ziara-ya-wakongwe-wa-real-madrid-ilete.html
Na Evance Ng'ingo
JUMAPILI iliypopita kilifanyika kikao cha kutangaza ziara ya kihistoria ya mchezo wa soka kuwahi kutokea hapa nchini.
Tukio hilo sio tu la kwanza kwa hapa nchini bali ni la kwanza pia hata kwa Afrika nzima kwa ujumla kutokana na ukubwa wake
.
Hilo ni kuhusiana na ujio wa timu ya Real Madrid Legend inayoundwa na wachezaji wa zamani wa klabu ya soka ya Real Madrid ambao watafanya ziara rasmi kuanzia mwezi wa nane.
Itakuwa ni ziara ya siku nne ya aina yake kwa medani ya soka hapa nchini kwa kuwa wachezaji hao wa zamani watakuwa hapa nchini kwa siku nne.
Ikiwa Agost 21 ndipo watakapowasili rasmi na kuingia uwanjani mwezi huohuo siku mbili baade yaani Agost 23.
Ziara hiyo ni muhimu sio tu kwa kuhamasisha soka hapa nchini bali pia hata kwa kutangaza vivutio vya utalii kwa hapa nchini.
Wakiwa chini ya udhamini wa Super Market ya TSN, ziara hiyo itaendana sambamba na kutangazwa katika vyombo vya habari vya nchini Hispania.
Hayo ni mafanikio makubwa ya kutangaza utalii kwa njia ya soka kuwahi kutokea hapa nchini.
Kwa kuwa Hispania ni moja kati ya nchi za Ulaya ambazo zinatoa idadi kubwa ya watalii kuja hapa nchini, hivyo kupitia ziara hiyo itakuwa ni nafasi pekee ya kujitangaza na kulipata soko la Hispania na nchi jirani.
Ziara hiyo itaitangaza zaidi Tanzania kimataifa hasa kutokana na wachezaji wakubwa wa sasa wa timu ya Real Madrid ambao ni Gareth Bale, Christiano Ronaldo pamoja na kipa Iker Casillas kuongoza kampeni ya kuutangazia ulimwengu juu ya ujio wa timu hiyo ya wachezaji wa zamani.
Kutokana na ukubwa wa majina ya wachezaji hao duniani ni dhahiri kuwa hiyo itakuwa ni fursa kubwa zaidi kuitangaza Tanzania.
Ni dhahiri kuwa soka litakuwa limetuletea heshima kubwa ya kutangaza nchi yetu kimataifa zaidi.
Akizungumzia ujio huo kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jamal Malinzi anasema kuwa ujio wa wachezaji hao wa zamani wa klabu hiyo ni heshima kubwa kwa Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa ni nchi ya kwanza kwa bara la Afrika kupata heshima hiyo.
Anaongeza kuwa wakiwa hapa nchini wataumana na kikosi maalum cha wachezaji wa sasa kitakachoitwa Tanzania Eleven ikiwa na wachezaji wa sasa wanaotamba ambao watawekwa kambini tayari kupambana na timu hiyo ya wachezaji wa zamani wa klabu ya Real Madrid.
"Yani kutokana na ujio huo kuwa na nia pia ya kutangaza vivutio vya utalii vya hapa nchini kwa njia ya Luninga itakayooneshwa moja kwa moja nchini Hispania hivyo ni heshima kubwa kwa Tanzania".alisema Malinzi.
Aliongeza kuwa"Hii sio kitu cha kawaida kwanza ni ndio mara ya kwanza kwa Afrika na ndio wanaanzia Tanzania hivyo ni imani yetu kuwa tutatangazika vya kutosha ila changamoto kubwa mbele yetu ni kuhakikisha kuwa tunajipanga ili tusijeaibika".
Malinzi anaongeza kuwa kutokana na ukubwa wa ziara hiyo, TFF imejipanga kuhakikisha kuwa inashiriki kikamilifu katika kufanikisha ziara nzima kuwa ya yenye tija kubwa.
Kwa upande wake mwakilishi wa TSN Supermarket, Dennis Sebo anasema kuwa katika makubaliano yao wamekubaliana kuwa wa zamani kama vile Louis Figo, Zinedin Zidane na Van Nestroy ni lazima wawepo.
Anaongeza kuwa kwa upande wake Figo imedhihirika kuwa atakuwapo na hivyo kusisitiza kuwa ni muda kwa washabiki wa soka kusubiria kuona mchezo huo.
"Lengo kubwa ni kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Hispani kupitia soka lakini pia tutatangaza utalii wetu kwa kiasi kikubwa katiak nchi ya Hispania na nchi nyingine zitakazoonesha mchezo huo"anasema Sebo.
Kabla ya ujio wa timu hiyo ya Real Madrid Legend kuja hapa nchini mwezi Agost, walianza kuwasili hapa nchini kwanza baadhi ya viongozi wa timu hiyo na kuzungumza na waandishi wa habari.
Akizungumza kwa niaba ya timu hiyo, mchezaji wa zamani wa Real Madrid ambae ni kapteni wa timu hiyo ya Real Madrid Legend, Ruben de la Red anasema kuwa wamechagua kuanza kuja Tanzania kwa kuwa ni nchi ambayo wamekuwa wakiisikia kwa muda mrefu wakiwa nchini kwao.
Anasema kuwa wamekuwa wakisikia kuhusiana na utalii wa hapa nchini na wamevutika hata kushiriki katika kuutangaza.
"Tunasikia Ngorongoro, Kilimanjaro pamoja na mengine mengi na tutakuwa na furaha na amani kubwa kuja kucheza soka hapa Tanzania
Alikuwana mchezaji mwenzake Rayo Garcia pamoja na mkuu wa mahusiano wa klabu hiyo ya Real Madrid Legend team Isaac Recarey Sanchez.
Inatakiwa serikali kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) pamoja na wadau wengine wa utalii wanatakiwa kujipanga kuhakikisha kuwa ziara hiyo inakuwa ni yenye mafanikio makubwa katika kuutangaza utalii wa hapa nchini.
Lakini sio hivyo tu ila inaweza kabisa kutumiwa fursa kama hiyo katika kuunganisha nguvu ya kuinua soka la Tanzania hasa kwa kuweka ukaribu zaidi kati ya vituo vya kukuzia vipaji vya soka vya hapa nchini na vya kule Hispania.
Ikumbukwe kuwa wapo watoto wenye vipaji katika vituo vya hapa nchini ambao ni hivi juzi tu wlaishinda kombe la dunia kwa watoto wa mitaani michuano iliyofanyikia Brazil na hivyo basi inamaana kuwa angalau kuna nia na uwezo mkubwa wa watoto wa hapa nchini katika medani ya soka.
Mwanzo wa uhusianao mzuri kati ya klabu ya Real Madrid na Tanzania usiishie tu baada ya kumalizika kwa ziara ya wachezaji hao wanaokuja mwezi Agost ila kunaweza kukawa na mahusiano endelevu hasa katika nyanja za kukuza soka la vijana.
Ni imani ya watanzania kwa ujumla kuwa wadau wa soka na utalii wamejipanga kuhakikisha kuwa ziara hiyo inaleta faida kwa sekta ya utalii na soka kwa ujumla.
======================