MWAKA wa 2014 ulikuwa ni mwaka wa aina yake katika medani ya sanaa nchini.
http://habari5.blogspot.com/2015/01/mwaka-wa-2014-ulikuwa-ni-mwaka-wa-aina.html
Na Evance Ng'ingo
Kwa mwaka huo sekta ya sanaa ni moja kati ya sekta ambazo zilikumbana na mambo mbalimbali kama vile vifo na hata mafanikio kwa baadhi ya wasanii.
Kwa upande wa mafaniko baadhi ya mambo ambayo yalililetea sifa kubwa taifa hili ni ushindi wa Idris Sultan katika shindano la Big Brother Afrika.
Kijana huyo aliibuka na ushindi huo uliopelekea kujipatia kitita cha Dola za Kimarekani 300,000 ambazo ni sawa na Milioni 524 za kitanzania.
Ushindi huo wa shindano hilo ni moja kati yavitu vya kukumbukwa kwa mwaka wa 2014 kwa kuwa ni kuna moja katia ya tukio la ushindi kupatikana katika sekta ya sanaa.
Lakini pia kwa upande mwengine kuna msanii Nasib Abdul, Diamond Platinum, ambae kwa sasa ni mmoja kati ya wasanii wakubwa si kwa hapa nchini tu bali hata kwa Afrika Mashariki na ambae anaanza kufahamika kwa Afrika nzima kwa ujumla.
Kwa upande wa msanii huyu alipata tuzo kadhaa kwa mwaka huu ambapo mbali na kupata Tuzo saba katika utoaji wa Tuzo za Muziki za Kilimanjaro kwa mwaka huu.
Licha ya kujipatia tuzo hizo lakini pia amejishindia tuzo katika Shindano la Chanel O Music Award ambapo aliibuka na tuzo mbili katika shindano hilo.
Ushindi huo mbali na kumtangaza msanii huyo nje ya Tanzania lakini pia umesaidia kwa kiasi kikubwa kufungua milango yake ya shughuli za sanaa.
Pia umemwezesha kijana huyo kulitangaza taifa la Tanzania kwa njia ya sanaa kwa kiasi kikubwa kitu ambacho kwa muda mrefu hakikuwahi kutokea.
Sekta ya sanaa kwa mwaka 2014 imeonekana kung'aa zaidi katika kulitangaza taifa.
Katika mashindano yaliyoshirikisha michezo ya aina mbalimbali Tanzania haikufanya vema kwa mwaka jana lakini angalau kuna mahala ambapo jina la Tanzania limewakilishwa vema nje ya nchi ambapo ni katika sanaa.
Lakini pia Diamond kwa mwaka huo huo wa jana alijitaidi kushindania Tuzo mbalimbali za kimataifa kama vile BET na MTV ambapo hakufanikiwa kupata tuzo.
Mbali na kufanya vema kwa sekta hiyo ya sanaa lakini pia ilikumbwa na mahasibu mbalimbali kama vile vifo vya wasanii wakubwa na mengineo.
Kifo cha mwanamuziki nguri wa Muziki wa Dansi, Maalim Muhdin Gurumo ambae alifariki dunia baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mefu kidogo.
Gurumo aliwahi kufanya kazi na bendi mbalimbali za muziki wa dansi kuanzia Bendi ya NUTA Jazz, Mlimani Park Orchestra, Orchestra Safari Sound (OSS) na Msondo Ngoma ambayo ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013.
Marehemu Gurumo alizikwa kijijini kwake Masaki, Kisarawe Mkoa wa Pwani.
Pia moja kati ya mapigo makubwa katika sekta ya sanaa ni kifo cha mzee Small ambae alifariki akiwa katika hospitali ya Muhimbili ambapo alikuwa akitibiwa ugonjwa wa Kiharusi.
Alizikwa katika makaburi ya Tabata Segerea na hivyo kuwa mmoja kati ya wasanii walioacha simanzi kubwa katika tasnia ya sanaa mwaka 2014.
