Swahili Fashion 2013 ilivyokuwa
http://habari5.blogspot.com/2013/12/swahili-fashion-2013-ilivyokuwa.html
Swahili Fashion ya 2013 ilivyokuwa
NaMtaalamu wa Mitindo
MOJA kati ya matukio makubwa yaliyotokea mwaka huu katika medani ya Mitindo ni pamoja na kufanyika kwa onesho la Mavazi la Swahili Fashion ambalo lilifanyika kwa siku tatu.
Katika onesho hilo lililowashirikisha wabunifu ndani na nje ya nchi kulikuwa pia na utoaji wa tuzo mbalimbali za washindi wa vipengele vilivyokuwa vikigombaniwa.
Kwa mwaka huu onesho la Swahili fashion linaonekana kuwa na mvuto zaidi hasa ikilinganishwa kuwa kulikuwa na wabunifu kutoka nchi nyingi ambao na walionesha kazi nzur.
Wabunifu kutoka Zambia, Kenyam Uganda, Msumbuji, Namibia, Afika Kusini, Ghana, Jamhriya Zchek na nyinginezo.
Akizungumzia onesho hilo kwa mwaka huu Mwandaaji wa onesho hilo Mustapha Hasanali anasema kuwa kwa mwaka huu wabunifu wengi wameonesha kazi zao mpya tayari kwa mwa ujao.
Anasema kuwa wabunifu wameonesha uwezo katika kununi ambapo kila kazi iliyooneshwa inaweza kuwa na manufaa pia kwa watanzania.
Alisema kuwa wabunifu wa nje takribani 15 wameonesha mavazi yao katika onesho hilo.
"Najua kwa sasa Swahili Fashion imewagusa watu wengi sana kwa kuwa ni onesho kubwa katika Afrika Mashariki na Kati na hivyo linazidi kukua na kuwapata wabunifu wengi kutoka sehemu mbalimbali"anasema Mustapha.
Anasema kuwa onesho la Swahili fashion limewatambulisha wabunifu wa kitanzania mbalimbali katika ulimwengu wa masuala ya fashion duniani.
"Hili ni moja kati ya mashindano yanayokubaliwa sana hapa nchini na hata nje ya nchi kutokana na umakini wake wa uandaaji lakini pamoja ni kutokana ukubwa wake"anasema Mustapha.
Anaongeza kuwa Swahili Fashion inatakiwa kutumiwa vema na wadau wote wa masuala ya Mitindo nchini katika kujitangaza ndani na nje ya nchi.
Anasema kuwa inatakiwa kwa sasa wabunifu wa kitanzania kuhakikisha kuwa wanatumia onesho hilo sio tu kutangaza biashara zao lakini pia kuhakikisha kuwa wanaongeza hamasa kwa watanzania ya kuvaa mavazi yaliyobuniwa hapa nchini.
Kwa upande wake Mbunifu Bora wa mwaka 2013, Evelyn Rugemalila anasema kuwa kupitia onesho la Swahili Fashion watanzania wanapata nafasi ya kuwajua zaidi wabunifu wao.
Anasema kuwa hili likifanikiwa inabakia kuwa ni kazi kwa wabunifu wa hapa nyumbani wenyewe kutumia fursa zilizopo ktaika tasnia hiyo.
Anasema kuwa kwa sasa watanzania wamehamasika kuvaa mavazi yaliyobuniwa na wabunifu wa hapa nyumbani ambapo wanashonesha magauni kutoka kwa wabunifu hao wa ndani.
Anaongeza kuwa kwa upande wake akiwa kama mbunifu wa bora wa mwaka huu amefikia hatua hiyo kutokana na kazi zake alizowabunia watu ambao ni watanzania wanaopenda na kuthamini kazi za wabunifu wa hapa nyumbani.
