Benki ya Twiga yaingia Kariakoo
http://habari5.blogspot.com/2016/09/benki-ya-twiga-yaingia-kariakoo.html
Tawi la Twiga Bancorp Kariakoo |
Na Mwandishi Wetu
WAFANYABIASHARA wa
Kariakoo wametakiwa kutumia zaidi huduma za kibenki zipatikanazo katika eneo
hilo ili kurahisisha uwekaji na utoaji wa fedha kwa ajili ya maendeleo ya
biashara zao.
Mwito huo umetolewa na
Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Twiga, Cosmas Kimario wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusiana na uamuzi wa benki hiyo kufungua tawi lake
Kariakoo.
Alisema, Kariakoo ina
mzunguko mkubwa wa fedha ambao wafanyabiashara wakubwa na wadogo wamekuwa wakisaidia
mzunguko huo.
Alisema kuwa kutokana
na hali hiyo benki zimekuwa zikiwekeza zaidi katika sekta hiyo na kuwa zimekuwa
zikiendeleza wafanyabiashara hao katika uhifadhi wa fedha zao.
“Kwa sasa tunabiashara
kubwa pale Kariakoo ambayo lazima tuweke tawi. Biashara yetu kubwa ni utoaji wa
mikopo kwa uharaka kwa wafanyabiashara mbalalimbali, ubadilishaji fedha za
kigeni, utumaji wa fedha nje ya nchi” alisema Kimario.
Aliongeza, Twiga ikiwa
ni Benki ya serikali jukumu lake kubwa la kwanza ni kuhakikisha inchangia
ukuaji wa uchumi kwa kuwezesha biashara kuendela zaidi, kuinua sekta isiyo
rasmi kupitia mikopo ya vikundi, kuwapatia huduma bora za kibenki wananchi pale
walipo ili kuongeza na kupanua wigo wa matumizi ya tasisi za kifedha kwa
watanzania.
Aliongeza kuwa kwa
ufunguzi huo wa tawi Kariakoo, Twiga Bancorp itakuwa imewafikia wananchi wengi
wa eneo hilo hususani wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitembea kufuata huduma
zetu upande wa mjini kati Dar es Salaam na kuwanyima fursa baadhi ya wateja
kutoka maeneno ya Kariakoo, Ilala, na viunga vyake.
"Ufunguzi wa tawi
hili ni hatua mojawapo ya utekelezaji wa agizo la serikali lililoitaka benki
hii kujitanua zaidi katika utoaji wa huduma zake, kuimarisha utendaji, na sisi
tumeitikia kwa kuendelea na upanuzi wa huduma zetu kwa watanzania ambao
kimsingi ni benki yao hii" alisema Kimario.
=============