Seghito: Mwanamuziki, Mjasiriamali, Mbunifu wa Mavazi

TASNIA ya burudani inazidi kutanuka hasa kwa kutoa ajira kwa vijana ambapo wengi wamejiajiri katika tasnia hiyo kwa namna tofauti.

Kuna ambao wamejiajili kama waimbaji, wachezaji wa muziki, waimbaji, huku wengine wakiwa wamewekeza kwenye sekta hiyo kama njia mojawapo ya kujipatia kipato.
Wapo wasanii ambao wao wenyewe wameamua kuwekeza kwenye fani hiyo kwa kuanzisha bendi zao ili kutumia kama njia mojawapo ya kuongeza ajira kwa kuajili vijana wengine.

Mwanadada, Annette Ngongi jina maarufu katika sanaa anajulikana kama Seghito, ni binti wa miaka 26 ambae kwa sasa anamiliki bendi inayoendana na jina lake la kisanii, Seghito.

 Mwanadada huyu mrembo, ni mrefu wa wastani huku akiwa na mwili wa kisanii, macho mazuri pamoja kila aina ya sifa ya mwanadada hasa wa kiafrika kusifiwa.

Mwanadada huyu aliiona fursa kwenye tasnia ya muziki ambapo aliamua kuichukua kwa staili ya aina yake hasa sio tu kwa kuimba kama bendi lakini hasa kwa kuitumia bendi kama njia mojawapo  ya msingi katika kumuingizia kipato.
Kwa sasa anatamba zaidi katika sherehe mbalimbali akiwa kama mwimbaji anaeimba nyimbo za aina mbalimbali kuanzia za kigeni hadi kuimba zile zenye maadhi ya kiafrika, kinyumbani na hata za kwake mwenyewe.

Mwanadada huyu alianzia kuimba katika Nyumba ya Kutunzia Vipaji Tanzania (THT) ambapo alijiunga nayo mwaka 2010 hadi kuja kuachana nayo mwaka 2011 kabla ya kwenda kusomea Shahada ya Biashara na Masoko Chuo Kikuu Tumaini Iringa.

Akiwa THT aliona kadi iliyokuwa ikifanywa na wasanii wakati huo akina Elias Barnaba, Mwasiti Almasi, Maunda Zorro, Linah Sanga na wengineo ambao kwa pamoja walimfanya kuvutiwa zaidi muziki.

Anasema, akiwa THT alinolewa na mwalimu wa wasanii chuoni hapo Kanali Gento ambae alikuwa akimwelekeza thamani ya vyombo vya muziki hasa katika kunogesha muziki wa dansi, anasema kuwa alifundishwa matumizi ya vyombo hivyo.
Anasema kuwa aliingizwa kwenye bendi ya THT na alijikuta akifanya kazi kwa ukaribu zaidi na wasanii kama vile akina Wahu wa Kenya, Chameleone wa Uganda na wengineo wa hapa nchini.

Anaongeza, "kwa kuwa nilikuwa nikipenda muziki tangia mdogo basi hiyo ya kujiunga na THT ilikuwa ni kama ndio imefungua mlango wa mafanikio ya muziki kwa kiasi kikubwa na nilifanya hivyo kabla ya kwenda kusoma".
Anasema, hata alipoondoka THT kwenda Iringa kusoma aliitumia elimu ya THT kuendeleza zake yake kwa kujiunga na bendi ya The Sweet Noise ya mkoani humo.

"Yani ni sawa na kuwa nimeikuta kazi ninayoipenda na kuanza kuifanyia kazi sasa nimemaliza kidato cha sita nikaanza muziki THT, sasa nimeanza kusoma Chuo Tumaini nkajiunga na bendi na sasa ninaendelea na masomo hapa Chuo Kikuu Huria nikisomea Shahada ya Uzamili katika uendeshaji wa miradi ninamiliki bendi yangu" anasema Seghito huyo.
Bendi yake hiyo ya No String Attached Band, imekuwa ikijihusisha zaidi na uimbaji katika maharusi, matukio muhimu pamoja na hafla kadhaa anazoalikwa.

Kupitia bendi hiyo ameshiriki matamasha makubwa mbalimbali kama vile Jahazi, Barazani na mengineo mengi huku akifanya kazi kwa ukaribu zaidi na hoteli za Hyatt Regency pamoja na Mgahawa wa Akemi.
Anasema kuwa yeye ni mmoja kati ya waasisi wa muziki wa Jazz na Afro Soul kwa hapa nchini kwa kuwa wakati anajikita kwenye muziki huo ulikuwa ni bado haujatamba na kupigwa sana kwa muda huo.

Anasema kuwa kwa sasa kupitia staili yake hiyo amekuwa akialikwa kwenye  hafla tatu au zaidi kwa wiki na amekuwa akizitendea haki shoo zake hizo kwa kuimba vema zaidi.

"Kwa mtu akikodisha kuimba kwenye harusi yake hakika hatojutia kuniita kwenye hafla yake kwa kuwa nina mbinu mbalimbali za kibunifu katika uimbaji, naweza kukutungia wimbo wako hapo hapo kulingana na zima nzima ya hafla husika" anasema Annette.

Anasema kuwa " ikiwa ni harusi ninaweza kuimba na kucheza na pia hata kukutungia wimbo hapo hapo wa harusi yako huku nikiimba na waimbaji wangu wa bendi, lengo likiwa ni kuiboresha kazi zaidi".

Anaongeza amekuwa akijiongezea kipato cha kusukuma maisha yake kwa kuwa anaichukulia kazi yake anayoifanya ni sawa na shughuli nzima ya kiujasiliamali.

Anasema kuwa ameimba nyimbo zake nyingi alizoshirikiana na wasanii kadhaa huku nyingine akiw ameshirikishwa kama vile alioimba na Ochu, pia upo wimbo alioimba na Cliff  Mitindo uitwao Sogea sogea.

Pia ana wimbo alioimba na Florence wa Cheza za Leo itafahamika, Don't Let Go pamoja na Bora uende huku akiweka shauku yake kufanya kazi na wasanii kama vile akina Barnaba,Carols Kinasha na Dunga Santuri,

Licha ya kuwa na mwelekeo mzuri katika medani ya muziki lakini mwanadada huyo anaweka wazi kuwa anakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile, kutokufahamika kwa muziki na kupewa heshima stahiki.

Jamii kutoipa heshima inayostahili fani yake ya muziki
huku akikumbana na changamoto ya ucheleweshwaji wa malipo ya kazi zake za muziki pamoja na kutopewa kipaumbele kwa nyimbo za aina anayoimba kwenye vituo vya radio.

Annette ambae pia ni mbunifu wa mavazi yenye nakshi za kiasili anasema kuwa kama isingekuwa anaipenda kazi yake ya muziki basi angekuwa ameshaacha na kwenda kufanya kazi za uigizaji aua uhanaharakati wa Haki za Wanawake na Watoto.

Akizungumzia kuhusiana na ubunifu wake wa mavazi anasema kuwa anabuni nguo za wanawake kwa wanaume na akuwa anaipenda kazi yake hiyo na analenga kuwa mbunifu wa kimataifa.

Katika baadhi ya mambo ambayo anayapenda ni pamoja na kusoma vitabu, kucheza kikapu pamoja na kubadilishana mawazo na watu mbalimbali huku akiweka wazi kuwa anapenda kula Pilau Nyama.

Related

Sticky 78440782341307806

Post a Comment

emo-but-icon

item