Lakini pia wakati ukikaribia kumalizika mwaka wa jana tasnia ya Sanaa ikapata pigo jingine ambalo ni kifo cha mwanamuziki nguri wa muziki wa dansi, Shen Karenga kilichotokea Desemba 15.
Mwanamuziki huyo aliekuwa amelazwa kwenye hospitali ya Amana akiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu alizikwa kwenye makaburi ya Kisutu.
Marehemu alikuwa akikumbukwa hasa kwa umahiri wake katika upigaji wa gitaa la solo na uimbaji, kipaji ambacho kilimwezesha kufanya kazi katika bendi mbalimbali za muziki hapa nchini akianzia na Bendi ya Lake Tanganyika Jazz mwaka 1964, na baadaye Bendi Maarufu ya Tabora Jazz ikijulikana zaidi kama Wana Segere Matata.
Kifo hicho kiliacha simanzi kwa wadau wa sanaa wa hapa nchini kutokana na mchango wa mwanamuziki huyo katika medani ya sanaa nchini.
Kifo kiliendelea kuwaandama wasanii tena ambapo mwaka huohuo Novemba 8, Khamis Kayumbu ‘Amigolasi mwanamuziki aliyewahi kutamba na bendi ya African Stars Twanga Pepeta alifariki dunia.
Alifariki akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya taifa ya Muhimbili, akisumbuliwa na magonjwa ya Moyo ambapo mara ya mwisho alikuwa ni mwanamuziki wa bendi ya JKT Ruvu Stars.
Mwaka jana pia alifariki msanii wa filamu Adam Kuambiana ambae alizikwa makaburi ya Kinondoni.
Msanii huyu alikuwa mahiri katika uigizaji hasa alikuwa pia ni mhasisi mzuri wa kazi za sanaa kwa ujumla huku akiwa anapigania zaidi kazi za wasanii wenzake.
Lakini pia mwaka huohuo pia alifariki mwigizaji mwengine aliekuwa akifahamika kwa jina la Rachel ambae nae alikuwa mchango mkubwa katika uigizaji.
Alizikwa katika makaburi ya Kinondoni pia ambapo maelfu ya watu walijitokeza kumwada msanii huyo ambae alikuwa akianza kuibukia kwa kasi katika tasnia hiyo.
Lakini pia itaka kutokea tena pigo jingine kwa kifo cha mchezaji mahiri wa muziki wa dansi nchini Aisha Madinda ambae kifo chake kiligubikwa na utata kadhaa.
Mwanadada huyo ambae alichangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha taswira ya watu katika kuwatazama wachezaji wa muziki huo.
Akiwa mwanadada mzuri aliwavutia wengi katika suala zima la uchezaji wa muziki na kujikuta akipendwa na kuchukuliwa ni kama mfano wa kuigwa.
Alipoteza maisha akiwa njiani kupelekwa hospitali na alizikwa katika makaburi ya Kigamboni mwaka huohuo wa jana.
Upande wa muziki wa Bongo Fleva Said Salum Hemed, Side Boy Mnyamwezi nae alipoteza maisha mwaka huohuo wa jana kwa ajali na hivyo kutoa pigo kwenye tasnia ya sanaa kwa upande wa muziki wa Bongo Fleva.
Ila pia msanii YP aliekuwa na kundi la Wanamume TMK pia alifariki mwaka huo huo wa jana.
Kwa ufupi mbali na kupatikana kwa mafanikio makubwa katika tasnia ya muziki kwa mwaka jana lakini pia kulikuwa na mengi ya hudhuni ambayo jamii pia ilikumbana nayo.
Kwa mwaka huu nie vema kwa wasani pia wakajipanga kuwa na mafanikio zaidi huku wale ambao Mungu aliwachukua kwa mwaka jana wapumzike kwa amani.