Wasanii, wadau waitetee haiba ya sanaa nchini


Na Evance Ng'ingo
KWA hivi karibuni serikali kupitia Bodi ya Filamu na Baraza la Sanaa la Taifa ilizuia kazi mbalimbali za sanaa za wasanii wa muziki pamoja na filamu.

Msanii Dully Sykes kupitia wimbo wake wa Kabinti Special alikumbwa na adhabu ya kuzuiwa kwa kuoneshwa kwa filamu hiyo.


Dully ambae ni msanii wa muda mrefu katika medani ya muziki wa kizazi kipya hapa nchini alikumbwa na lungu la Basata kufuatia katika wimbo wake huo mwishoni kuna muda anaonekana msanii Nasib Abdul, Diamond akiingia kukumbatiana na Dully Sykes huku akiwa amevalia fulana iliyoandikwa neno la Kejeli kwa askari.


Fulana hiyo imeandikwa neno la kiingereza kwa kejeli kwa askari "Fuck Polis" ambalo ndio limesababisha dosari katika wimbo huo.


Msanii mwengine ambae ni msanii wa filamu aliyekumbwa na adhabu hiyo ni Mahsein Awadh Said, maarufu kama Dk Cheni.


Cheni yeye amekumbwa na adhabu ya kuzuiliwa filamu yake kutokana na kile alichoigiza katika filamu hiyo akisema kuwa amekubali kuolewa.


Jina la filamu hiyo linaitwa Nimekubali Kuolewa jina ambalo limeenekana kuwa ni kikwazo kwa watu wa Bodi ya Filamu na kuamua kuifungua filamu hiyo.


Binafsi mbali na kupongeza juhudi hizo za Bodi ya Filamu katika kusaidia suala zima la nidhamu katika tasnia ya filamu hapa nchini linaimarika.


Ili kuifanya tasnia ya sanaa hapa nchini isimame na kuwa ajira rasmi kama kazi nyingine ni lazima wasanii wenyewe pia kujitambua katika kufikisha ujumbe husika.


Nikisema kuufikisha ujumbe uliokusudiwa nina maana ya kuwa na njia mbadala ambayo haipotoshi maana ya elimu husika ambayo msanii anataka kutoa kwa wanajamii.


Ni imani yangu kuwa msanii Dk Cheni katika filamu yake ya Nimekubali Kuolewa alikuwa anayo nia ya kutoa elimu katika jamii husika.


Ila namna ya kuufikisha ujumbe ndio leo imepelekea kuzuiwa kwa filamu hiyo na Bodi ya Filamu hapa nchini.


Ni vema wasanii wakajenga utamaduni wa kushirikisha wataalamu wengine katika kupitia kazi zao kabla hazijaingia mtaani.


Tena sio tu kabla ya kazi hizo kuingia mtaani ila ikiwezekana kuwa ni hata kabla ya filamu hizo kupelekwa katika Bodi ya Filamu.


Utaratibu wa sasa uliopo ni lazima msanii apeleke filamu yake Bodi ya Filamu ili ikubaliwe ila kwa sasa ni vema wakawa wanashirikisha mawazo ya wasanii wenzao au wadau wengine wa sanaa.


Iwapo Cheni angefanya hivyo ni lazima jina la filamu hiyo kuitwa Nimekubali Kuolewa lisingekuwapo ila kungekuwa na jina jingine lisilokuwa na mkanganyiko wowote.


Jina Nimekubali kuolewa na kwenye kasha la filamu hiyo kuna sura ya Cheni ikimuonesha amevaa kanga na ameweka nywele za kike kichwani.


Hapo harakaharaka picha inayopatikana kwa watu ni kuwa alikuwa akihamasisha ushoga na sio vinginevyo.


Mbali na kuwa kwa sasa tayari Bodi ya Filamu imeshaongelea suala hilo na kumtaka kufanya mabadiliko huku msanii mwenyewe akiwa ameshakubali kufanyia mabadiliko jina hilo,  ila taswira inayoonekana hapa ni kuwa kuna umuhimu wa wasanii kujenga mfumo shirikishi wa kazi zao kabla hata ya kwenda bodi ya Filamu.


