Elizabeth: Mjasiriamali alielenga kuimarisha ufugaji.
http://habari5.blogspot.com/2017/01/elizabeth-mjasiriamali-alielenga.html
Bi Elizabeth akiwa na wafugaji wa kuku wa mayai |
Elizabeth (mwenye koti jeupe) akiwa kwenye ziara ya kutembelea
moja ya miradi ya kiufugaji, hapa alikuwa Vingunguti Dar es Salaam.
|
Huyu ndio Mjasiriamali Bi Elizabeth Swai |
Na Evance Ng'ingo
SEKTA ya ufugaji kwa muda mrefu imekuwa ikichukuliwa ni kama sekta ya kawaida ambayo haina mchango mkubwa sana kwenye kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja.
Lakini kwa sasa kumekuwa na fursa nyingi zaidi katika sekta ya ufugaji ikinufaisha wafuagaji wengin wa ngazi tofauti toka wadogo, wa katikati na wakubwa.
Pia wapo wanawake ambao wamezishika fursa zipatikanazo katika ufugaji kujihusisha katika sekta hiyo kwa njia tofautitofauti zikiwapo za kujinufaisha au kuwanufaisha watu.
Elizabeth Swai, amejikita katika sekta ya ufugaji kwa kuuza vyakula vya kuku, kutotolesha vifaranga, kutoa huduma za ugani, kutoa nafasi ya masoko ya mayai, na na pia kutoa huduma nyingine zinazohusiana na ufugaji.
Yeye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya AKM Glitters Limited inayojihusisha na bidhaa za ufugaji pamoja na utengenzaji wa chakula cha kuku, hiyo kwake sio tu biashara kama biashara ila ni shughuli ambayo ameisomea pia.
Mwanama huyu alianzisha kampuni hiyo mwaka 2006 ambapo ikiwa ni baada ya kuacha kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la WFP (Shirika la Chakula duniani).
Elizabeth anasema aliamua kuacha kazi kwa nia hasa ya kutoa huduma hizi kwa wakulima na wafugaji ambao ndio wengi katika taifa katika nia ya pamoja ya kupunguza umasikini na kuongeza kipato cha watanzania. Mama huyu aliona fursa kubwa katika sekta ya ufugaji.
Anasema kuwa akiwa na WFP alikuwa na nafasi nzuri na ambayo alikuwa akiona kuwa ingeweza kuendelea kumpatia mshahara mzuri na kujiwezesha zaidi kimaisha lakini nafsi yake ilikuwa na msukumo tofauti wa kuweza fikia wengi katika kuboresha vipato vyao kupitia shughuli ya ufugaji.
Anaweka wazi kuwa aliona kuwa akiwa na ofisi hiyo ni sawa na kuwa alikuwa hafanyi yale ambayo alikuwa akitakiwa kuyafanya kwa undani zaidi na hivyo kuamua kuacha kazi na kufanya kazi zake.
Anaweka wazi kuwa ikiwa ni baada ya kuifanyia kazi ofisi pamoja na ofisi nyingine zilizo chini ya Umoja wa Mataifa kwa miaka 17 alipata ujuzi wa mambo mbalimbali na ndio yaliyomwezesha kuanzisha kampuni yake hiyo.
Anasema kuwa pia aliwahi kufanya kazi na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR, akiwa anafanyia kazi zaidi mkoani Kigoma
Akizungumzia kuhusiana na historia ya kampuni yake hiyo ya ufugaji, anasema kuwa alianzisha kampuni hiyo kwa kuwa alikuwa na shauku pia ya kusaidia jamii ya wafugaji.
Anasema kuwa baada ya kuianzisha mwaka 2006 na kuanza kazi rasmi ikiwa imesajiliwa mwaka 2007, alifanya kazi kwa muda na kisha mwaka 2009 hadi 2012 aliamua kujiendeleza zaidi katika elimu ya masuala ya ufugaji.
Mama huyu anaamini katika taarifa sahihi kwa kupitia elimu na warsha mbalimbali ambazo zimewea kumpanua uwezo wa kufikiri na kupanga mikakati ya kampuni yake. Mama huyu ana digrii ya Maendeleo ya Jamii, ujasiriamali, hoteli na menejiment ya ofisi, elimu ya ukatibu muhtasi, elimu ya hesabu na biashara na elimu ya menejiment na nyinginezo. Pia ana elimu ya ufugaji kuku katika ngazi ya diploma.
Anasema, alianza biashara yake hiyo akiwa ameweka kipaumbele zaidi katika nidhamu ya kazi yake hiyo.
Anasema kuwa amekuwa akiiona kampuni yake hiyo ikikua siku hadi siku na kisha kuja kufikia hatua ya kufahamika na kuendeleza kazi kwa ufanisi zaidi.
Kwa sasa imekuwa ikiendeshwa sio tu kama ofisi ila ni kama pia mradi wa kuwasaidia wafugaji wa kuku na wakulima.
Katika shughuli zake za kuelimisha katika suala zima la ufugaji wa kuku anasema kuwa ameweza kuwafikia wafugaji kutokea mikoa ya Morogoro, Tabora, Dodoma, Simiu, Singida, Manyara, Shinyanga vijijini, Dar es Salaam, Pwani nk pamoja na sehemu mbalimbali za Tanzania.
Lengo la kampuni hii kubwa ni kuwaona wafugaji wa kitanzania wanakuwa kiuchumi na kunufaika na kila kile kitokanacho na sekta hiyo kuanzia mifumo hadi sera za kuwainua wafugaji"anasema Elizabeth.
