Mbinu mpya katika kutokomeza Ukeketaji

Bibi huyu alikuwa mkeketaji kwa sasa ameacha kazi hiyo

Mkurugenzi wa Tamwa kulia akiwa na Sister Germaine wa kituo cha Masanga kilichopo Tarime kinachosaidia waliokimbia ukeketwaji

Ms Tausi Hassan wa UNFPA akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Singida kabla ya kuanza kwa semina hiyo


Na Evance Ng’ingo   

UTAMADUNI wa wanaume katika baadhi ya mikoa kusisitiza kuoa wanawake waliokeketwa unaonekana umechochea kwa kiasi kikubwa kuendelea kwa utamaduni wa ukeketaji katika mikoa husika.

Hali hiyo kwa kiasi kikubwa imepelekea wazazi kuendelea kuhakikisha kuwa watoto wao wanakeketwa ili kujihakikikishia kuwa wanakuja kunufaika na mahali pindi watoto wao wafikiapo umri wa kuolewa.

Hali hiyo pia imepelekea wazazi hasa akinamama kuwa chanzo cha kuhakikisha kuwa watoto wa wa kike wanakeketwa ili mwisho wa siku kuepuka ugomvi kutoka kwa baba wa msichana husika ambapo wengi wao wamekuwa wakipingana na kuwa na watoto ambao hawajakeketwa.

Mkoa wa Singida ni moja kati ya mikoa ambayo imekuwa na tatizo hilo kwa muda mrefu na hasa kutokana na wanaume kusisitiza kuwa hawataki kuoa wanawake ambao hawajakeketwa.

Katika kukabiliana na tatizo la ukeketaji mkoani humo na mikoa mingine, imependekezwa kuwa inatakiwa kuwapo na kampeni ya kubadilisha utamaduni wa wanaume kupenda kuoa wanawake waliokeketwa ili mwisho wa siku kupunguza hali ya ukeketwaji wa wanawake mkoani humo.

Katika kongamano lililowashirikisha Wanasheria, Wakuu wa Wilaya pamoja na wadau wengine wa haki za binadamu ilibainika kuwa iwapo wanaume wakisema kuwa wapo tayari kuoa hata wanawake wasiokeketwa basi itapelekea wazazi kuacha kulazimisha watoto wao kukeketwa.

Diwani wa Viti Maalum wa kata ya Ikungi Singida mjini, Asha Munjori anasema kuwa mila potofu zinazoweza kubadilishwa ni chanzo kikubwa kinachoendeleza tatizo hilo.

Anasema kuwa umaskini umewafanya wazazi wengi kutegemea zaidi mahali zitokanazo na kuwaoza watoto wao na hawapo tayari kuona wanakosa mahali hizo.

Anaongeza kuwa kutokana na msisitizo huo wa wanaume kutaka kuoa wanawake waliokeketwa ndio unazidi kuchochea wazazi kuwakeketa kwa kuwa wanajua kuwa iwapo wakishindwa kufanya hivyo hawatawaoezesha na hivyo watakosa mahali.

“Sasa hapo unategemea nini zaidi iwapo kama wanaume wanasema kuwa wanataka wanawake waliokeketwa basi unakuta hata mwanamke mwenyewe anaona kuwa ni lazima akeketwe ili kujihakikishia kuolewa na wengine wanaona kuwa ni ufahali”anasema Asha.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kilichoandaa mkutano huo kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu duniani (UNFPA) imesema kuwa mkoa wa Singida una asilimia 51 ya ukeketaji.

Pia inaongeza kuwa Mkoa wa Manyara unaongoza kwa asilimia 71 ukifuatwa na Mkoa wa Dodoma ukiwa na asilimia 64.

Kisha unakuja mkoa wa Arusha una asilimia 59 na Singida asilimia 51 huku Mara ukiwa na asilimia 40.

Mkurugenzi Mkuu wa Tamwa Valerie Msoka anasema kuwa kwa sasa inahitajika mbinu nyingine zaidi katika kukabiliana na tatizo la ukeketaji wa wanawake katika mkoa huo na mikoa mingine iliyokithiri na suala hilo.

Anasema kuwa iwapo jamii ikielimika zaidi kuhusiana na suala hilo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuliondoa  katika jamii husika na hilo linaweza kufanikiwa kwa ushirikiano wa wadau na jamii husika.

“Tumekuwa tukiendelea na kuwaelimisha wadau wanaofanya kazi na wanajamii katika mazingira hasa ya vijijini kulikokithiri hali hiyo lakini kwa sasa tunaona kuwa tunatakiwa kubadilisha pia fikra za wanaume ili hatimae watangaze kuwa wanaweza kuoa hata mwanamke asiekeketwa”anasema Valerie.

