RIP Shem Kalenga

Na Mwandishi Wetu
MWANAMUZIKI Mkongwe wa zamani nchini Shem Karenga amefariki dunia katika hospitali ya Amana alipokuwa amelazwa.

Mwanamuziki huyo alikuwa ni kati ya wanamuziki wachache wenye uwezo wa kucharaza gitaa huku akiimba kwa wakati mmoja.

Marehemu aliwahi kutamba kwenye miaka ya 1970  akiwa na bendi ya Tabora Jazz wana Segere Matata.

Alizaliwa mwaka 1950 eneo la Bangwe mkoani Kigoma na kupata elimu yake katika shule ya msingi Kihezya kati ya mwaka 1957 na 1964.

Alianza kujifunza muziki akiwa mwanafunzi katika shule ya wamissionari na huko ndiko fani hiyo ilianza kuchipua hatimaye mwaka huo huo wa 1964  akajiunga na bendi ya Lake Tanganyika Jazz iliyokuwa na maskani yake mjini Kigoma.

Alipoingia Lake Tanganyika Jazz alijifunza Ala za muziki za drums, Kinanda na gita la rhythm, Solo. Besi gita pamoja akiimba.

Alidumu  katika bendi hiyo kwa kipindi cha miaka minane na mwaka 1972 Shem Kalenga aliitwa katika bendi ya Tabora Jazz ambako aliingia kwa kishindo na nyimbo zake alizozitunga akiwa na Lake Jazz na kuanza kuzipiga katika bendi yake mpya.

Nyimbo hizo zilikuwa Dada Asha na Remmy ambazo zilimpa umaarufu na kujulikana kwa haraka na kuwa simulizi katika kila pembe za mji  huo wa Tabora.

Shem alipata ushindani mkubwa baada ya kuwakuta wakali wengine wa kupiga gita akina Kassimu Kaluwona, Athuman Tembo pamoja na Salumu Luzila na  Issa Ramadhan ‘Baba Isaya’ lakini alijitutumua  na kuwa mmoja kati ya wapiga solo gita  bora la katika bendi hiyo.

Mwaka wa 1983 Shem Kalenga aliicha bendi hiyo kwa sababu zake mwenyewe na kuachana na mambo ya muziki kwa muda.Lakini baada ya kuondoka yeye bendi hiyo haikudumu tena na ikapotea katika ramani ya muziki.

Aliondoka Tabora  mwaka 1990  baada ya kuitwa na mfanyabiashara wa jijini Dar  es Salaam Baraka Msilwa ambaye alimuomba ajiunge katika bendi yake ya M.K. Beat iliyokuwa ikipiga katika mtindo wa ‘Tunkunyema’ Bendi hiyo ilikuwa ndugu na ile ya M.K. Group.

Ndani ya M.K.Beat Shem Kalenga  aliwakuta vijana machachari akina Maliki Star, Bwani  Fanfan, Sisco Lunanga na Fungo Shomari. Kwa mshikamano waliokuwa nao  waliweza kuiinua Bendi hiyo vilivyo na kuwa tishio kwa bendi zingine za jijini Dar es Salaam.

Bendi hiyo ilisambaratika mwaka 1995 na mwaka uliofuatia alianzisha bendi yake ya Tabora Jazz Star ambayo ina wanamuziki sita na huburudisha katika kumbi mbalimbali za jijini Dar  es Salaam hadi sasa. 

Anasema miaka ya hivi karibuni biashara huria ziliporuhusiwa, Studio nyingi binafsi zilifunguliwa lakini hazina manufaa kwao kufuatia kiwango cha pesa zinazotozwa na Studio hizo  kuwa kubwa mno kiasi cha wao kushindwa kumudu kulipia.

Related

Technology 5186276874886391930

Post a Comment

emo-but-icon

item