Kumekucha Uchaguzi Chalinze
http://habari5.blogspot.com/2014/03/kumekucha-uchaguzi-chalinze.html
Wanachama wa CCM wakimsubiria mheshimiwa apite |
Mgombe Ubunge kwa tiketi ya Alliance for Tanzania Famers Party (AFP) Ramadhan Mgaya (kulia) akichukua fomu kutoka kwa Ofisa wa Uchaguzi Wilaya ya Bagamoyo Shija Andrew. Saba |
Habari Kamili.
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhwan Kikwete jana alichukua fomu katika ofisi za msimamizi wa uchaguzi wilayani Bagamoyo na leo anatarajia kurudisha fomu hiyo.
Ridhwan alipokuwa akienda kuchukua fomu hiyo alisindikizwa na mamia ya wanachama wa CCM wa jimbo la Chalinze na Bagamoyo wakiwa wanaimba na kucheza kumshangilia mgombea huyo.
Mara baada ya kuchukua fomu kutoka kwa ofisa wa uchaguzi wa wilaya ya Bagamoyo Shija Andrew, Ridhwan alimhakikishia ofisa huyo kuwa atazingatia taratibu zote za uchaguzi na kutoendesha kampeni za matusi na vurugu.
Baada ya kuchukua fomu hiyo pamoja na nakala nyingine muhimu za uchaguzi aliongozana tena na mamia ya wafuasi wake kuelekea kwenye ofisi za CCM Bagamoyo ambapo alizungumza na waandishi wa habari.
Katika mazungumzo yake hayo Ridhwan alitaja vipaumbele vyake kwa kuleta maendeleo kwa wakazi wa Chalinze ambapo alisisitizia kuimarisha upatikanaji wa maji salama na ya uhakika, kuimarisha afya, elimu pamoja na kukuza ajira kwa viajan.
"Kama mnavyofahamu kuwa Chalinze ni eneo ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi kama vile maji, umeme na hata suala zima la ajira kwa vijana sasa pindi ambapo nikipata Ubunge kwangu mimi nitahakikisha kuwa napunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo hilo"alisema Ridhwan.
Aliongeza kuwa "Mimi nimeguswa na changamoto mbalimbali zinazowakuta wakazi wa wilaya hii na kama ambavyo nilisema kuwa sikushinikizwa ila ni kwa matakwa yangu mwenyewe naona kabisa kuwa nipo katika hali na nguvu ya kushirikiana na wakazi hawa kumaliza shida za Chalinze".
Ridhwan pia alisema kuwa atasaidia kutatua ugomvi wa mara kwa mara unaowakumba wakulima na wafugaji na kuwataka wakazi wa Chalinze kutoacha kumchagua.
Wakati huo huo mgombea wa Ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema Matayo Torongey akizungumza baada ya kuchukua fomu alisema kuwa anavyo vipaumbele vingi kimojawapo ikiwa ni kuinua maisha ya wakazi wa Chalinze.
Naye mgombea Ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Alliance For Tanzania Farmers Party (AFP) Ramadhan Mgaya akizungumza baada ya kuchukua fomu alisema kuwa anatambua nafasi ya kilimo na ufugaji katika kukuza maisha ya wakazi wa jimbo la Chalinze.
Wagombea wa AFP na Chadema walipokutana wakati wakichukua fomu walianza kutaniana ambapo Ramadhan Mgaya wa AFP alimwambia mgombea wa Chadema Matayo Torongey akimsisitizia kuwa ataongoza Ubunge huo na kisha kumwachia nafasi ya pili Matayo.
Matayo alionekana kushangaa vazi la Mgaya wa AFP kuwa linafanana na lile la Chadema na kumtaka kujiunga nao katika kuchukua jimbo hilo.
Leo Ridhwan jana hiyo alitangaza kuwa leo atarejesha fomu za kugombea ubunge katika ofisi ndogo za uchaguzi.
Uchaguzi wa jimbo la Chalinze unakuja kufuatia kifo cha aliekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Ramadhan Bwamdogo aliefariki Januari 22 mwaka huu.