Mwanamke bora wa mwezi
http://habari5.blogspot.com/2015/01/mwanamke-bora-wa-mwezi.html
Na Cynthia Buhama, Turdaco
TUZO hutumiwa kuonesha hali ya kutambua mchango wa mtu katika kuleta maendeleo kwenye kazi, shughuli au hata taarifa mbalimbali katika jamii.
Mara nyingi huwa inachangia katika kuhakikisha kuwa mhusika anaepewa tuzo hiyo anahamasika zaidi katika kuendeleza yale mazuri ambayo anakuwa ameyafanya na kumpatia tuzo husika.
Mfano kwa mtu anaepewa tuzo kutokana na mchango wake katika kuendeleza masuala ya Sayansi, tuzo hiyo inaweza kuwa mchango katika kuendeleza shughuli zake za kisayansi.
Suzane Mashibe aliwahi kushinda Tuzo katika kipengele cha wanawake mahiri katika sekta ya Sayansi na Teknolojia iliyotolewa na Shirika lijishughulishalo na Mafanikio kwa akinamama (TWA).
Tuzo hizo zitolewazo kila baada ya miaka miwili kwa mwaka huu zitatolewa Machi 7.
Susan Mashibe ni mmoja kati ya akina mama walionufaika na Tuzo hiyo kwa maana ilimhamasisha zaidi kwa kutambua juhudi zake katika kusaidia masuala ya Teknolojia.
Ni mwasisi wa na Mkurugenzi Mtendaji wa VIA Aviation ambayo ilikuwa ikijulikana awali kama Tanzanite Jet Centre (TanJet).
Akiwa kama mjasiriamali aliejikita kwenye biashara hiyo ya angani akiwa amejikita katika kusaidia sekta binafsi katika masuala ya anga.
Ni mwanamke wa kwanza kuidhinishwa kuendesha ndege za biashaara za abiria na utengenezaji wa ndege.
Ni mwakilishi wa Baraza la kimataifa la masuala ya Biashara ya Anga kwa hapa Tanzania.
Suzane anasema kuwa kwa upande wake alipopewa tuzo hiyo iliamsha hali ya kujiamini zaidi na kuendeleza harakati zake katika sekta hiyo.
Anasema kuwa tangia kupewa kwa Tuzo hiyo mwaka huo hadi sasa amejikuta ikimsaidia kuendelea kufanye mengine mengi makubwa katika sekta ya anga na hivyo kuendeleza masuala ya Sayansi kwa ujumla wake.
"Tuzo ni nzuri kwa kuwa kwanza zinaongeza hamasa kwa kuwa inakuwa imekutambua kama mdau katika kuendeleza sekta husika kitu ambacho ni kikubwa na cha msingi zaidi"alisema Suzane.
Anaongeza kuwa" nikiwa kama mwanamama ambae nimenuia kuleta mabadiliko katika sekta hiyo kwa tuzo hiyo ilinihamasisha kufanya makubwa zaidi na kuwa nitaendelea tena na tena".
Kwa upande wake Rais wa TWA, Irene Kiwia anasema kuwa tuzo hizo zimekuwa na lengo la kusheherekea mafanikio ya wanawake nchini katika shughuli mbalimbali.
Anasema kuwa kwa kila mwaka wamekuwa na vipengele mbalimbali wanavyoshindanisha ambapo ni kama vile sanaa na utamaduni, ujasiriamali, elimu, afya, sayansi na teknolojia, kilimo, ustawi wa jamii na michezo.
Pia kuna tuzo kwa mshiriki wa mafanikio mwenye umri mdogo, mwanamke aliefanya vizuri ndani ya mwaka mzima pamoja na mwanamke aliefanya vizuri katika maisha yake.
"Huwa kuna shughuli ambazo wanawake hawa wanakuwa wamezifanya kwenye jamii kupitia nyanja tofauti hapa nchini" anasema Irene.
Anaongeza kuwa "kuna vigezo mbalimbali vitatumika katika kuwachagua washindi katika kila kipengele ambapo anatolea mfano wa kuwa vigezo kama kama vile utofauti waliouonyesha katika jamii zao, jinsgani wameweza kuwavutia na kuwashawishi watu wengine, na jinsi gani wameweza kuwagusa na kuwafikia watu tofauti tofauti kutokana na huduma zao hizo."anasema Irene
Anaongeza kuwa kwa kawaida Tuzo hizo huwa zinaenda sambamba na mafunzo ya kujenga uwezo wa wasichana viongozi katika nyanja tofauti walio kati ya umri wa miaka 18-27.
Anasema kuwa wasichana hao wanachaguliwa kutoka katika mikoa yote ya Tanzania ambapo wanachaguliwa wasichana kadhaa na kisha kuhudhuria mafunzo hayo ya wiki sita.
Wasichana hao watakutanishwa na wanawake wanaofanya vizuri katika biashara, kazi za jamii na idara tofauti kwa ajili ya kupewa motisha an kujifunza.
Mategemeo yetu ni kuwa baada ya mafunzo haya wasichana wataenda kuwa chachu ya mabadiliko mikoani mwao kwa kuwafundisha wenzao wengi yale watakayojifunza.
Aliongeza kuwa ili kusambaza hali ya kutaka maendeleo pamoja na mabadiliko kwa wasichana wadogo nchini kote mafunzo hayo yanalenga kuwajengea pia uwezo wa kujitambua.
"Najua leo tunapowasikia watu kama akina Suzane ni sio tu kwamba wao walikaa na kubweteka kisha kujikuta wakiwa akina mama wenye mafanikio namna ile, hapana walijengewa uwezo na waliokuwa juu yao na wao wamekuja kufanikiwa"anasema Irene.
Mwenyekiti wa TWAA, Mrs. Sadaka Gandhi anasema kuwa kwa sasa suala la uwezeshaji kwa wanawake linapewa kipaumbele duniani kote.
"Tuzo hizi zitaonesha uwezo na ugunduzi wa wanawake katika sehemu tofauti, Tunaamini kuwa wale wote watakaoshiriki watakuwa chachu ya mabadiliko kwa wasichana kutoka vijijijini, wafanyabiashara na wanawake wengi chini Tanzania” anasema Sadaka.
"Katika kipindi cha miezi mitatu, tunaomba watu mbalimbali ajitokeze kuchagua wanawake ambao wanafanya vizuri katika fani zote kuanzia mfanyabishara mwenye jitihada kubwa, mwalimu wa namna ya kipekee na hata mtu ambaye ameweza kuleta mabadiliko muhimu katika jamii yake". Gandhi.
Anasema kuwa kwa mwaka huu Julai 31 ndio mwisho wa kutuma maombi.
Anawataka wanawake wanaojiona kuwa wana vigezo vya kushiriki wanaweza kujipendekeza ama kupendekezwa kupitia tovuti ya www.twa.or.tz.
Kamati ya TWAA inawajumuisha Bi Mary Rusimbi - Mwanaharakati na Mwanzilishi wa Programu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania, Jaji Joaquine De Mello, Dk. Marcelina Chijoriga - kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bwana. Innocent Mungy - Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Sadaka Gandi - Mwanasaikolojia na mfanyakazi za Jamii, Irene Kiwia - Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya mahusiano ya jamii Frontline Porter Novelli.
=============