Diamond, Alikiba wafunika Tamasha la Tigo Music la Leaders



Na Evance Ng'ingo
MAGIWJI wa muziki wa Bongo Flava, Alika Kiba na Nassib Abdul maarufu kama Diamond walitia fora kwenye tamasha la Tigo lililofanyika Uwanja wa Leaders juzi, huku likishuhudiwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara.

Wasanii hao walikuwa ni kati ya wasanii 18 wa muziki huo waliotoa burudani safi katika tamasha hilo lililohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es salaam.

Alianza Ali Kiba kwa kucheza na kuimba nyimbo zake mbalimbali ambazo zilivutia kwa kiasi kikubwa mashabiki waliokuwapo katika shoo hiyo.

Alipopanda jukwaani alishangikiwa kwa kiasi kikubwa na washabiki wake na alivutia zaidi hasa kutokana na alivyokuwa akicheza na kisha kuna muda aliamua kubadilisha nguo na kurejea tena uwanjani, hivyo kuongeza hamasa zaidi kwa mashabiki wake.

Ndipo ikafuata zamu ya Diamond ambapo alianza kwa shoo kali kabla ya kuwashukuru mashabiki wake kwa kumpigia kura zilizomwezesha kupata tuzo tatu za kimataifa, huku pia akiwamwagia fedha za noti ya sh. 2,000.

Burudani siku hiyo ilianzia majira ya saa 10:00 jioni ambapo bendi ya Sikinde ilifungua pazia kisha kufuatwa na Msondo na mwimbaji wa taarab Khadija Kopa na kufuatiwa na Isha Mashauzi.

Wengine waliopamba burudani hiyo ni Christian  Bella pamoja na bendi ya Malaika,  Yamoto bendi, Vanessa Mdee, Barnaba Classic, Jux, Shaa, Fid Q, Professor J, Don Coliando, Weusi, AY na FA.

Akizindua huduma hiyo ya Tigo Music inayowawezesha wateja wa Tigo kujipatia nyimbo mbalimbali, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara alisema kuwa amevutiwa na huduma hiyo kwa kuwa inafungau milango ya kipato zaidi kwa wasanii.

“Kwa kuwa kutakuwa na nyimbo zaidi ya milioni 36 na hivyo kuwaongezea uwanja zaidi wa burudani wapenzi wa muziki na bado wasanii wananufaika na huduma hii, hili ni suala zuri zaidi katika kukuza sanaa hapa nchini,” alisema Fenella.

Pia Meneja Mkuu wa Tigo Diego, Gutierrez alisema kuwa kampuni hiyo mbali na kuendeleza sekta ya mawasiliano lakini pia imejitaidi kuendeleza sekta ya sanaa kwa namna mbalimbali.

Alisema kuwa kupitia tamasha hilo lililowakutanisha wasanii 18 wananchi wamejipatia fursa ya kuburudika na kuwa kampuni hiyo imewawekea mazingira mazuri ya kunufaika zaidi kwa njia ya nyimbo hizo zaidi ya milioni 36 zitakazokuwa zikipatikana kwa wateja wake.

Related

Technology 8044911360499404282

Post a Comment

emo-but-icon

item