Ah!!! soma aliyosema Lulu Mahakamani
http://habari5.blogspot.com/2014/02/ah-lulu-akiri-kuwa-mahakamani.html
MSANII wa filamu, Elizabeth Michael 'Lulu' amekubali kuwa alikuwapo nyumbani kwa aliyekuwa msanii mwenzake Steven Kanumba, siku aliyofariki dunia, hata hivyo amekana kumuua.
Mwanadada huyo alisema hayo jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Rose Teemba wakati aliposomewa maelezo ya kesi ya kumuua msanii huyo bila kukusudia.
Baada ya kusomewa maelezo ya kesi na Wakili wa Serikali Monica Mbogo, Lulu alikiri kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba, pia alidai alikuwepo nyumbani kwa Kanumba siku ambayo alifariki dunia na walikuwa na ugomvi.
Awali Wakili Mbogo alidai kuwa, Lulu na Kanumba walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Aprili 7 mwaka juzi, Kanumba akiwa nyumbani kwake Sinza Vatican alimwambia mdogo wake Setti Bosco ajiandae watoke na wakati wakijiandaa Lulu alifika na kuingia chumbani.
Alidai baada ya muda kidogo, Bosco alisikia malumbano kati yao ambapo Kanumba alikuwa anamtuhumu Lulu anaongea na mwanaume mwingine mbele yake.
Mbogo alidai, Bosco alisikia Lulu analia na aliposogea akamuona anajaribu kutoka mlangoni lakini Kanumba alimvuta na kufunga mlango, hata hivyo muda mfupi baadaye Lulu alitoka chumbani na kumwambia kuwa Kanumba ameanguka sakafuni.
Aliendelea kudai kuwa, Bosco alipoingia alimkuta Kanumba sakafuni akampigia simu daktari wake Palpas Kageiya ambaye baada ya kufika na kumpima aligundua amekufa na kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi.
Alidai Lulu alikamatwa Aprili 8 saa 11 alfajiri katika eneo la Bamaga na kushitakiwa mahakamani kwa kesi ya kuua bila kukusudia.
Baada ya maelezo hayo, Lulu alikiri kuwepo nyumbani kwa Kanumba na walikuwa na ugomvi, akajaribu kutoka chumbani lakini alivutwa ndani na mlango ukafungwa, pia alikiri kuwa alipotoka alimueleza Bosco kuwa Kanumba kaanguka. Amekiri kukamatwa na kushitakiwa kwa kesi hiyo.
Upande wa Jamhuri utakuwa na mashahidi wanne pamoja na vielelezo ambavyo ni ripoti ya uchunguzi wa daktari na ramani ya tukio, na Lulu atakuwa na mashahidi watano pamoja na vielelezo ambavyo ni panga na ripoti ya daktari.
Jaji Teemba alisema mshitakiwa ataendelea kuwa nje kwa dhamana na pande zote mbili zitapewa tarehe ya kesi kusikilizwa.
Lulu anakabiliwa na mashitaka ya kumuua bila kukusudia msanii maarufu wa filamu nchini, Steven Kanumba kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu. Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili mwaka juzi katika eneo la Sinza Vatican, Dar es Salaam.
Awali kesi hiyo ilikuwa ya mauaji, ambayo haina dhamana. Lakini, baada ya kukamilisha upelelezi, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) alibadilisha mashitaka na kuwa ya kuua bila kukusudia, ambayo yana dhamana.
Januari 29 mwaka jana, Lulu aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa na Mahakama na kesi hiyo ilihamishiwa katika Mahakama Kuu na kusajiliwa kama shauri la jinai la kuua bila kukusudia namba 125 la mwaka juzi.
Mwisho.