Lelo: Mtanzania azungukae dunia kwa kutumia baiskeli, lengo ni kudhamini wanafunzi kupata elimu ya chuo kikuu, Tigo yajitosa kumsaidia

Hapa alikuwa nchini Brazil

Akiwa Peru na askari katika eneo la mpakani

Hapa akiwa anaendelea na safari zake


Ndo huyu kijana mwenyewe


KIJANA Elvis Munis (26) amebadilisha mtazamo uliojijenga kwa watu wengi kuwa wazungu peke yao ndio wanaweza kuchangisha fedha au kuhamasisha vita dhidi ya masuala mbalimbali katika jamii kwa kuzunguka dunia nzima.

 Munis ambaye jina lake maarufu ni Lelo alianza harakati za kuzunguka nchi mbalimbali duniani kwa kutumia usafiri wa baiskeli lengo likiwa ni kuchangisha fedha za kusomesha vijana wenzake ikiwa ni pamoja na kuhamasisha suala zima la utunzaji wa mazingira.

 Kijana huyo alianza safari yake kutokea mkoani Kilimanjaro na aliamua kuanzisha ziara zake hizo nchin Peru. Lengo lake ni kuchangisha milioni 150 kwa ajili ya kuwawezesha vijana wenzake kupata elimu ya juu. 

Hata hivyo wakati akianza harakati hizo hakuwa peke yake alikuwa na wenzake ambao hata hivyo waliishia njiani kwa kuwa walikuwa na majukumu yao mengine mengi zaidi kama vile kusoma na mengineyo. 

Wenzake hao hawakuwa na jukumu la kuzunguka dunia badala yake walikuwa wakitakiwa kuchangisha wakiwa hapa hapa nchini na kilichotokea kwa upande wa Lelo anasema kuwa alihamasika zaidi kuchangisha fedha hizo. 

Lelo kabla ya kuanza  ziara yake hiyo alikuwa akifanya kazi kama msaidizi wa watalii akiwasaidia kubeba mizigo yao kupanda na kushuka milimani hasa Mlima Kilimanjaro kufanya kazi zao za kitalii. 

Aliipatia kampeni hiyo jina la from Kili to Chile akiwa na maana ya kuwa kampeni hiyo inaanzia Mlima Kilimanjaro kuelekea Chile na ndipo alipoamua kuanzia safari yake hiyo Peru. 

Ilimlazimu kutumia usafiri wa ndege kutoka Tanzania kuelekea Afrika Kusini na kisha kuchukua Viza ya kwenda Peru ambapo alianza safari yake hiyo kwa kutumia baiskeli. 

Akiwa Peru alianza ziara yake ya kuzunguka kwenda nchi zote za Amerika ya Kusini huku njiani akiwa anatoa elimu ya masuala ya mazingira pamoja na pia kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia suala hilo la elimu. 

Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita kwa njia ya mtandao wa kijamii wa Skype akiwa nchini Liberia, Lelo anasema kuwa kwa sasa amemaliza ziara za bara la Amerika na ameanza ziara ya nchi za bara la Afrika. 

Anasema kuwa alipokuwa barani Amerika Kusini alikumbana na changamoto mbalimbali. 

Anasema kuwa haikuwa rahisi kwa watu wa kawaida katika nchi hizo kumuelewa kwa kuwa inaonekana kuwa ni utamaduni ambao ni mgeni kwao. 

Anatolea mfano kuwa katika nchi kama vile Brazil alikuwa akipata shida zaidi kutoka kwa wananchi hususan maeneo ya vijijini alikokuwa akipita. 

Anasema kuwa wapo waliokuwa wakimhisi kuwa ni mhusika wa biashara ya dawa za kulevya kutokana na hata njia alizokuwa akipita kutoka nchi moja na nyingine. 

Anasema kuwa kuwa ilikuwa ni safari kubwa yenye changamoto nyingi kuanzia baridi kali njiani, na muda mwengine kulazimika kulala porini mahala ambapo alikuwa hata hapajui. 

Anafafanua zaidi kuwa kila anapoenda anatumia hema analotembea nalo katika nchi mbalimbali akiwa amelifunga katika baiskeli yake. 

Anaongeza kuwa akifika mahala popote akitaka kupumzika anaamua kulifunga na kisha kulala katika hema hilo.

 "Nikiwa njiani na kujiona kuwa nimechoka na siwezi kuendelea na safari zangu, huwa ninaamua kufunga hema na kulala njiani hasa pale ambapo ninaona kuwa nipo sehemu isiyokuwa na hoteli," alisema Lelo.

