Simba yajifariji, yaahidi makubwa kwa Mbeya City
http://habari5.blogspot.com/2014/02/simba-yajifariji-yaahidi-makubwa-kwa.html
MBALI na kubugizwa 1-0 na timu ya Mgambo JKT katika mchezo uliochezwa juzi kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga Simba inaonekana kuwa ni bado yenye kujiamini na kuahidi kufanya vema kwenye mchezo ujao.
Simba ambayo kwa sasa imeshuka hadi nafasi ya nne ina pointi 31. Simba ambayo ipo kwenye mfululizo wa ziara zake mikoani ikiwa imetoa sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar mchezo uliochezwa wiki moja kabla ya kukutana na JKT Mgambo.
Kwa sasa Simba ambayo inatarajia kuumana na Mbeya City Jumamosi ijayo jijini Mbeya imejipanga kuhakikisha kuwa inaonesha makali yake dhidi ya timu hiyo.
Akizungumza na gazeti hili kocha wa Simba Zdravko Logarusic alisema kuwa matokeo ya mchezo huo wa juzi ni matokeo kama mengine lakini hata hivyo aliahidi kufanya vema dhidi ya Mbeya City.
Alisema kuwa Simba ikiwa na wachezaji wake wote makini na wenye uwezo mkubwa kisoka haina sababu ya kuogopa mchezo ujao kwa kuwa kushindwa kufanya vema katika michezo yake iliyopita haina maana ndio ishindwe kwa Mbeya City.
"Kwa sasa wachezja wanajipanga kuendelea na mazoezi ili kujiandaa kuikabili Mbeya City hiyo siku ya Jumamosi na tunaahidi kuwa tutafanya vema siku hiyo"alisema Zdravko Logarusic.
Kwa upande wake msemaji wa Simba, Asha Muhaji alisema kuwa kwa sasa timu ipo Dar es salaam ikiendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Kinesi.
Alisema kuwa timu hiyo itaelekea Mbeya kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Mbeya Ciy siku yoyote kuanzia sasa pale tu uongozi utakapoamua.
"Kwa sasa timu ipo katika hali nzuri ikiendelea na mazoezi na inawezekana siku yoyote kuanzia Jumatano, Alhamis au Ijumaa itaeelekea mkoani Mbeya kwa ajili ya mchezo huo"alisema Asha.
===================