Lakini pia anasema kuwa mila ya kubadilishwa sio hiyo tu ila pia kukabiliana na utamaduni mpya wa ukeketaji wa wanawake ambao kwa sasa umeanzia katika ngazi ya chini kabisa.
Hapo anamaanisha kuwa kwa sasa hasa watoto wachanga wameanza kukeketwa wakiwa bado wapo hospitalini.

Anasema kuwa utamuduni huo ndio mbaya zaidi kwa kuwa watoto wakiwa bado wachanga wanakeketwa na wahudumu wa afya hasa katika hospitali zilizopo kwenye mikoa iliyokithiri kwa suala hilo.

Utamadunia huo ndio hatimae umepelekea Kauli Mbiu ya mwaka huu kusema kuwa “Ushirikishwaji wa Wahudumu wa Afya katika kupiga vita Uketeketaji”.

Kuuli mbiu hii imekuja wakati mwafaka ambapo kwa sasa tunaambiwa kuwa kuna wahudumu wa vituo va afya ambao wamekuwa wakijihusisha na ukeketaji.

Hawa ni wale ambao wanapoona kuwa mwanamke aliefingua amejifunga mtoto wa kike basi kwao inakuwa ni wakati wa kuwakeketa hapo hapo lakini wanakuwa wameshawishiwa zaidi na wazazi wa watoto wenyewe.

Hiyo inatokana na kuona kuwa katika jamii wamebanwa kwa kiasi kikubwa na wanajamii katika kupinga vita ukeketaji na hivyo wanaona kuwa njia ya kufanikisha ukeketaji ni wakati wakiwa bado wachanga hasa ikiwa ni takribani siku mbili baada ya kuzaliwa au hata wakiwa wamezaliwa.

“Inasikitisha kuona kuwa hata wapo wahudumu wa afya ambao kwa sasa wamejikita nao katika kujihusisha na masuala hayo kwa hasa ikizingatiwa kuwa hao ni wasomi ambao wangetakiwa kupambana na suala hilo”anasema Valerie.

Anaongeza kuwa “ hasa wahudumu wanaojihusisha na suala hilo ni wale ambao wametokea kwenye maeneo ambayo yamekithiri kwenye ukeketaji ambapo wapo ambao nao wamekeketwa au wanaona kuwa ni jambo la heri kulingana na vile ambavyo wao wamekua wakiamini”.

Kwa kuwa ni imani  iliyojijenga hasa kwenye ile jamii iliyoathirika na ukeketaji  kuwa mwanamke asiekeketwa hafai kuolewa na ni sawa na mkosi katika jamii, dhana hiyo imeendeleza tabia ya ukeketaji.

Vita vya ukeketaji vinahitaji zaidi mabadiliko ya fikra hasa katika kubadilisha mawazo ya wahusika wakuu wa suala hilo.

Ili kufanikisha hilo inatakiwa wanasiasa kutumiwa zaidi hasa katika kuzungumza na wananchi.


Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Fatma Toufiq anasema kuwa kuna haja ya kuwa na vikao vya mara kwa mara na wananchi katika kulizungumzia suala hilo.

Anasema kuwa wapo wananchi ambao wanabadilika na kuacha lakini wanajikuta wakianza tena kuendelea na ukeketaji wa wasichana.

Anasema kuwa utamaduni uliowazunguka ndio unapelekea suala hilo kufanyika na kwa sasa anaotoa wito kwa wananchi uhakikisha kuwa hali hiyo inamalizwa.

“Mila Mila potofu ndio changamoto kubwa inayotukabili kwa sasa wananchi wa mkoa huu na hilo tunatakiwa kuliondoa ili kuwa na jamii bosa zaidi” anasema  Mkuu huyo wa wilaya ambae pia ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Women Wake Up.

 Huu ni wakati pia wa kutumika kwa nguvu za kisiasa pia hasa kwa kuwatumia viongozi wa kisiasa katika mikoa iliyoathirika zaidi na ukeketaji huo.

Kwa kuwa wapo baadhi ya wanasiasa ambao nao wamekulia kwenye mazingira ya kushuhudia ukeketaji huo labda wamekeketwa nao au walikuwa wakishiriki katika kukeketa baadhi yao wamekuwa wakilifungua macho suala hilo linaloendelea kwenye jamii zao.

Ni vema nao wakashiriki hasa kwa kuungana na kuweka katika moja ya kauli mbiu zao za uchaguzi kwa mwaka huu hasa kwa kusema kuwa piga vita ukeketaji kwa jamii bora hali ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha watu kuachana na ukeketaji huo.

Inasikitika kusikia kuwa wapo wasichana ambao wamekuwa wakikimbia kutoka katika jamii zao na kukimbilia katika maeneo salama hasa kwenye nyumba za imani kama makanisa kwa lengo la kuepuka ukeketwaji.
============

Related

Sticky 8351583069060099810

Post a Comment

emo-but-icon

item