Yanga "Ligii hii ni cha mtoto kwetu"
http://habari5.blogspot.com/2014/01/yanga-ligii-hii-ni-cha-mtoto-kwetu.html
KOCHA wa Yanga Hans van der Pluijm amesema kuwa ana imani kuwa kikosi chake kitafanya vema katika mzunguko wa pili wa ligi unaonza leo.
Yanga ambayo kwa sasa inaongoza ligi kwa inafungua dimba katika mchezo utakaochezwa leo kwenye uwanja wa Taifa dhidi ya Ashant United.
Akizungumza na gazeti hili kocha wa huyo wa Yanga alisema kuwa anakiona kikosi chake kipo katika hali nzuri kimchezo wa leo na ligi nzima kujumla.
Alisema kuwa kutokana na mazoezi waliyofanya nchini Uturuki yamewapa imani ya kufanya vema katika michezo yote ya ligi.
Alisema kuwa akishirikiana na kocha wake msaidizi Charles Mkwasa wachezaji wa kikosi hicho wamenolewa katika kila idara kuanzia ushambuliaji, ulinzi na wamefuzu kushiriki vema ligi hiyo.
"Wachezaji wapo katika hali nzuri na hakuna majeraha na tunataka kuona kuwa kila kitu kinaenda sawa na kutete ubingwa wetu katika mzunguko huu wa pili"alisema Van.
Wakati huo huo katika tovuti ya klabu ya Yanga kuna taarifa inayoonesha kukatishwa tamaa na hatua ya kuzuliwa kwa mchezaji Emanuel Okwi wakati dirisha la usajii likiwa limefungwa.
Taarifa hiyo iliyopo kwenye tovuti hiyo imeweka wazi hati ya uhamisho na mawasiliano yaliyofanyika kati ya klabu hiyo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Taarifa hiyo ilielezea kuwa uongozi wa klabu ya Young Africans umeamua kuweka hadharani ukweli kuhusiana na usajili wa mshambuliaji wake wa kimataifa kutoka nchini Uganda Emmanuel Okwi ambaye kamati ya maadili na hadhi za wachezaji imemzuia kuichezea Young Africana mpaka watakapopata uthibitisho kutoka FIFA.
Ilifafanua kuwa Young Africans ilikamlisha usajili wa mshambuliaji huyo tangu Disemba 15 mwaka 2013, na kupata hati ya uhamisho wake wa kimataifa (ITC) ambayo iliwasilishwa TFF pamoja na fomu mama za usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom.
Ilionesha kuwa baada ya kukamilisha zoezi hilo TFF ilipitisha jina lake kwa kutupatia leseni no: 921225001 ambayo inamruhusu mchezaji kuichezea Young Africans na kisha kulituma CAF Disemba 31, 2013 kwa ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika ambapo CAF nao walimuidhinisha kuwa mchezaji halali wa Young Africans kwa mashindano hayo.
Akifafanua zaidi taarifa hiyo Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kiziguto alihoji uhalali wa Kamati ya Maadili na Hadhi za Wachezaji kuchukua maamuzi hayo sasa wakati ilikuwa na muda wa kitosha tangia Disemba 15 mwaka jana ambapo usajii ulikamilika.
"Cha kustaajabisha siku mbili kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Kamati ya Maadili na hadhi za wachezaji wakamzuia mchezaji huyo kuichezea Young Africans ilihali akiwa ameshaidhinishwa na TFF na CAF kuwa mchezaji halali wa Young Africans".alisema Kizuguto.
"Kinachoshangaza ni kwamba wanakuja kutoa maamuzi hayo mwezi mmoja na nusu baada ya dirisha la usajili kufungwa, ikiwa ni siku mbili kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom".alihoji Kiziguto.
Okwi anachukuliwa kama msaada mkubwa kwa timu yake hiyo ya Yanga katika mzunguko huu wa pili wa ligi unaoanza leo.
Kuzuiwa kwake kucheza kunaonekana kuwa ni pigo kwa Yanga ambayo ilikuwa ikimtegemea kama mmoja kati ya washabuliaji wake muhimu kwenye ligi hii inayoanza leo
Mwisho