Mtanzania endesha baiskeli Ulaya, Amerika na Afrika kuchangisha fedha za elimu
http://habari5.blogspot.com/2014/01/lele-aendesha-baiskeli-ulaya-amerika-na.html
Mtanzania Elvis Munis (26) wa mkoani Kilimanjaro mwenye lengo la kuzunguka katika nchi za bara la Ulaya, America, Asia na Afrika kuchangisha doal laki moja kusaidia elimu kwa sasa amefikia nchini Liberia.
Kijana huyo ambae ni maarufu kwa jina la Lelo ni mwenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro na alianza harakati zake mwaka 2011 akianzia Afrika Kusini na anatarajia kumaliza safari yake hiyo Juni mwaka huu kwa nchi za Afrika Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi ya kampuni ya Mahusiano ya Frontline Potter Noveli kwa njia ya mtandao wa Skype, Lelo alisema kuwa akiwa katika nchi hizo ambazo amepita amefanikiwa kuchangisha dola elfu 14 kutoka kwa wasamalia wema mbalimbali.
Alisema kuwa fedha hizo zote zinatumwa kwa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Conservation Research Center (CRC) lenye jukumu la kupitia maombi ya wanafunzi wanaotakiwa kusaidiwa.
Alisema kuwa akitoka nchini Liberia ambapo yupo kwa sasa ataelekea nchini IIvory Coast, Ghana na nyinginezo za Afrika Magharaibi kabla ya kuja kumalizia ziara yake Afrika Mashariki mwezi Juni mwaka huu.
Aliongeza kuwa katika nchi anazokuwapo anatumia usafiri wa baiskeli kutoka nchi moja kwenda nyingine isipokuwa pale anapotakiwa kuvuka kutoka bara moja kwenda jingine.
Akizungumzia wito wake kwa watanzania katika suala zima la elimu alisema kuwa ili kuleta mabadiliko katika jamii inatakiwa watanzania kuungana mkono katika kuwekeza kwenye elimu kwa kuwa ndio msingi mkuu wa maendeleo nchini.
"Mimi kwa sasa lengo langu ni kuzunguka kilomita elfu hamsini na nikitoka hapa naenda Ivory Coast, Nigeria na nchi nyingine za Afrika Magharibi kabla ya kuja Afrika Mashariki kumalizia ziara yangu hii ambayo nilianza mwaka 2011"alisema Lelo.
Kampuni ya Tigo kwa upande wake imempatia kijana huyo milioni 16 kwa ajili ya kusaidia harakati zake hizo za kuchangisha fedha za elimu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano huo na Lelo, Meneja wa Mawasiliano wa Tigo John Wanyancha alisema kuwa kampuni ya Tigo kama mdau mkubwa wa elimu imenuia kusaidia harakati za kijana huyo hadi kufikia malengo yake.
"Huyu kijana ni mfano wa kuigwa kwakuwa amekuwa na harakati ambazo hata sisi Tigo tumeamua kuziunga mkono kwa kusaidia milioni hizo ambazo zitamsaidia na yeye pia kwenye kuzunguka huko nje ya nchi kuchangisha fedha"Alisema Wanyancha.
Mwisho