Tatizo kubwa lililopo hapa ni kwamba bado wakati wasanii wakiwa wanasema kuwa wanataka mafanikio katika sanaa hasa hiyo ya filamu lakini wao hawabadiliki kiutendaji na kifikra.


Bado wapo wasanii wanaofikiria kuwa wakiwa wanasimamia filamu zao wenyewe kwa kila kitu ndio mafanikio au ndio kuonekana kuwa ni wasanii wazuri.


Utakuta filamu msanii huyo huyo anakuwa mwongozaji wa filamu,mwigizaji, mhariri wa filamu na hata ndio anakuwa anashughulikia masuala yote muhimu.


Hii ni ndio inapelekea kushindwa hata kujua jina zuri la filamu au hata picha nzuri ya kuweka kwenye kasha la mbele la filamu.


Katika filamu hiyo anayopinga masuala ya ushoga Cheni angeweza kuiita jina kama vile Ushoga noma, tupinge ushoga au jina lolote lenye kuleta mantiki ya ujumbe iliokusudiwa.


Kwa upande wa msanii Dully Sykes ambae kesi yake hiyo inatoa elimu pia kwa wasanii wengine, watu wanaweza kusema kuwa mbona kuna video za nyimbo za Bongo Fleva zenye zisizokuwa na maadili ikilinganishwa na hii.


Binasfi video hiyo ya Dully Sykes niliipenda sana na tena ni moja kati ya video ambazo zinavutia kuanzia mwanzo wake hadi hapo ambapo Bodi ya Filamu ilikuja kulalamikia.


Iwapo kampuni iliyorekodi wimbo huo ingeliona hilo la Diamond kuvaa fulana yenye kutukana askari na kuona ubaya wake basi leo hii video hiyo isingelalamikiwa na bodi hiyo.



Hivyo kwa kuwa katika video za muziki ni tofauti na zile za filamu za kuigiza ambapo katika video za muziki asilimia kubwa zinakuwa zinapangwa na waongozaji wa video husika.


Hivyo hao waongozaji wanatakiwa kuwa makini na kazi zao hasa kwa kuhakikisha kuwa kila kitu kinakuwa sawa kwa kuzingatia maadili ya kitanzania na kurekodi video bora.


Hata hivyo walichokifanya wasanii hao Dully Sykes pamoja na Dk Cheni cha kukubali kukosolewa na kuahidi kubadilika ni hatua nzuri katika kuboresha tasnia hiyo hapa nchini.


Naipongeza Bodi ya Filamu kwa kazi nzuri ya kuangalia maadili katika suala zima la picha za muziki na filamu.


Pia hata kwa wasanii ambao wamekuwa wakifuata maadili ya tasnia nzima kwa ujumla.


Lakini pia Bodi ya Filamu sasa kama ilivyotilia mkazo wasanii wa filamu kupeleka filamu zao katika bodi kabla ya kuziingiza mtaani pengine ni vema kwa BASATA kutilia mkazo kwa wasanii kuhakikisha kuwa wanapokea Video za wasanii wa muziki kabla nao hawajaingiza sokoni nyimbo zao.


Kutokana na maendeleo ya teknolojia kwa sasa kuwa makubwa video za wasanii zinaweza kuingizwa moja kwa moja kwenye intaneti na kutumiwa katika mitandao ya kijamii ya Facebook na pengine Youtube na hata zikija kupingwa ni tayari zinakuwa zimeshaonekana kwa wanajamii.


Ilivyo kwa Bodi ya Filamu inawabana wasanii wa filamu kuhakikisha kuwa wasanii hao wanazipeleka kwanza kuangaliwa na ndivyo inavyotakiwa kuwa kwa BASATA waziangalie Video za wasanii wa muziki kabla wasanii hao hawajaziingiza sokoni.


Video ya Kabinti Special hata leo mtu anaweza kuitafuta video hiyo na kuiangalia kama kawaida katika mitandao ya kijamii kwa kuwa huko zimeshaenea sasa ujumbe unazidi kuenea zaidi.


Related

Sticky 904848859676835773

Post a Comment

emo-but-icon

item