Makala Video za Wasanii. Utengenezaji wa Video za wasanii utazamwe kwa jicho la tatu
http://habari5.blogspot.com/2014/07/makala-video-za-wasanii-utengenezaji-wa.html
Na Evance Ng'ingo
KWA sasa hapa nchini karibia kila msanii akiulizwa kuhusiana na gharama ya video ya wimbo wake mpya aliotengeneza basi utasikia kuwa imegharimu miliono 45 au 50.
Hii inamaanisha kuwa wapo wasanii ambao wamewekeza kwa kiasi kikubwa fedha nyingi kwenye utengenezaji wa video zao.
Lakini pia ni lazima kujiuliza iwapo ni kweli gharama hizo wanazotaja au ni kutafuta tu sifa ingawaje wapo wasanii ambao thamani za video zao zinaendana kabisa na gharama wanazozitaja
Video hizo nyingi za gharama kubwa zinatengenezwa zaidi Afrika Kusini, Nigeria na Uingereza ambapo wapo wasanii kadhaa waliotengeneza video zao kwenye nchi hizo
Wapo wasanii kama vile akina Nasib Abdul, Diamond au akina Ommy Dimpoz ambao hivi karibuni video zao walizotengeneza Uingereza zimegharimu mamilioni ya fedha.
Ni juhudi nzuri zinazofanywa na watu hao na zinatakiwa kupongezwa kwa hatua kama hiyo ya kutengeneza video za gharama kubwa na zinaonekana kuwa ni za viwango
Kwa hapa nchini wapo watu kadhaa walioamua kuwekeza kwenye utengenezaji wa video za wasanii ambao nao pia wamekuwa wakitengeneza video nzuri.
Watengenezaji wa video kama vile akina Adam Juma, Karabani Karabani au Nisher Nisher wamekuwa wakisifiwa pia kwa kutengeneza video zenye viwango kwa hapa nchini.
Swali litabakia kuwa ni kwa nini wasanii wanaenda kutengeneza video zao nje ya nchi huku kwa hapa nchini wakiwapo watengenezaji wakubwa wa video.
Msanii Ambwene Yesaya ambae kwa upande wake ametengeneza video ya wimbo wake Asante kwa mtengenezaji Bosco wa Kenya anasema kuwa watengenezaji wa nje hawana utofauti sana na wa Tanzania.
Anasema kuwa tofauti kubwa ni kwamba wale wa nje wanakuwa wameshafanya kazi nyingi za wasanii mbalimbali na hivyo wanakuwa na radha tofauti na wa hapa.
Anaongeza kuwa pia inawezekana watengenezaji wa video za wasanii wa hapa nchini wakatengeneza vema zaidi tena hata kuwashinda wale wa nje.
"Utengenezaji wa video unahitaji zaidi ubunifu na pia hata uzoefu wa kazi yenyewe hicho ndio kinachokuja kuwa tofauti na watengenezaji wa video wa nje ya nchi, suala la vifaa nalo linaweza kuwa muhimu lakini ndo hivyo unaweza kuwa navyo na ukachemka pia"anasema Ay.
Kwa upande wake Karabani Karabani anasema kuwa biashara hiyo kwa sasa imekuwa na kuna watengenezaji wengi wa video wenye uwezo tofauti tofauti.
Anaongeza kuwa wapo watengenezaji wa video ambao wanachukulia ni kama kazi ya kuuzia sura huku wapo ambao wanafanya kama kazi kamili.
Anaongeza kuwa kwa upande wake anafurahia kuona kuwa wapo wasanii ambao wanatambua thamani ya Video katika kukuza sanaa zao.
Anafafanua kuwa iwapo msanii akiwa amefanya kazi nzuri ya sanaa na kisha kuwa na video nzuri na yenye kuvutia ni rahisi zaidi kupata shoo mbalimbali.
Hii inajidhihirisha kwa msanii Diamond ambae amepata shoo nyingi kutokana na kujitangaza kupitia video yake ya My Number One ambayo imetengenezwa na kampuni ya Ogopa Dj.
Kutokana na mazingira ya video hiyo kuwa ni Afrika Kusini basi imeiongezea thamani ya video hiyo na kuifanya ionekane kuwa ni nzuri zaidi.
Binafsi naona kuwa kuwatumia watengenezaji wa video za wasanii wa hapa nchini na kuwatumia wale wa nje utofauti mkubwa uliopo ni kwamba wa nje wanakuwa na mianya mingi zaidi ya kusambaza kazi zao na kuonekana kimataifa zaidi.
Kampuni kama Godfather ambayo inatengeneza video nyingi za wasanii wa Nigeria, Afrika Kusini na ndio iliyowahi kutengeneza video kadhaa za AY na ule wimbo wa sasa wa msanii Linah Sanga uitwao Ole Themba.
Kampuni hii inaweza kusambaza video zake inazotengeneza kupeleka kwenye Chanel kubwa za muziki duniani kama vile Trace, Mtv ile ya Marekani kwenyewe na sehemu nyingine.
Kwa kuwa na mianya hiyo inawaongezea thamani na kuwafanya wasanii wengi wa hapa nchini kutengeneza video zao huko kwa kuwa wanajua nini wanachokuja kunufaika nao.
Utofauti huo unatakiwa kuzibwa na watengenezaji wetu wa video za muziki za hapa nyumbani.
Kama hao akina Nisha, Karabani pamoja na Adam Juma kuhakikisha kuwa wanajikita kwa kuzitafutia soko video za nje ya Tanzania.
Inaweza kuwa sio jukumu lao kufanya hivyo lakini ndio waone kuwa kuna haja ya kufanya hivyo ili angalau kuweza kushindana sokoni.
Sina wasiwasi na watengenezaji wa video za wasanii wa hapa nyumbani kwa kuwa uwezo wanaweza kuwa sawa na wale wa nje katika uelewa wa nini kifanyike kwenye kutengeneza video hizo lakini wanapaswa kuiga baadhi ya vitu kutoka kwa watengenezaji wa video za nje.
Itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa matumizi ya gharama kubwa katika kutengeneza video hizo kwa kuwa wasanii watapenda kutengeneza video zao hapa nchini.
Lakini pia itarejesha au kuanzisha aina ya video zenye radha na maadhi ya kitanzania hasa kwa sababu ukiangalia video za watu kama Godfather walipotengeneza video ya Mafikizolo ya Khona na ule wimbo wa Ole Themba wa Linah wanaonekana kama zina maadhi sawa ambayo ya Afrika Kusini.
Pia ni vema wasanii wa hapa nchini wakienda kutengeneza video zao za muziki nje ya nchi wajitaidi kuhakikisha kuwa kunakuwa na vitu vyenye kuutambulisha utanzania wetu.
Nimeipongeza video ya Linah Sanga hiyo ya Ole Themba lakini ingeweza kuwa na angalau hata kasehemu kadogo ikaonekana bendera ya Tanzania au hata kutaja jina hilo ili kuonesha kuwa ni msanii wa Tanzania.
Ingawaje video hiyo anaimba kwa kiswahili na kuonesha kuwa ni mtanzania ila angeozea vitu kama hivyo ili kuiweka kikwetu kwetu zaidi.
Wawekezaji wajitokeze zaidi na kuwekeza kwenye tasnia hii ya utengenezaji wa video za wasanii kwa kununua vifaa vya kisasa na kisha kuiongezea thamani kazi hiyo.
Kama wasanii wanaweza kutumia mamilioni ya fedha katika kutengeneza video za nyimbo zao nje ya Tanzania watengenezewe mazingira yatakayowafanya watengeneze video zao hapa nchinio.
=============================