Mkurugenzi
wa Maendeleo ya Biashara wa Twiga Bancorp, Solomon Haule akiongoza wafanyakazi
wa Twiga Bancorp kukabidhi funguo wa bajaji kwa kikundi cha Vikoba cha
Mfugandege cha Yombo Mchimbo wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo ya pikipiki na
bajaji kwa vikoba vya jijini Dar es salaam.
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Twiga Bancorp imetenga Shilingi bilioni
tano kwa ajili ya kuwakopesha wajasiliamali nchi nzima kupitia vikundi vyao.
Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi wa Maendeleo ya
Biashara wa benki hiyo Solomon Haule katika hotuba yake aliyoisoma niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo,
Cosmas Kimario wakati wa uzinduzi wa mikopo hiyo.
Uzinduzi huo pia ulienda sambamba na kukabidhi
mikopo ya bajaji na pikipiki kwa vikundi kadhaa vya vikoba vya jijini Dar es
Salaam, tukio lililofanyika katika tawi la benki hiyo lililopo Mlimani City.
Katika hotuba yake hiyo Haule alisema kuwa benki
hiyo imedhaminia kumkwamua mtanzania wa kawaida katika changamoto kubwa za
umaskini.
Alisema kuwa katika kutambua nafasi ya vikundi vya
ujasiriamali katika kuwaendeleza wananchi kukabiliana na umaskini benki hiyo
imeamua kutumia vikundi hivyo na kwa masharti ya nafuu.
Alisema kuwa benki ya Twiga inawasaidia bila ya
kuwawekea vikwazo kama vile kuhitaji hati ya nyumba, shamba au taarifa
zilizokaguliwa za kibenki ila wanachotaka kutoka kwao nia ya dhati ya katika
kutumia mikopo hiyo kujikwamua na umaskini.
“Benki mbali na kuwapatia mikopo pia inawapatia
elimu ya ujasiriamali inayojumuisha namna ya kutumia fedha zao kibiashara na
njia mbadala ya kurejesha mikopo kwa wakati” alisema Haule.
Aliongeza kuwa benki hiyo baadae itaanza kukopesha
mjasiliamali mmoja mmoja ambapo watalengwa zaidi wale wajasiriamali ambao
wametoka katika vikundi hivyo waliokwisha vikopesha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha Chama cha
Madereva wa Bajaji kilichopo Mikocheni kwa Kairuki (Chamabavi) John Roberto
ambacho kimekopeshwa bajaji moja alisema
kuwa chini ya utaratibu huo wamekwishapata bajaji nane.
“ Sisi tangia mwaka jana tumekuwa tunakopeshwa na
kisha tunarejesha kwa riba katika benki hii na baadae mwanachama huyo anaachiwa
bajaji inakuwa ni ya kwake moja kwa moja tumenufaika na mpango huu” alisema Roberto.
|