TRACE Music Star ilete neema ya muziki hapa nchini
http://habari5.blogspot.com/2014/10/trace-music-star-ilete-neema-ya-muziki.html
Yamoto Bendi akitoa burudan kwenye uzinduzi huo |
Mkurugenzi wa Masoko wa Airtel akizungumza siku hiyo |
Na Evance Ng'ingo
KWA sasa, fani ya muziki imekuwa ikiendana na mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa yamesaidia kukuza fani hiyo.
Kumekuwa na matumizi ya mitandao mbalimbali katika kutoa huduma ya muziki ambayo kwa sasa imeshazoeleka.
Kwa sasa mitandao ya kijamii kama You tube imekuwa ikionesha kabisa na video za wasanii mbalimbali wakifanya kazi zao. Zipo hata huduma za muziki kwa njia ya simu ambazo zinatumiwa na wadau kadhaa kujipatia burudani.
Lakini kwa kuwa kazi hizo zote zinafanywa na wasanii, wasanii nao haohao wamekuwa pia wakikabiliana na matumizi hayo ya teknolojia katika kujitangaza.
Kwa kuwa wasanii hata wakubwa wanatokana au wanaanzia kwenye uchipukizi, hivyo kumekuwa na mikakati mbalimbali ya kuwaibua chipukizi wenyewe.
Kwa sasa hata wasanii chipukizi pia wamewekewa mikakati mizuri ya kuvumbua vipaji vyao.
Mikakati hiyo ambayo pia ni ya kiteknolojia imekuwa ni rahisi katika kupata na kuendeleza vipaji vya wasanii.
Mradi wa Airtel Trace Music Star unaoendeshwa kupitia Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel ni moja kati ya mikakati ya kisasa katika kuinua vipaji.
Mradi huo una lengo la kukuza vipaji vya muziki na kuwawezesha wanamuziki chipukizi wa Kitanzania kujulikana katika anga za muziki duniani
Hatua hiyo inatokana na ushirikiano kati ya Airtel na Kampuni Muziki ya Trace ambayo imekuwa ni msingi mkubwa wa kuendeleza sanaa ya muziki duniani.
Trace pia inamiliki chaneli ya muziki ya Trace, ambayo kwa sasa ni moja ya chaneli kubwa za muziki zinazoheshimika zaidi duniani.
Lakini pia ili kutimiza ndoto za wasanii wanaotaka kuibukia katika medani ya muziki, pia ameshirikishwa msanii wa Marekani, Akon.
Mradi huo sio tu kwa wasanii chipukizi au wasanii wa Tanzania peke yake, ila pia unahusisha wasanii kutoka nchi 13 za Afrika.
Mkurugenzi wa Masoko wa Airtel, Levi Nyakundi anasema kuwa mpango huu unaenda sambamba na dhamira yao ya kuwawezesha vijana wenye ndoto ya kuwa wanamuziki bora kuonesha uwezo wao kuwawezesha kufikia ndoto zao.
“Tunafahamu kuwa Tanzania ina vijana wengi wenye vipaji vya muziki, lakini hawajajulikana katika anga za muziki na ndio maana leo tunazindua programu hii na kuwawezesha kujiunga kirahisi kupitia simu yake ya mkononi na kushiriki Airtel Trace Music Stars na kuibuka kuwa wanamuziki bora,” alisema Nyakundi.
Alisema watakaochaguliwa kutoka Tanzania wataungana na wa nchi za Kenya, Uganda Zambia, Madagascar, Malawi, Nigeria, Ghana, Burkina Faso, Chad, Congo Brazzaville, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Gabon.
Aliongeza kuwa, “waimbaji bora kutoka kwenye kila nchi watachaguliwa na kuzawadiwa baada ya kuingizwa kwenye mashindano yatakayowashirikisha waimbaji bora kutoka nchi nyingine ili kupata mshindi atakayetwaa taji la mwanamuziki mwenye kipaji bora Afrika.”
