Ifahamu hali ilivyokuwa kwenye mkutano wa Simba

Rage akiwa amekumbatiana na Dalali baada ya kumalizika kwa mkutano wao

Meza ya Rage ilizamiwa na wanachama waliokuwa na jaza hawa ni wanachama wa Simba kutoka tawi la Mpira Pesa

Alikutana na marafiki wake wa muda mrefu kwenye Simba

Huyu jamaa ilikuwa bado kidogo arushe ngumi

Na Mwandishi wa blog hii
JUMAPILI iliyopita klabu ya Simba ilifanya kwa mafanikio makubwa mabadiliko ya katiba yake.

Mabadiliko hayo ya katiba yalifanyika katika ukumbi wa Police Officers Mess  ambapo wanachama walitumia muda mwingi kubishania vipengele mbalimbali vya katiba hiyo.


Vipengele vilivyojadiliwa na kufanyiwa marekebisho ni Bendera na Nembo ya klabu, Wajibu wa Wanachama,Idadi ya Mgawanyo wa Wajumbe, Maamuzi ya Uchaguzi na Sifa za Wagombea.

Kipengele ambacho kilizua mjadala mkubwa katika mkutano huo ni suala zima la  idadi ya wanachama wanaotakiwa katika matawi ya Simba

.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo walitoa mawazo yao kutaka idadi ya wanachama wa Simba katika ngazi ya kata wawe 500.


Idadi hiyo ilipingwa na wajumbe wengi kwa kuwa waliona kuwa hiyo ingeweza kuwa fursa ya kufanyika kwa mapinduzi.


Kwa katiba ya Simba inatoa fursa kwa wanachama wakiwa idadi ya nusu ya wanachama wote wanaweza kufanya mkutano mkuu.


Hivyo kama iwapo tawi likiwa na wanachama 500 ni rahisi kwa watu wanaotaka kufanya mapinduzi kununua matawi zaidi ya mawili au matatu na kisha kufanya mapinduzi.


Wapo wajumbe ambao walitaka kata kuwa na wanachama 250 kila moja.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati  ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspope anasema kuwa anaona kuwa kwake anataka wawepo wanachama 1000.


Anafafanua kuwa idadi hiyo ni nzuri kwa kuwa inawapatia watu wengi fursa ya kuwa wanachama wa klabu hiyo.


Ilionekana kuwa kuna makundi tofauti ambapo kundi moja lilikuwa likitaka wanachama kufikia 250 huku wengine wakitaka kuwepo kwa wanachama 500.


Aliepelekea kuibuka kwa mzozo mkubwa ni Mwenyekiti wa matawi ya Simba Mkoa wa Dar es salaam, Ramadhan Hamis, Don King kusema kuwa kwa upande wake anaona kuwa na wanachama 500 ni sawa na hivyo kupelekea wanachama kumzoea kwa hasira.


Hoja hiyo iliibua mzozo mkubwa hadi kufikia hatua ya wanachama kuisogelea meza kuu hali iliyopelekea askari Polis waliokuwapo mahala hapo kuingilia kati na kutuliza ghasia.


Hata hivyo Rage alipopata nafasi ya kuzungumzia kipengele hicho alitoa nafasi kwa wapiga kura kuchagua ni idadi gani wanainataka na ndipo kikapita kipengele cha wanachama 250 kwa ngazi ya kata.


Wajumbe wa mkutano huo waliendelea kuwa na mjadala mkubwa kuhusiana na masuala mbalimbali ya katiba yao mpya wanavyotaka iwe.


Ipo hoja ambayo ilionekana kupitishwa kwa ushabiki na upenzi wa klabu hiyo lakini imeonekana kuja kupingwa katika wadau mbalimbali wa sheria.


Hoja hiyo ni kuruhusu mgombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wa klabu hiyo aliewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai.


Awali katiba ya Simba ilikuwa ikizuia mtu aliewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai kushindwa kugombea uongozi wa ngazi yoyote ya klabu hiyo.


Wanachama waalikataa kipengele hicho kwa kusema kuwa kinawanyima haki wanachama wenye uwezo wa kuongoza.


Wanachama hao walisisitiza kuwa kosa la jinai sio sababu ya kuwakosesha wanachama wa Simba fursa ya kugombea kwa kuwa hata kutukana ni kosa la jinai pia sasa iweje mtu akifungwa kwa kosa hilo na aje kuuziwa kuongoza.