"Kupitia maonesho kama haya ya Swahili Fashion na mengineo ni wakati wa wabunifu kujuana na kufanya kazi kwa pamoja lakini pia ni fursa ya kuwapata wateja wetu"anasema Evelyn.
Kwa upande wake mbunifu mwengine ambae anamiliki lebo ya Zaidi Afrika Zamda George ambae amekuwa akijihusisha na tasnia ya ubuinifu kw atakribani miaka mitano anasema kuwa Swahili fashion ni jukwaa la kujikuza kibiashara zaidi.
Anaongeza kuwa kwa sasa wadau wengi wa harusi wanatengeneza nguo zao kwa wabunifu wa ndani hasa magauni ya Harusi.
Anaongeza kuwa kwa kupitia onesho la Swahili Fashio alijitangaza zaidi na kuimarisha biashara zake na kwa sasa anashona gauni moja la Harusi kwa laki 8 huku nguo ya kawaida ya kima cha chini ni 50,000/=
" Kwa kawaida natumia wiki mbili kukamilisha gauni la Harusi na ambalo linakuwa imara na lenye mvuto na kwa sasa ubunifu wa mavazi hapa nchin ni biashara ambayo nadhani inatakiwa kutazamwa kwa jicho la pili kwa kuwa inaweza kuwa na faida sio tu kwetu lakini hata kwa nchi pia"anasema Zamda.
Katika onesho la mwaka huu pia kulikuwa na utoaji wa tuzo kwa washindi wa vipengele mbalimbali ambavyo vinahusiana na masuala ya mavazi.
Tasnia ya uanamitindo ikiwa ni moja kati ya tasnia ambayo ipo karibu zaidi na ubunifu wa mavazi nayo pia kulikuwa na shindano la kutafuta wanamitindo bora wa kike na kiume.
Kwa upande wa kipengele cha Mwanamitindo bora wa kiume nafasi ilichukuliwa na Lota Mollel huku wa kike ikichukuliwa na Winfrida Ngonyani.
Akizungumza na gazeti hili Mwinfrida ambae aliwahi kuwa Miss Universe mwaka jana anasema kuwa kwake kupitia Swahili Fashion anajiongezea fursa mbalimbali za kujiongezea kipato.
"Mimi ninaona kuwa Swahili Fashion imenifungulia njia kwa kiasi fulani kwa kuwa ninapata fedha mbili tatu kama model lakini pia nimejiongea wigo wa kufanya kazi mbalimbali na watu tofautitofauti."anasema Winfrida.
Moja kati ya vipengele 18 vilivyoshindaniwa katika tuzo hizo ni pamoja na Mbunifu Bora Chipukizi ambapo mwanadada kutoka nchini Kenya Bhoke Samuel alishinda.
Katika kipengele cha mbunifu chipukizi kama hicho pia kiliwahi kushindaniwa miaka ya nyuma na wabunifu walioshinda wengine wao wameendelea kufanya vema zaidi hadi mwaka huu.
Mfano mzuri ni Grace Kijo ambae aliwahi kushiriki mwaka 2009 kama mbunifu chipukizi lakini kwa mwaka huu 2013 ameingia pia kama mbunifu mkubwa tu na kuonesha nguo nzuri.
Anasema kuwa kwa mwaka anabuni zaiid nguo za kike na kuongeza kuwa anajipanga kuhakikisha kuwa anatumia jukwaa la Swahili Fashion kufika mbali zaidi katika tasnia ya ubunifu.
"Kwa kuwa kwa sasa nikijilinganisha na miaka ya nyuma naona kuwa nimepiga hatua na ndio maana mwaka huu hata ukiangalia na miaka iliyopita kwa mwaka huu kazi yangu inaonekana kuwa imeimarika zaidi"anasema Grace.
Katika onesho la Swahili Fashion la mwaka huu wabunifu wengi walionekana kuendelea kukipa kitenge nafasi zaidi kwa kukitumia katika kunakshi kazi zao za sanaa.