Kumbukia ilivyokuwa siku ya Msanii Oktoba 25
http://habari5.blogspot.com/2014/11/kumbukia-ilivyokuwa-siku-ya-msanii.html
Na Evance Ng'ingo
TANZANIA kwa mara ya kwanza hivi karibuni ambayo hufanyika kila Oktoba 25 ya kila mwaka.
Nchi nyingine zimekuwa zikiadhimisha siku hiyo lakini kwa hapa nchini imeadhimishwa kwa mara ya kwanza jumamosi iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City.
Kampuni ya Hakneel Production ndio iliyohusika na uandaaji wa shughuli nzima ikisaidiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Maadhimisho hayo yalienda sambamba na burudani safi kutoka wa wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya na asili.
Katika kuonesha umuhimu wa siku hiyo kwa sekta ya sanaa hapa nchini kulikuwa na utoaji wa Tuzo kwa wasanii waliotoa mchango uliotukuka katika sanaa hapa nchini.
Tuzo hizo zilitolewa na Makamu wa Mohamed Gharib Billal aliekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Msanii wa uchoraji wa muda mrefu Edward Tinga Tinga alikabidhiwa unayotambua mchango wake uliotukuka kwa kumtunuku tuzo ya Mafanikio ya Muda mrefu katika maisha ya sanaa.
Tingatinga alifariki mwaka 1972 baada ya kuishi kwa miaka 40.
Msanii huyo anaheshimika kwa uwezo wake wa kuchora picha kwa njia za vidoti doti ambapo kwa sasa zinauzika zaidi hata nje ya nchi na kumpatia heshima kubwa msanii huyo.
Pia Makamu wa Rais alitoa tuzo kwa msanii Joseph Kanuti kwa kutambua mchango wake katika kusaidia masuala ya kijamii.
Kanuti alitokea mkoani Morogoro ambapo kwa kiasi kikubwa aliwafundisha wanamuziki kadhaa suala zima la matumizi ya ala za upepo na elimu nzima ya muziki.
Waliwakilishwa na ndugu zao waliofika kuwachukulia Tuzo hizo siku hiyo.
Siku hiyo iliyopambwa na burudani safi kutoka kwa wasanii wa aina mbalimbali kuanzia muziki wa asili hadi muzii wa kizazi kipya ulifana na kuvutia karibia kila mmoja aliekuwapo ukumbini hapo.
Makamu wa Rais katika hotuba aliwataka wasanii kuiga mfano wa kazi nzuri kutoka kwa wasanii akina Tingatinga na Kanuti kwa kuwa walifanya kazi yao ya sanaa kwa umakini mkubwa hadi sasa wanaendelea kuheshimika.
"Serikali inatambua nguvu ya sanaa katika kutengeneza ajira kwa vijana pamoja na kusaidia jamii, hivyo imeweka sera nzuri zitekelezwazo kikamilifu zenye kulenga kuwasaidia wasanii"alisema Makamu wa Rais.
Anasema kuwa kwa kutambua hilo hata katika katiba iliyopendekezwa suala la sanaa limepewa kipaumbele kikubwa na litafanyiwa kazi kwa hali na mali katika kuwasaidia wasanii.
Siku hiyo iliyopambwa na viashiria vya muziki wa kiutamaduni pamoja na wa kisasa ilizinduliwa kwa burudani kutoka kundi la Street Dancers.
Walicheza nyimbo kadhaa zilizoimbwa na wasanii wa muziki wa Bongo Fleva na kisha ikafuata burudani ya muziki kutoka kundi la Super Nyamwela akiwa na wachezaji wenzake watatu.
Baada ya hapo ilikuja ngoma za asili kutoka kwa Kundi la Kelekele na Ukerewe mkoani Mwanza lililonogesha kwa burudani zake za ngoma za asili.
Kundi hilo lililokuwa na wachezaji zaidi ya 10 walizikonga nyoyo za wapenzi wa burudani kutokana na umahiri wao wa kucheza ngoma na ilifikia hatua wapiga ngoma wakapanda juu ya ngoma.