Mmoja kati ya waliotoa hoja ni Juma Selemani ambae anasema kuwa anawajua watu wenye uwezo na fedha za kuongoza klabu ya Simba lakini wanakwazwa na hoja hiyo ya jinai.


Anasema kuwa ni vema angalau kungekuwa na aina za jinai za kuzuiliwa kwa kuwa sio kila kosa ilimradi ni la jinai basi linamzuia mwanachama kugombe.


"Sasa inashangaza kusikia kuwa ilimradi mwanachama eti alikutwa na kosa la jinai basi anazuiwa kugombea uongozi hii itakukosesha Simba kuwa na viongozi wazuri"anasema mwanachama huyo.


Karibia kila mwanachama alionekana kuunga mkono hoja kuwa kipengele kinachozuia mwanachama aliewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai kuondolewa.


Baada ya kupiga kuwa na wanachama kuunga mkono kuruhusiwa wenye jiani kugombea uongozi, kikapitishwa kipengele cha kuruhusu wanachama wote wa Simba sasa ilimradi wamekaa kwenye chama kwa miaka miwili kugombea.


Lakini hata hivyo hoja hiyo inakuja kupingwa na baadhi ya wadau wa michezo nje ya Klabu ya Simba.


Aloyce Komba ni mwanasheria na pia mwandishi wa habari wa michezo wa muda mrefu hapa nchini.


Anasema kuwa kwa uamuzi huo wa Simba kupitisha mabadiliko ya katiba na kuruhusu mgombea mwenye jinai kugombea ni kosa la kisheria.


Anafafanua kuwa katiba zote ziwe za vyama vya siasa,michezo na vyama vinginevyo ni lazima ziendane na katiba mama ya nchi ambapo yenyewe inakataza mtu mwenye kutiwa hatihani kwa kosa la jinai kugombea uongozi.


Anasema kuwa huenda wanachama kwa wakati ule na kwa mapenzi yao waliona kuwa ni sawa kufanya mabadiliko hayo ya katiba lakini sio lazima yapitishwe na msajili wa vyama vya michezo wa wilaya ya Ilala ambapo klabu hiyo imesajiliwa.


Anaongeza kuwa hata Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) na hata Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) yenyewe pia yanapinga mtu mwenye kosa la jinai kugombea uongozi.


"Sasa hao Simba katiba yao itakubaliwa na nani kama wadau wote wanapinga utaratibu huo wa mgombea wa uongozi kuwa aliewahi kukutwa na jinai"anasema Komba.


Hata hivyo kwa upande wake Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura anasema kuwa kwa sasa TFF inasubira nakala ya mabadiliko hayo ili kujiridhisha kwanza kabla ya kusema lolote.


"Ah najua tumekuwa tukiwataka Simba kufanya marekebisho yao ya katiba lakini sio lazima kila kitu kipitishwe kama kilivyo kwetu na kuchukulia kuwa haya ndio mabadiliko rasmi ila inatakiwa kwa sasa tusubirie kwanza wakitupa nakala ya mabadiliko yao ya katiba na kisha tufanyie kazi."anasema Wambura.


Wanachama wa Simba katika mkutano wao huo pia walibadilisha nembo ya klabu hiyo inayoonesha picha ya mnyama Simba akiwa amesimama na badala yake inatakiwa picha  ya akiwa kwa namna yoyote ile ilimradi ni Simba.


Rage akizungumzia mkutano huo anasema kuwa mbali na kuwa wenye mafanikio makubwa lakini umeimarisha hali ya urafiki na amani kwa wanachama.


"Kama mlivyoona kuwa tumebishana hadi kifikia hatua ya kutaka kupigana lakini mwisho wa siku tumepeana mikono na kusalimiana wote kwa pamoja"anasema Rage.
Katika mkutano huo ambapo wanachama walionekana kutaka kuanzisha vurugu baada ya kutoa neno la kejeli kwa kuwaita wanachama hao mambumbumbu lakini walisameheana na kukumbatiana mwishoni.


Rage alionekana akiwa na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba kipindi kilichopita Hasani Dalali wakikumbatiana na kujadiliana masuala mbalimbali kuhusiana na maendeleo ya Simba.
Kwa sasa TFF inasubiria mapendekezo hayo ya katiba kutoka klabu hiyo, Simba ilibanwa na TFF kuhakikisha kuwa inafanyia marekebisho kadhaa katiba yake.
==================

Related

Sticky 4771959228654141486

Post a Comment

emo-but-icon

item