Anaongeza kuwa"kampuni hii imekuwa mstari wa mbele kusikiliza sauti za wafugaji na kuziwakilisha kwa wahusika na hasa kwa wale wanaosimamia shughuli za kiserikali katika wilaya husika".
Lengo lake katika miaka miaka minne kuanzia January 2017 mpaka 2021, Elizabeth akishirikiana na wadau wake wakuu kama serikali, Tanzania ambako atafungua mawakala wanawake 25 katika kila mkoa ili kufikisha huduma za ugani vijijini na kufungua mlango wa biashara na wafugaji kibiashara.
Anasema kuwa kampuni yake hiyo imekuwa ikiwatumia vijana kutokea vyuo vya ufugaji na kilimo katika kutoa elimu hiyo kwa wafugaji hasa wa mikoani.
Anasema kuwa kila mwaka wamekuwa wakichukua wanafunzi zaidi ya 50 ambao wanawaongezea ujuzi kuhusiana na masuala ya elimu na kisha kuwapeleka mikoani kuwafundisha wafugaji.
Anasema, vijana hao wamekuwa wakiishi vijijini hadi kwa muda wa miezi mitatu ambapo moja kati ya vitu wanavyowafundisha wafugaji ni pamoja na utunzaji wa fedha.
Anasema kuwa kwa kuwa wafugaji wamekuwa wakipata faida kutokana na ufugaji wao huo, hivyo kuna umuhimu wa kuwaelimisha kuhusiana na suala zima la kuendesha biashara hiyo pamoja na kuimarisha vikoba vyao.
Anaweka wazi kuwa kupitia kampuni yake hiyo amekuwa akiwaelekeza wafugaji kuhusiana na namna ambavyo wanaweza kunufaika na fedha za serikali zitolewazo kwa wafugaji.
"Najua kuna fursa nyingi katika ufugaji na hasa huu wa kuku kwa kuwa kwanza ni miradi ambayo imekuwa ikiwainua kimaisha wafugaji wengi na hivyo AKM Glitters Company imekuwa ikiwaelezea wafugaji ni wapi kuna fursa wanazoweza kunufaika nazo" anasema Elizabeth.
Akizungumzia kuhusiana na ni kwa namna gani anaweza kusimamia familia pamoja na shuguli zake hizo, anaweka wazi kuwa yeye ni mama wa mtoto mmoja aliyemaliza digrii ya sheria, hivyo jukumu lake lililobaki ni moja tu kufanya kazi kwa bidii na uaminifu.
Anasema kuwa kama mwanamke mjasiriamali anakumbana na changamoto mbalimbali lakini anasimama na kuzishinda kwa kuwa amekuzwa katika misingi ya kutafuta.
Kutokana na umahiri wake huo katika sekta ya ufugaji amejikuta akishirikiana na wadau wengine mbalimbali katika kuanzisha miradi kadhaa ya kuwasaidia wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla.
Yeye ni mwanzilishi wa mtandao wa Mtandao wa Wanawake wa Afrika wanaojihusisha na Kilimo na pia ni mmoja wa waanzilishi wa Africa Agriculture Academy.
Anawataka wanawake kujitambua na kuwa na nia ya kufanikisha kila kile wanachoamua kukifanya. Anakerwa na wanawake wasiothamini wanawake wenzao au kudharau nguvu ya pamoja.
Mwanamke anatakiwa awe na moyo wa upendo na kusimamia haki bila kujali udini, kabila au nafasi ya uwezo katika jamii. Anasema kuwepo na wanawake kuwatukuza wengine wa nje ya nchi huku wakidharau kuwainua watanzania wenzao.
Anawataka wanawake kuwa na hali ya kujiamini, kujiona ni sawa na wajasiriamali wengine, kujiheshimu pamoja na kujiendeleza kielimu.
Lakini pia anachukizwa na tabia ya watu wanaokula fedha za serikali zinazolenga kuwasaidia wafugaji na kutaka kuona kuwa fedha hizo zinakwenda moja kwa moja kwa wafugaji husika.
Anamuomba Rais John Magufuli kuhakikisha kuwa anaitazama sekta hiyo ya wafugaji ili katika harakati zake za kuwa na Tanzania ya viwanda aone kuwa hiyo sekta inaweza kuchangia katika kufufua maeneo ya serikali yaliyowekwa kwa ajili ya ufugaji kuku.
Anasema kuwa zipo taasis za kifedha ambazo zinaweza kuwasaidia wafugaji lakini kunakuwa na changamoto kadhaa inazowawezesha kufanikiwa katika hilo.
Kwa upande wake Elizabeth ametoa ajira ya kudumu kwa wafanyakazi wake 46 huku akiwa amejipanga kuajili wafanyakazi wengine 77 watakaokuwa na jukumu la kuhudumia wafugaji katika mradi mkubwa anaotarajia kuuanzisha mwezi ujao.
Elizabeth mbali na kutumia muda wake mwingi kufanya kazi na kusaidia jamii ya wafugaji lakini mwanadada huyo anapenda pia kujihusisha na masuala kadhaa ya kijamii.
Anapenda kusikiliza muziki hasa zile za live band na nyimbo za vijana wetu. Inafurahisha kuona jinsi ambavyo vijana wetu wanachangai katika pato la taifa kwa kutumia vipaji vyao.
Anapenda sana kusoma vitabu pamoja na kuangalia filamu na hasa vyote vile vyenye kuchochea mfumo chanya.
Mwanadada huyu anaonekana kuwa ni nadhifu na mwenye kujipenda pia hasa akiwa anaamini kuwa kila anachoweza kukifanya ni lazima akifanikishe kwa nguvu zake bila ya kutegemea uanamke wake ila uwezo wake kwa kuwa anaamini kuwa anaweza, ataweza na lazima aweze.