Wazo langu kuhusianana na usajili Bongo




HIVI jana tu ilikuwa ndio siku ya mwisho ya kufungwa rasmi kwa pazia la usajili wa ligi kuu.

Pazia hili lililokuwa lifungwe tangia Alhamisi ya juzi ilibidi kusogezwa mbele kutoa nafasi ya kukamilishwa kwa usajili huo.

Hiyo ni kutokana na kushindwa kukamilika kwa wakati usajili ambapo moja kati ya sababu kubwa ikiwa ni kushindwa kwa matumizi mazuri ya kieletroniki kufanyia usajili.

Ingawaje zipo sababu nyingine mbalimbali nyuma ya pazi lakini pia kuna sababu kuwa klabu zimekuwa zikizembea kutokana na kutokamilishwa kwa sababu mbalimbali za usajili.

Kutokana na hali hiyo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliamua kusogeza mbele tena muda kwa saa 48 hivyo ilikuwa ni kunzia juzi hadi jana.

Binafsi naona kuwa suala hili sio la kuachwa kimzahamzaha kwa kuwa kuahirishwa ahirishwa kwa kufungwa kwa usajili inashusha hadhi ya ligi.

Iweje klabu zinajua kabisa kuwa siku ya kufungwa kwa dirisha la usajili iwe ni siku fulani lakini bado kuwe kuna uzembe wa kukamilisha kwa usajili huo.

Haiingii akilini kusikia kuwa ni klabu moja tu ya Ligi Kuu ambayo  ndio ilikamilisha kwa wakati kutoa taarifa TFF kuhusiana na usajili wake.

Huku pia kwenye ligi daraja la kwanza napo ikiwa ni timu ya Kimondo Fc peke yake iliyokamilisha usajili wake.

Inaanisha kuwa suala hilo la kukamilisha kwa taarifa za usajili kwa wakati halitiliwi mkazo kabisa na wahusika na nio maana hali imekuwa hivyo.

Ninashawishika kuamini kuwa hata ikifika siku ya kukamilishwa kwa usajili wa wachezaji wa kimataifa ambapo ni Septemba 6 mwaka huu huenda hali itakuwa ni hivyo hivyo.

Ikumbukwe kuwa uzembe uliofanywa kwenye kukamilisha usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu wa hapa nchini ukifanywa kwenye kukamilisha usajili wa wachezaji wa kimataifa hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Hiyo ni kwa sababu taarifa za usajili wa wachezaji wa kimataifa wanaocheza ligi yetu zikifafungwa ndio basi tena na hakuna cha kuongezwa muda.

Hiyo ni kwa sababu taarifa zinakusanywa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na hapo muda ukifika ndio hakuna cha kuongeza tena.

Sasa basi kwa kuwa wahusika wanafahamu hilo ni vema wakajipanga kuhakikisha kuwa wanatimiza masharti kabla hata ya muda kufika.

Lakini pia ili kuzuia hali kama hiyo kujirudia ni vema kwa TFF kuepuka kuongeza ongeza muda.

Au ikiwezekana kuwe na kipengele kitakachowaadhibu wale wanaochelewesha kukamilisha taarifa zao za usajili kwa wakati.

Hiyo itasaidia kuondoa uzembe wa aina hiyo kujirudia na kuongeza thamani halisi ya ligi kama inavyotakiwa.

Ni matumaini yangu kuwa wazo langu litazingatiwa na wahusika na kuzingatiwa kwa faida ya  kuongeza hadhi ya ligi yetu.
 

Related

Sticky 5756965480804844969

Post a Comment

emo-but-icon

item