LUPITA NYONG’O: Binti Mkenya aliyeingia kwa kishindo Hollywood





.Avuta wengi kwa filamu yake na akina Brad Pitt
.Ni binti wa wanasiasa mahiri Prof. Anyang Nyong’o
.Apania makubwa baada ya kuipamba kazi ya bil. 32/-
Na Mwandishi Wetu


LUPITA NYONG’O mtoto Seneta wa nchini Kenya ambae kwa sasa anatamba katika medani ya siasa nchini humo akiwa kama Seneta.


Nyong’o si jina geni hata kidogo katika medani za siasa Ukanda wa Afrika Mashariki. Huyu ni mwanasiasa machachari na msomi wa Kenya aliyeshika nyadhifa kadhaa ikiwa pamoja na Uwaziri katika utawala wa Mwai Kibaki.


Kufikia Machi mwaka huu, alikuwa Waziri wa Afya.Na baada ya uchaguzi mkuu uliomweka madarakani Uhuru Kenyatta, Nyong’o kwa sasa ni Seneta.


Licha ya umaarufu alio katika siasa na pia kitaaluma, jina la Nyong’o limepata msukumo mpya utakaoendelea kulifanya lidumu na kupata umaarufu zaidi duniani.
Safari hii ni kupitia binti yake, Lupita Nyong’o ambaye nyota yake imeanza kung’ara katika tasnia ya filamu.


Binti huyo msomi, ingawa hajafikia ngazi ya baba yake ya kuwa msomi wa shahada ya uzamivu, amebahatika kung’ara katika filamu yake ya kwanza ndani ya Hollywood, 12 Years A Slave.
Tayari filamu hii iliyowashirikisha mastaa kadhaa akiwemo Brad Pitt, imeshakuwa gumzo na hata kuingizwa katika tuzo za ubora.


Lupita amejipatia umaarufu mkubwa kutokana na jinsi alivyoicheza kwa ustadi filamu hiyo ya bei mbaya ambayo maandalizi yake yamegharimu dola za Kimarekani milioni 20 (sh bilioni 32).


Alicheza filamu ya kwanza ya East River mwaka 2008, kabla ya kuibuka na 12 Years A Slave na sasa akiwa katika hatua za mwisho za kuivisha filamu ya Non-Stop itakayoachiwa mwaka kesho. Aidha, mwaka 2009 aling’ara katika tamthilia ya Shuga.


“Mungu ni mkubwa. Hatimaye ndoto zangu zimeanza kuwa kweli. Kwa kuwa nimeingia Hollywood na mguu mzuri, sitapenda kubweteka.


 Ni kazi tu sasa mpaka dunia ijue kuna vipaji katika kila kona ya dunia, ikiwa pamoja na Kenya,” anasema binti huyo aliyezaliwa Mexico ambaye baba yake alikuwa anafundisha katika vyuo vikuu vya huko, akakulia Kenya na baadaye kusoma Marekani alikoanza kufanya kazi kwa kishindo.

Ingawa jina lake linaanza kung’ara kimataifa, hata hivyo Lupita si mgeni katika tasnia ya filamu, kwani baada ya kujikita darasani kusomea sanaa katika vyuo vya elimu ya juu vya Hampshire na Yale, alifanya kazi kama mwongoza filamu.


Alishiriki pia kutengeneza filamu kadhaa mahiri, zikiwemo  The Constant Gardener ya mwaka 2005 iliyoongozwa na Fernando Mereilles na nyingine, The Namesake ya mwaka 2006 iliyoongozwa na Mira Nair.


Na baada ya kuongoza kwa muda mrefu, ameamua kujikita `mzima mzima’ katika kuigiza, akianzia na 12 Years A Slave yenye wakali wa Hollywood kama Brad Pitt, Chiwetel Ejiofor, Benedict Cumberbatch, Michael Fassbender, Paul Giamati na Alfre Woodard.


Katika filamu hiyo, Lupita aliyeigiza kama Patsey anacheza kama binti aliyetekwa New York na kuuzwa kama mtumwa huko Louisiana katika ya miaka ya 1850. Katika filamu hiyo, Patsey anaonesha uchakaramu wa kila aina, akisaka mbinu za kutoroka aweka kurudi nyumbani.


Utukutu wake huo ulimsababishia adhabu kadhaa, na wakati mwingine akiangukia katika mitego ya mapenzi ya `mabwana’ waliowasimamia watumwa. Inavutia kuitazama na inathibitisha gharama halisi ya sh bil. 32. Filamu hii imetengenezwa kwa wiki saba, kuanzia Juni 27, 2012 na ilimaliziwa Agosti 13 mwaka huu.


“Sasa iko mtaani. Nimefurahi sana kuona imepokelewa vizuri. Kitendo cha kuingizwa katika Tamasha la Filamu la Kimataifa la Toronto ni heshima nyingine ya kipekee,” anasema binti huyo ambaye pia akiwa Kenya alicheza filamu ya `In My Genes’  inayozungumzia tatizo la ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, yaani albino.


Huyo ndiye binti wa Kenya, Lupita Anyang Nyong’o ambaye licha ya kutoka katika familia maarufu, yeye mwenyewe ameamua kujitengenezea umaarufu kupitia filamu, na hakika kwa jinsi alivyoanza, ana nafasi kubwa ya kutamba katika tasnia hiyo duniani. Hata hivyo, kwa sasa ni jambo la kusubiri na kuona.


Maoni

Wasanii wengi wenye asili ya Kenya wanaonekana kujitambua zaidi kutokana na namna ambavyo wanaichukulia sanaa kwao ni kama kazi.

Lupita alijijua kuwa anacho kipaji na ndio maana ameweza kufika mbali katika medani ya sanaa akiwa ugenini nchini Marekani.


Je hivi wasanii wetu wa hapa nyumbani au hata wale ambao wamefikia hatua ya kuishi nje ya nchi wanalo angalau wazo la kuhangaikia anga la kimataifa la uigizaji wa filamu?


Lupita mbali na kuwa mtoto wa aliyekuwa waziri wa Afya wa Kenya lakini aliiona fursa na akaikimbilia kwa kuwa mwenyewe anasema kuwa alisikia kuwa kuna usaili na akajaribia humo humo na hadi leo nyota yake imeng'aa.


Tujitume watanzania huku tukitambua kuwa ubunifu unaweza kutuletea manufaa ya baadae na kujikuta tukiitangaza nchi yetu pia.

Related

Sticky 384318434699811587

Post a Comment

emo-but-icon

item