 Anaongeza kuwa kwa upande wake anatumia dola tano hadi saba kwa siku kwa ajili ya mlo na pale ambapo anakuwa kwenye miji mikubwa analazimika kulala kwenye gesti za bei ya chini kabisa. 

Anaongeza kuwa hadi sasa amefanikiwa kukusanya milioni 25 kutoka katika harakati zake hizo, fedha ambazo amezipata kutoka kwa wadau mbalimbali. Akizungumzia namna ambavyo anazikusanya fedha hizo, Lelo anasema kuwa akiwa katika kila nchi anakusanya kuanzia dola 2 na kuendelea na anawahamasisha wananchi kwa njia mbalimbali kukusanya fedha hizo. 

Ni fedha ambazo akishazikusanya anazituma moja kwa moja katika shirika la Conservation Research Center (CRC) lililopo Arusha lenye jukumu la kupitia maombi ya wanafunzi wanaotaka kupatiwa udhamini huo. 

Anasema kuwa pia amezunguka nchi za Marekani na Canada na pote huko amekuwa akipatiwa misaada mbalimbali. 

Akizungumzia ziara zake kwa nchi za Afrika ambapo ndio ameanza kwa sasa anasema kuwa akitoka Liberia anaelekea Siera Leon na kisha kuelekea nchi nyingine za Ghana, Nigeria na nyinginezo. 

Lelo anasema kuwa anaona kuwa akiwa katika ziara yake kwa nchi za Afrika anakabiliwa na changamoto ya kutembea katika misitu, na majangwa pengine kukutana na wananchi wenye roho nzuri na hata mbaya.

 Anatarajia kuzunguka nchi 15 za Afrika na Juni mwaka huu atamalizia ziara yake kwa nchi za Kenya, Uganda, Burundi na kisha kufikia Tanzania. Anafafanua kuwa mara nyingine anakabiliwa na magonjwa  mbalimbali kama vile malaria na mengineo ambapo hulazimika kulipia gharama za matibabu.

Lelo anaongeza kuwa baiskeli anayoitumia kwa sasa ni ya pili ambayo amekuwa akiitumia kuzungukia nchi za za Ulaya na Amerika, baada ya baiskeli ya kwanza kuibwa akiwa katika harakati za kuanza ziara yake akitokea Tanzania kwenda Afrika Kusini.


Lakini kwa nini kijana huyu emeamua kutumia baiskeli kufanya kazi yake hiyo, anasema kuwa akiwa kama mwanaharakati wa mazingira ameamua kutumia baiskeli. 


Anasema kuwa baiskeli haitumii mafuta na inatumia zaidi nguvu zake mwenyewe na akiwa kama mwanaharakati wa mazingira anaona kuwa gari lisingeonesha uhalisia wa harakati zake hizo za kuyapigania mazingira. 

Lakini harakati za kijana huyo zinaungwa mkono na Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo ambao wamempatia milioni 16 kusaidia harakati zake hizo. 

Meneja Mawasiliano wa Tigo, John Wanyancha anasema kuwa harakati za kijana huyo zinatakiwa kuungwa mkono kwa kuwa ameonesha nia ya dhati ya kusaidia elimu na mazingira lakini kwa kutumia njia za kishujaa.

 "Yani huyo kijana anaonekana kuwa anatumia baiskeli yake kuchangisha fedha za kusaidia watu wengine na sisi kama Tigo tunamuunga mkono kwa kumwezesha yeye kufanya kazi yake hii vema zaidi," anasema Wanyancha. 

Anaongeza kuwa huo ni utamaduni wa aina yake kuona kijana wa kitanzania akitumia muda wake nguvu na ujasiri kuzunguka katika nchi ambazo kwanza inawezekana hakuwa amewahi kufika lakini ndio anaenda kwa mara ya kwanza na kuchangisha fedha za kusaidia Watanzania wenzake. 

Anasema kuwa Tigo imeguswa na harakati hizo hasa wakiwa kama wadau wakubwa wa masuala ya maendeleo ya elimu nchini.

 "Katika kufanikisha adhma ya kumsaidia kijana huyu sisi kama tigo tumeanzisha namba hii ya 0716 407057 ambapo kama kuna mwenye kuhitaji kusaidia harakati za Lelo ajitokeze na kumtumia mchango wake kwa njia ya Tigo pesa " alisema Wanyancha.

Related

Sticky 4508028431739116129

Post a Comment

emo-but-icon

item