Wane Star: Gwiji wa sanaa akimbiwae na wanawake, Ana watoto watano, mama tofauti
http://habari5.blogspot.com/2014/02/wane-star-gwiji-wa-sanaa-akimbiwae-na.html
Wanne Star akiwa na Mamis hapo ilikuwa mwaka 2010 kulia ni Sara Israel Miss Tanzania 2010, aliembeba ni Jenifer Kakolaki huku Alexia akiangalia |
Wane akiwa kazini |
Wasanii wake |
WANE Star ni moja kati ya wasanii wakubwa wa muziki wa asili hapa nchini ambae amefanya kazi hiyo kwa miaka zaidi ya 25 sasa.
Msanii huyu ni mzaliwa wa mkoani Mbeya na alianza kujishughulisha na shughuli za muziki na ngoma za jadi tangia akiwa na miaka 8 akiwa mkoani humo.
Jina lake halisi ni Wane Salim Mgaya
Wane amerithi kazi hizo za asili kutokea kwa wazazi wake ambapo anasema kuwa Mama na Baba yake wote walikuwa wasanii walionufaika na mpango wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere kwa kuchukuliwa na kupelekwa nchini China kujinoa kisanaa.
Hayati baba wa taifa alikuwa na mpango maalum wa kuchukua msanii mmoja mmoja kutoka kila mkoa na kisha kuwaendeleza katika elimu ya sanaa China
Anasema kuwa baba yake ambae ni mwenyeji wa mkoa wa Tanga alichukuliwa kama msanii peke yake kutoka mkoani humo kwenda kusomeshwa sanaa na serikali nchini China.
Anaongeza kuwa hata mama yake kipindi hicho akiwa msanii mkubwa wa mkoani Mbeya na alikutwa na bahati hiyo ya kwenda China na ndipo walipokutana na kuwa na uhusiano.
Wakiwa nchini humo mama yake baada ya kujigundua kuwa mjamzito aliamua kurejea nchini kujifungua na baada ya hapo alimwacha wane kwa babu na bibi yake Mbeya na kisha akaondoka kurejea China.
Wane alilelewa na babu na bibi yake mkoani Mbeya hiyo ikiwa ni kufuatia kuachwa kijijini na mama yake na kisha baada ya hapo na ndipo lilipotokea jina la Wane.
Huku babu yake huyo akiwa muislamu na mama yake mkristu walishindwa kuamua mtoto wao ajiunge na dini gani huku wakikwazika wampatie mtoto huyo jina la kikristu au la kiislamu
Babu na Bibi yake huyo waliamua kuchanganya majina ya ukoo wao ambapo ukoo wa babu yake ni
Wasiwaye huku bibi yake akiwa ni kabila la Washipela na ndipo wakakubaliana kutoa jina la Wane.
Jina hilo likiwa linamaana ya kuwa Wangu na hasa hapo ndipo baraka zake katika sanaa zilianzia.
Akiwa na miaka 10 alichukuliwa na kundi la sanaa kutoka mkoani Mtwara lililoenda kikazi Mbeya na walikuwa wakimfahamu mama yake huyo aliekuwa msanii mkubwa Mbeya.
Anasema kuwa alichukuliwa na kisha kuanza kufanya shughuli za sanaa ambapo alikaa na kundi hilo kwa muda mrefu kabla ya kwenda China.
Anasema kuwa akiwa Mtwara alianza uhusiano na msichana wa kichina ambae alimpeleka China kujifunza Sarakati,Mazingaombwe pamoja na Ubunifu.
"Yani hapo ilikuwa ni baada ya kukaa muda Mtwara nikijifua masuala ya sanaa tu kuimba na kucheza ngoma na ndipo Mungu alipoanza kufungua njia na kunikutanisha na mwanamke wa kichina na kwenda kusoma sanaa nchini humo"alisema Wane.
Anasema kuwa wakati huo wote alikuwa hajui lolote kuhusiana na mama wala baba yake na wala alikuwa hajui kuwa walikuwa China muda huo.
Anaongeza kuwa baada ya kusoma sanaa china alilazimika kurejea Mbeya ambapo alichukuliwa na shule ya msingi Muungano lakini wakati huo wote yeye mwenyewe alikuwa hajui kusoma wala kuandika na ndipo walimu hao walipomlazimisha kuingia darasani.
Alianza kusoma kuanzia darasa la kwanza hadi la tatu kabla ya kuhamishiwa shule nyingine iitwayo Maanga napo alienda kufundisha sanaa na akaendelea na darasa la tano.
Wane alipendwa kutokana na uwezo wake wa kufundisha sanaa kwa kuwa miaka hiyo alikuwa ametokea China na hivyo alikuwa na ujuzi mkubwa.