Baada ya burudani hiyo ikafuata burudani kutoka kwa mwimbaji wa nyimbo za taarabu Isha Ramadhani maarufu kama Isha Mashauzi ambae aliimba nyimbo nne akiwa na wacheza shoo wake.
Kwa namna ambavyo siku hiyo Ukumbi wa Mlimani City ulipambwa ilivutia na kufanya siku hiyo kuonekana kweli ni ya msanii na inahusiana na msanii wa kitanzania.
Ukumbini hapo kulipambwa na jukwaa lililokuwa limegawanyika mara mbili na hivyo kutoa mwanya kwa wageni kuoana vema burudani hiyo huku nje kukiwa kumepambwa na nakshi za asili kama miti, vinyago na vitambaa vya asili.
Jukwaa lilipambwa kwa viashiria vya Pundamilia huku wafanyakazi wa tukio hilo wakiwa wamevalishwa kiasiliasili pia.
Ilikuja kuwa ni furaha zaidi hasa pale ambapo msanii Nasib Abdul, Diamond alipopanda jukwaani baada ya kutimu saa tano kasoro ambapo akiwa na madansa wake walitumia dakika takribani 45 kutoa burudani safi.
Diamond alionekana nadhifu kimavazi pamoja na madansa wake hao.
Walianza kuingia madansa wakiwa wamevalia suruali nyeupe pamoja na fulana sweta za bluu ambapo walianza kwanza kucheza kabla ya kuja Diamond jukwaani.
Alipotokea Diamond alianza na wimbo wake Nataka Kulewa, kisha kufuata nyingine kama Mawazo na Moyo Unaniuma.
Alifanikiwa kuzikonga nyonyo za watu wengi hasa kwa umakini wa kuteka jukwaa na kuimba na washabiki wake huku akiwafuata vitini.
Ilikuwa ni shoo ya aina yake hadi ilifika wakati gazeti hili lilimuona Makamu wa Rais akiwa anafurahia na kutikisa kichwa kwa furaha.
Kabla ya kumalizia shoo yake na wimbo wa Kitolondo msanii huyo alijidai kama amemaliza shoo yake na watu walianza kulalamika wakimuita arejee na kisha aliporejea akamalizia na wimbo wake huo kisha kuondoka.
Awali Makamu wa Rais alipokabidi tuzo kwa wasanii ilitajwa kuwa zinaendana na Milioni Moja moja kwa kila mmoja lakini baade kwa mapenzi yake aliamua kuwaongezea tena milioni tano.
Zawadi hiyo inawahusu washindi wa Tuzo hizo walioshinda siku hiyo ambao ni Kanuti na Tingatinga.
Wachekeshaji kutoka Kenya Fred Omond na nduguye siku hiyo walijitaidi kwa kiasi kikubwa kuchekesha kabla ya kuja kwa bendi ya Yamoto.
Baada ya hapo ilifuata burudani ya kipekee kutoka kwa bendi ya Yamoto.
Vijana hao wanne walitoa burudani safi ambapo waliimba Live jukwaani wakiwa na bendi yao hiyo.
Walitawala vema ukumbi huo kwa kuimba na kucheza kwa staili tofauti.
Nyimbo zao za kama vile Najuta na ule wa Niseme ambapo washabiki wao waliungana nao jukwaani kucheza muziki pamoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hakneel Production, Godfrey Mahendeka anasema kuwa kampuni yake imeamua kuratibu siku hiyo kwa kutambua mchango wa sanaa katika kukuza uchumi wa nchi.
Anasema kuwa itaendelea kufanya hivyo kwa kuwa inaona kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuadhimishwa kwa siku hiyo muhimu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza anasema kuwa ni muhimu kuwa na maadhimisho kama hayo kwa kuwa yanaongeza thamani ya sanaa na kuonesha umuhimu wake.
"Tunataka ikifika wakati kila mkoa uwe na unaadhimisha siku hii muhimu kwa namna yao, kila iwe inafanyika huku wasanii nao wakiwa karibu zaidi na kujiona kuwa ni sehemu ya kazi" anasema Mngereza.
==================