Makala: Ubunifu wa mavazi nchini
http://habari5.blogspot.com/2014/10/makala-ubunifu-wa-mavazi-nchini.html
Na Evance
Ng’ingo
SEKTA ya mavazi ni moja kati ya sekta za kiutamaduni
ambazo zinazidi kukua kwa kasi huku changamoto kubwa ikiwa ni kulipata vazi la
taifa.
Sio suala geni kusikika masikioni mwa watu wakizungumzia
upatikanaji wa vazi hilo la taifa kwa kwa kumekuwa na michakato mbalimbali
iliyokwishawahi kufanywa na wadau mbalimbali katika kulipata vazi hilo.
Lakini pia katika kuendeleza utamaduni huo wa upatikanaji
wa vazi hilo kumekuwa na maonesho mbalimbali ya mavazi ambayo yamekuwa
yakifanyika sambamba na kuendeleza utamaduni wa mavazi chini.
Maonesho kama Lady in Red, Swahili Fashion, Usiku wa
Kanga za Kale, Malaika na mengineo yotee yanalenga kukuza utamaduni huo wa
mavazi.
Ili kuendeleza utamaduni huo kuna wabunifu mbalimbali
ambao kila kukicha wamekuwa wakibuni mavazi kulingana na uhitaji wa soko kwa
wakati husika.
Mbunifu Evelyn Rugemalila wa Eve Collection anasema kuwa
kwa sasa soko kubwa lipo kwenye nguo za maharusi pamoja na sherehe za Kitchen
Party mahsus kwa akina mama.
Anasema kuwa kwa upande wake anaona kuwa fursa katika
soko hilo ndio inatoa mwanya wa ajira kwa watu wengi kwa sasa
wanaojishughulisha na kazi za ubunifu.
Anasema kuwa wanadada wengi kwa sasa wanatambua kazi za
wabunifu wa ndani na wamekuwa wakiwatumia katika kuwashone nguo zao za
kibunifu.
Anaongeza kuwa kwa upande wake amekuwa akipata fursa za
kuwashonea wanawake wengi hasa katika hafla mbalimbali.
“Inatakiwa kuwepo kabisa na sera kwanza ya kulinga
hakimiliki ya kazi ya mbunifu wa mavazi hasa katika kutambua kazi zao, lakini
pia inatakiwa kwa wabunifu pia kuzidisha ubunifu wa kazi ili kuendeleza tasnia
hii inayokua kwa kasi hapa nchini”anasema Evelyn.
Ili kuendelea kuwa na wabunifu wakubwa wa mavazi hapa
kama akina Mustapha Hasanali, Evelyn Rugemalila na wengineo inatakiwa pia
kuwepo na mikakati endelevu ya kuwavumbua na kuwaendeleza wabunifu chipukizi
hapa nchini.
Wapo wabunifu ambao mbali na kuwa na vipaji lakini
havijaonekana na kufanyiwa kazi ipaswavyo na kuwawezeesha kuchangia kikamilifu
maendeleo ya tasnia hiyo.
Mratibu Wiki ya Mavazi ya Swahili Fashion, Honest Arroyal
anasema kuwa kupitia wameanzisha shindano la la kuvumbua vipaji lijulikanalo
kama Emerging Designer Awards.
Anaongeza kuwa ni katika shindano hilo ambapo wabunifu
chipukizi wanaonesha uwezo wao katika ubunifu wa mavazi na kasha anachaguliwa
mbunifu mmoja ambae ndio anatangazwa kuwa ni mshindi.
Anasema kuwa chini ya utaratibu kama huo wabunifu kama
akina, Martin Kadinda, Pooja Jeshang, Sara Mosengo Aly Salim wa Mkoto Design na
wengineo wamepatikana.
Anafafanua kuwa kwa mwaka huu ambapo onesho hilo
litafanyika Desemba 6, 7 na 8 pia
kutakuwa na shindano kwa ajili ya wabunifu chipukizi.
Anaongeza kuwa hadi sasa wabunifu wengi wameshajitokeza
na kuchukua fomu za ushiriki ikilinganiwa na miaka ya nyuma.
“Najua ili kukuza utamaduni huu wa mavazi na kuipa tasnia
hii heshima inayostahili inatakiwa kuwepo kwa mikakati ya kisasa kabisa ya
kuwaibua wabunifu na Swahili Fashion ndipo mahala pake”anasema Arroyal.
Kwa upande wake Martin Kadinda anasema kuwa kupitia
maonesho ya mavazi ndipo vipaji vingi vinaibuliwa na kuwatengenezea mwanya wa
ajira vijana.
Anaongeza kuwa anaona kuwa kwa sasa hata wasanii wamekuwa
wakivalia nguo za wabunifu wa mavazi wa hapa hapa nyumbani.
Anaongeza kuwa kwa kufanya hivyo inaonesha ni kwa kiasi
gani tasnia hiyo ya ubunifu wa mavazi inahusiana na sanaa ya muziki kwa ukaribu
zaidi.
“Kwa mimi binasfi nilikua nikimvalisha msanii Nasib
Abdul, Diamond kwa kipindi kirefum, na amekuwa akionekana nadhifu tena vema
sana, hiyo ni kwa kazi yangu mimi kama mbunifu wa mavazi”anasema Kadinda.
Anaongeza kuwa kwa wasanii wa Marekani na kwengineko
duniani hali imekuwa ni tofauti kwa kuwa wao wenyewe wanauza nguo zao na
wanapata mabilioni ya fedha.
Hilo linajidhihirisha kwa msanii mahiri wa Marekani ambae leo anatumbuiza kwenye Tamasha la Serengeti Fiesta mwaka T.I.
Msanii huyo anamiliki mavazi yenye lebo mbalimbali kama
vile Hustle Gang, Akoo pamoja na Strivers Row ambayo yameanza kuuzwa kwenye
duka la Pop Up Shop lililopo Super Market ya Dar Free Market.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Grand
Hustle Records, Jason Geter ambayo ndio kampuni inayomsimamia msanii B.O.B na
mwanadada anayekuja kwa kasi Iggy Azalea wa Marekani, anasema anaamini soko
la Tanzania na Afrika kwa ujumla ni masoko makubwa kwa bidhaa zao.
‘Tuna matarajio makubwa kuhusiana na kuleta bidhaa zetu
nchini Tanzania, na tunatarajia sio tu kuleta bidhaa zetu hapa nchini, bali
kwenda mbali zaidi kwa kujifunza soko la mitindo hapa nchini’ anasema Geter.
Anaongeza kuwa
wasanii wanatakiwa kutumia umaarufu wao katika kujitafutia vyanzo vingine vya
biashara muhimu.
=============