Hivyo hiyo ni fursa kubwa kwa vijana nchini kujipanga kuhakikisha kuwa wanakabiliana na ushindani huo.
Kwa kuwa mshindi wa Afrika, atajishindia zawadi mbalimbali ikiwemo kurekodi na kusambaziwa nyimbo zake chini ya studio duniani pamoja na kufaidika na mafunzo ya kufuliwa kimuziki na nguli wa muziki wa Amerika, Akon hivyo hiyo sio bahati ya kupoteza.
Ikumbukwe kuwa kushindana ni rahisi mno kwa kuwa mshiriki anatakiwa kuhakikisha kuwa anapiga simu namba 0901002233.
Kwa kupiga namba hiyo na kisha kuanza kuimba inakuwa ni fursa kubwa kuonesha kipaji chake kirahisi zaidi.
Haina tofauti sana na mfumo uliokuwa ukitumiwa kwenye shindano la Bongo Star Search (BSS) ambapo wasanii kama akina Menina Atick ndio waliopatikana na kwa sasa wanasikika karibu kila kona ya Tanzania.
Kama alivyochaguliwa msanii huyo kwa njia ya kura ndivyo kwa washiriki hao watachujwa na kisha kutangazwa namba zao za upigaji wa kura na wengine kupiga kura kwa njia ya tovuti.
Iwapo miradi kama hiyo ingeanza mapema ni dhahiri kuwa ingekuwa imeshaibua vipaji vya wasanii mbalimbali wa hapa nchini ambao wangewakilisha vema nje ya nchi.
Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura, Lady Jaydee anayachukulia hayo ni kama mashindano ya pekee yanayotoa fursa kwa kijana yeyote ambaye angependa kuwa staa kushiriki.
“Nawahamasisha vijana kuchangamkia fursa hii kwa kurekodi freestyle yako ya fleva yoyote kali kupitia simu yako na kutuma nyimbo yako ili kujaribu zali lako,” anasema Lady Jaydee.
Anaongeza kuwa, “Pia napenda kuwaomba mashabiki na wapenzi wa muziki kuwapigia kura washiriki hawa kwa wingi ili kuweza kumpata ushindi. Kwa wanamuziki chipukizi mashindano haya si yakukosa maana wewe pia unaweza kuibuka kuwa staa wa Airtel Trace Music Star kwa njia rahisi tu Piga, Imba, Shinda.”
Naye Ambene Yesaya 'AY’ anasema amekuwa akihangaikia fursa kama hizo za kutafuta soko la kimataifa.
Anawataka vijana wa Tanzania kutambua kuwa kwa sasa zipo fursa nyingi katika muziki ambazo zinatakiwa kutumiwa vema.
“Wakati sisi tunaanza muziki, hali ilikuwa tofauti sana kwa kuwa tulikuwa hakuna mwanga wa kutosha kutuonesha nini cha kufanya katika muziki,” anasema AY.
Anaongeza kuwa, “sasa hali ni tofauti sababu mwanga upo kama hivi unaweza rekodi na Akon hivi hivi wakati sisi ni mzuri wako ili angalau kuanza kutoka kisanaa sasa kazi ni kwao vijana wenyewe.”
Msanii Menina Atik anasema kuwa hata kwa upande wake alipata umaarufu kupitia njia kama hiyo ya kupiga simu na kuibuka kama mshindi aliyeingia moja kwa moja kwenye kinyang'anyiro cha BSS kwa njia ya simu.
Utamaduni wa kuendeleza muziki kwa njia za kisasa unazidi kukua kwa kasi nchini na mbali na huduma hiyo ya Trace, lakini pia imeshuhudiwa huduma ya Mziiki yenye kumwezesha mtumiaji wa simu kupata nyimbo mbalimbali, huduma ambayo imezinduliwa nchini hivi karibuni.
********************tamati************
annet