Hiyo ilipelekea kuhamahama akiitwa sehemu mbalimbali kufundisha na akiwa ameshasoma darasa la tano akaamishwa tena kwenda kufundisha sanaa Bandari Mtwara napo akasoma darasa la sita na kisha akapelekwa kufundisha sanaa Bandari Tanga napo ndipo alisoma darasa la saba mkoani Tanga hivyo huyu msanii amesoma shule tano tofauti katika elimu yake ya msingi.
wane alifika Dar es salaam baada ya kuchukuliwa na Magereza Dar es salaam kufundisha sanaa na tangia hapo ndipo hadi sasa anaendelea na maisha yake ya sanaa jijini hapa.
Wane alibadilisha aina yake ya sanaa kwa kuchanganya vionjo mbalimbali na kuifanya sanaa yake kuwa ya kisasa zaidi hiyo ni baada ya kukutana na gwiji wa upigaji wa gitaa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Diblo Dibala katika tamasha la muziki Zambia aliemshauri kuchanganya ngoma za asili katika usasa.
Anasema kuwa baada ya kufuata ushauri huo alianzisha kundi la Wane Star na kuanza kufanya sanaa ya kibishara ambapo amezunguka nchi mbalimbali duniani.
Anasema kuwa ameitwa kutumbuiza na kufundisha ngoma za asili India, China, Marekani, Ujerumani, Arabuni na nchi nyingine mbalimbali duniani.
Anaongeza kuwa akiwa nchi hizo amejikuta akipata watoto pia hasa pale anapokuwa ziara ya muda mrefu, anasema kuwa kwa sasa ana watoto watano ambapo mmoja amezaa na mwanamke wa kikorea, mwengine amezaa na mwarabu huku pia akiwa na mtoto aliezaa na Mjerumani.
Anaongeza kuwa watoto wote hao ni wakubwa na wanaishi na mama zao katika nchi hizo huku wengine wawili ni watanzania ambapo mmoja yupo kidato cha sita Singida na mwengine akiwa anasoma sekondari hapa Dar es salaam.
Lakini Wane anaonekana kusononeshwa zaidi na ambavyo kazi yake ya sanaa imekuwa ikichukuliwa na baadhi ya wanawake anaokuwa na uhusiano nao na ndio maana hadi sasa hajaoa.
"Ninao hao watoto watano lakini kila mtu ninaekuwa na uhusiano nae wa kimapenzi anakataa kufunga ndoa nami hasa likifika suala hilo muhimu, wapo ambao nimeenda hadi kutoa posa lakini wananikimbia "anasema Wane.
Anasema kuwa kikwazo kinachomkwaza kuoa ni wanawake wengi au wazazi wao kutokubaliana na shughuli zake za muziki wa jadi na imani yake ya mizimu.
Anasema kuwa yeye sio Muislamu wala Mkristu ila ni mtu mwenye kuamini mizimu na ndio kikwazo cha wazazi wengi wa mwanamke kumkataa.
"Wapo ambao nilipata nao watoto hasa hawa wa hapa Tanzania na lakini walishindwa kuendelea kuwa nami kwa kuwa imani zangu haziendani nao mimi ni mtu wa mizimu zaidi"anasema Wane.
Anaongeza kuwa nyumbani kwake anaishi na joka kubwa ambalo analitunza na mara nyingine analitoa sebuleni.
Anaongeza kuwa "matukio kama haya yanahitaji moyo hasa kwa kuwa na mtu ambae hana imani za kitamaduni kuishi na mtu kama mimi".
Lakini hata hivyo hiyo haina maana kuwa hana uhusiano au ndio hataki kabisa kuwa na mtu ila kuna wakati anakuwa na mpenzi kumbe anakuwa na nia ya kumtumia kama daraja la kufika mbali.
Hapa anamaanisha kuwa anaweza kuwa ameenda na mpenzi wake kwenye ukumbi na wakati wakiwa wanaendelea na shoo unakuta mpenzi wake anaondoka na mtu mwengine.
Akizungumzia kwa nini asiwe na uhusiano na msanii mwenzake anaongeza kuwa hata wao pia kuna vikwazo vyake ambapo anafafana kuwa wanaweza kwenda kwenye onesho la muziki nje ya nchi na kisha wakati wa kurejea nchini wanatoroshwa.
Kitu kikubwa kilichowahi kumsononesha katika maisha yake ni pale alipooneshwa wazazi wake wakati huo wakiwa kwenye mashindano ya kitaifa ya sanaa na alipoenda kuwasalimia hawakumpatia ushirikiano.
Kwa sasa anasema kuwa mama yake alishafariki lakini baba yake mzazi bado yupo hai na ni mdau mkubwa wa sanaa wa hapa mjini ambae hadi sasa baba huyo hataki kumtambua Wane kama mwanawe.
Wane ndio anawafundisha walimbwende wa Miss Tanzania kucheza shoo zao kwa sasa anafanya shoo zake kila siku ya Jumatano katika onesho la Usiku wa Mwafrika katika hoteli ya Peacock na Jumapili Hoteli Giraffe.
Mwisho