Strong Girl kumtambulisha Diamond kimataifa zaidi

Na Evance Ng'ingo

MWANAMUZIKI wa mahiri wa muziki wa Bongo Fleva nchini Nasib Abdul anazidi kupanda chati kika kukicha ambapo amekuwa akishirikiana na wasanii wengi kutokea nje ya nchini ikiwa ni kama mkakati wake wa kukuza kipaji chake.

Msanii huyo ambae alianza kutambulika hapa nchini kwa kutumia wimbo wake wa Mbagala kwa sasa anafahamika karibia Afrika nzima kwa uwezo wake wa kuimba kwa sababu ameshirikiana na wasanii wa nchi za Afrika ya Magharibi.

Ni hivi karibuni msanii huyo ameandika historia ya sanaa yake kwa kushiriki katika wimbo uliolenga kubailisha mwelekeo wa viongozi wa Afrika katika kuwasaidia wanawake.

Katika wimbo huo uitwao Strong Girl Diamond Platnumz ameshirikishwa akiwa pamoja na wasanii wengine wakubwa akiwamo Bono ambae ni msanii mmoja kati ya wasanii wakubwa wanaotetea haki za binadamu.

Bono ni msanii wa Marekani ambae ni kiongozi wa kundi la muziki la U2 ambapo amekuwa akiimba kwenye matamasha mbalimbali makubwa ya muziki duniani.

Huyu ni mmoja kati ya wasanii wenye ushawishi mkubwa katika fani ya muziki nchini Marekani na kwengineko na amekuwa akiimba katika ubora wa hali ya juu.

Katika wimbo huo wa Strong Girl unalenga kuiambia dunia nzima kwa ujumla kuhusiana na uzuri wa kumwezesha mwanamke na kumsaidia kutimiza ndoto zake.

Ni wimbo ambao unawaambia viongozi kuweka vipaumbele vitakavyowawezesha wanawake kujiimarisha katika nyanja za kilimo, elimu, siasa, uchumi na mengine makubwa.

Kushiriki kwa Diamond katika wimbo huo ni inshara kuwa anajitangaza na kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kukuza sanaa yake pia huku akiwa anawatetea wanawake hao.

Akizungumzia kuhusiana na wimbo huo Diamond alisema kuwa ni heshima kubwa kwake kushiriki katika wimbo huo ambao umezungumzia kuhusiana na haki za wanawake katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

Anasema kuwa kushirikiana na wasanii wakubwa kama akina D' Banji, Bongo na wengineo mbali na kumtangaza zaidi lakini ametumia nafasi hiyo kufikisha ujumbe mkubwa kwa jamii ya wanawake na watu wengine katika kuendeleza na kulinda utu wa mwanamke katika jamii zao.

"Nawaomba watanzania na waafrika kiujumla wasikilize wimbo huu kwani ukimyanyua msichana na mwanamke, utakuwa umenyanyua kila mtu, na nina hakika viongozi wamesikia wito wetu wa kunyanyua wasichana na wanawake kama ajenda muhimu. Ni wakati wa kutekeleza sasa’ anasema Diamond.

Anaongeza kuwa "kwa kuurudia wimbo huu wa Msichana Imara, strong girl, kwa kuwashirikisha wasanii wa kike na kiume si tu unaongeza nguvu ya ujumbe bali unaweka msisitizo wa kumwezesha mwanamke  na kuonesha ushirikiano baina ya wanaume na wanawake kuhakikisha wasichana na wanawake wanainuliwa katika sekta tofauti hapa nchini".

Naye msanii D'Banj, anasema kuwa amejipatia heshima kubwa ndani na nje ya nchi yake kwa kushirikia kwenye wimbo huo wenye kulenga kusaidia mabadiiko ya dunia kwa kuonesha kuwa uwezeshaji wa wanawake ni suala la dunia nzima na ndio msingi mkubwa wa kuondoa umaskini uliokithiri.

Lakini pia Bono anasema kuwa "Wimbo huu ni zaidi ya wimbo au mwimbaji, na ni furaha kufahamu kuwa wakati wanamme ni sehemu ya tatizo, wamekuwa sehemu ya suluhisho’

Anasema kuwa ni wimbo ambao umemkutanisha na wasanii wengine wengi wakubwa wa Afrika na kuanza kuona mwanya  wa kufanya kazi nyingi zaidi na wasanii hao

"Ni mara yangu ya kwanza kuimba pamoja na wasanii wa Afrika na hiyo ni dalili kuwa kazi nzuri imeshafanyika na bado tutaendelea kuwa pamoja na wasanii wa Afrika katika kupigania haki za wanawake" anasema Bono.

Kwa upande wake D’Banj ambae ni moja kati ya wasanii wakubwa barani Afrika na kuwa amekuwa akiimba nyimbo nyingi za mapenzi pamoja na nyimbo nyingine za kijamii.

Anasema kuwa ni mara ya pili kukutana na Diamond katika sanaa kwa kuwa awali aliimba pamoja na Diamond katika wimbo wa kuhamasisha kilimo wa Chocolate.

Anaongeza kuwa kwa kuunganishwa pamoja katika wimbo wa Strog Girl ni wakati mwengine wa kuendeleza kazi za pamoja kati yake na msanii huyu wa Afrika Mashariki.

" Diamond ni msanii mkubwa Afrika na kwa kuimba nae tukiwa pamoja na Bono ni inshara ya kuanza kwetu kuimba pamoja katika harakati za kuendeleza wanawake ni inshara kuwa tutakuwa pamoja katika nyimbo nyingine nyingi zijazo" anasema D Banii.


Hivyo ni wimbo ambao umelenga kuwainua zaidi wanawake kutoka katika kila kona ya dunia na hivyo kwa kushirikishwa kwa msanii Diamond ni inshara kuwa wimbo huo unakuwa wa ukaribu zaidi na watanzania.

Pia katika wimbo huo mwigizaji wa filamu wa Nigeria Omotola Jalade ameshiriki kama video queen.

Strong girl ni wimbo ambao awali uliimbwa na wanamuziki wengine mahiri Afrika akina Vanessa Mdee, Arielle T, Blessing, Gabriela, Judith Sephuma, Selmor Mtukudzi, Victoria Kimani, Waje pamoja na  Yemi Alade.

Wasanii hao wameamua kufikisha ujumbe huo ukiwataka viongozi kuweka ajenda za maendeleo zinazozingatia usawa wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kuwaendeleza wanawake zaidi katika nyanja za uchumi, siaasa na maendeleo kwa ujuma.

Ujumbe huo wa wasanii hao unakuja wakati ikiwa mwaka huu malengo ya Milenia yaliyowekwa awali yakiwa yanafikia ukingoni na kwa sasa kunaundwa malengo mengine yenye lengo la kutoa dira kwa miaka mingine ijayo.

Kwa upande wa Umoja wa Afrika, AU, unaojumuisha nchi za Afrika wakuu wa nchi hizo walikwisha kukubaliana kuhusiana na njiambadala za kushugulikia umasikini unaoathiri zaidi wanawake.

=============



Related

Sticky 1536164547750306168

Post a Comment

emo-but-icon

item