Mziiki kuutangaza muziki wa Tanzania =Diamond aipa tafu
http://habari5.blogspot.com/2014/09/mziiki-kuutangaza-muziki-wa-tanzania.html
Na Evance Ng'ingo
KWA sasa biashara ya muziki inazidi kubadilika kila kukicha kutokana na maendeleo katika teknolojia duniani.
Tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na utamaduni wa kutumia zaidi santuri au kanda katika kupata muziki.
Ikaja kubadilika na kuwa zinatumika zaidi Cd katika kujipatia burudani hiyo ya muziki ambapo nayo pia ilikaa kwa muda mrefu kabla ya sasa kuanza kutumika kwa Cm kama njia moja wapo ya kujipatia muziki.
Utamaduni huu kwa sasa unaonekana kuwa unakua kwa kasi kwa kuwa sasa watu mbalimbali wanahifadhi nyimbo katika simu zao za mkononi.
Uhifadhi wa nyimbo hizo unarahisisha suala zima la upatikanaji wa burudani hiyo kirahisi zaidi kwa kuwa mtumiaji anaweza kusikiliza muziki mahala popote pale.
Wengine wanatunza nyimbo zao katika Ipad na kuzisikiliza muda wowote wautakao huku pia kukiwa na wale ambao wanazinunua na kuzitunza kwenye simu kwa njia ya mtandao.
Katika kuendeleza utamaduni huo unaokuwa kwa kasi ndani na nje ya nchi, kwa sasa hapa nchini imezinduliwa huduma iitwayo Mziiki.
Chini ya huduma hiyo ambayo mteja anaweza kuipakua (downloads) katika simu yake ambayo inaruhusu huduma hiyo kufanya kazi.
Kama simu ya mhusika ikiwa imeunganishwa na huduma ya Mtandao basi ni wasaha kwa watumiaji kunufaika na huduma hiyo ya mziiki.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayosimamia huduma hiyo, Arun Nagar, anasema kuwa huduma hiyo ni ya kipekee ikiwa inafanya kazi na wasanii kutoka nchi mbalimbali duniani.
Anasema kuwa ni huduma ambayo imeshasajili nyimbo 900 za wasanii wa nje ya Tanzania huku kwa Tanzania peke yake kukiwa kuna nyimbo za wasanii 200.
"Hii ni bidhaa kwa watanzania na waafrika kwa ujumla kwa kuwa nyimbo zao ndio zitakuwa zikihusika zaidi katika huduma hii"anasema Nagar.
Anaongeza kuwa"wasanii wa Tanzania wanayo nafasi kubwa zaidi katika kuhakikisha kuwa wanatumia fursa hiyo kutangaza nyimbo zao nje ya nchi".
Anaongeza kuwa wameshapewa leseni za kuendesha shughuli hizo katika nchi mbalimbali Afrika na wameshaingia makubaliano na wasanii kadhaa wa kufanya nao kazi.
“Mziiki ni huduma peke yake ambapo mtumiaji anaweza kujinufaisha na huduma nzuri ya muziki kwa bei rahisi zaidi, ikilinganishwa na huduma nyingine"alisema Nagar.
Anaongeza kuwa wasanii wengine wengi wanakuwa hawapo kwenye mazingira mazuri zaidi ya kupeleka nyimbo zao kwenye miradi mikubwa kama I tunes na mingineo hivyo hiyo ni fursa kwao.
Anaongeza kuwa kuna kila aina za nyimbo za kiafrika kama nyimbo za asili, Raggae, Blues, Afro Pop pamoja na nyinginezo.
Anafafanua kuwa bei kusikiliza nyimbo ni bure kabisa kwa kila nyimbo iliyopo ndani ya huduma hiyo isipokuwa kuna bei katika kufanya download ya huduma hiyo.
Kwa hapa nchini Mwanamuziki Nasib Abdul, Diamond Platinum ni mmoja kati ya wasanii waliopata nafasi ya nyimbo zao kutumiwa katika haduma hiyo.
Akizungumzia hatua hiyo anasema kwake ni wakati mwafaka wa kuendelea kupaa zaidi kimuziki kwa kuwa anaimani kuwa nyimbo zake kwa sasa zitasikika dunia nzima.
Anasema kuwa hata wapenzi wa muziki wake wanaweza kusikiliza nyimbo zake zote kwa njia hiyo.
Anaongeza kuwa kwa upande wake ina manufaa kwa kuwa mbali na kujinufaisha kimapato lakini pia inamnufaisha zaidi kisanaa.
Diamond anawataka wasanii wenzake kuhakikisha kuwa wanatumia pia huduma hiyo ya mziiki ambapo wanatakiwa kuhakikisha kuwa inapatikana katika simu zao za mkononi ili waweze kuifaidika nayo zaidi.
Wasanii wengine ambao nao pia nyimbo zao zipo katika huduma hiyo ni akina Rose Mhando, Bahati Bukuku na wengineo.
Huku katika muziki wa Bongo fleva pia kukiwa na wasanii wengine mbalimbali na pia kutoka nje ya Tanzania wapo wasanii wakubwa mbalimbali pia kama vile akina Jazzman Olofin na Ukoo Flani ikiwa pamoja na wengine akina Nonini wa Kenya, Jose Chameleone wa Uganda pia wapo.
Kwa kutumia huduma hizo inasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza fursa ya wasanii kujiendeleza kisanaa.
Hizo ni fursa ambazo wasanii wanatakiwa kuzitumia katika kutafuta soko la nje kwa kuwa hata Ulaya sasa wanaweza kujikuta nyimbo zao zikitumika kirahisi zaidi.
Wasanii wengine wanasambaza nyimbo zao au hata video zao katika huduma za simu kama vile Whastup, Istagram na huduma nyingine za mitandao.
Kinachotakiwa kwa wasanii wenyewe kujua ni kwa namna gani watanufaika na huduma hizi katika kutanua wigo wa kazi zao kwa ajili ya kujikwamua kwenye matatizo yanayomkuta.
Kwa sasa wa Ulaya tayari washajua hilo na wameweka mikakati ya kukuza vipato vyao
HIVI majuzi Jarida la Forbes lilitoa orodha ya wasanii wa muziki wa Hip Hop ambao wanaongoza kwa utajiri duniani.
Kati ya wasanii hao ambao wote kwenye kumi bora ni wasanii kutokea Marekani ambao wametajwa na vyanzo vyao vya utajiri.
Mwanamuziki wa muziki huo ambae pia ni Mtayarishaji wa Muzikim Dr Dre ndio aliibuka kinara kwa kuwa na kitita cha Dola za Kimarekani Milioni 620.
Hiyo ilitokana na kutumia fursa kama hizo za kuutangaza zaidi muziki wake katika kujiongezea kipato.
Mradi wa Mziiki umeitwa jina hilo ili kutoa taswira yenye mvuto zaidi kwa watu katika kulitaja jina hilo.
Iwapo wakisema Mziiki inakuwa ina mvuto zaidi katika kulisema jina hilo tofauti na kama ingeitwa Muziki ambalo ni jina halisi kisarufi.
========================