Twende, huduma ya simu inayowakutanisha wateja na madereva
http://habari5.blogspot.com/2017/01/twende-huduma-ya-simu-inayowakutanisha.html
Justine Kashaigili (mwenye shada la maua) wakati
akiwa mdogo, hapo alikuwa akisoma shule ya msingi
|
MAENDELEO ya teknolojia nchini yamepelekea simu kutokuwa kifaa cha mawasiliano peke yake ila imefikia hatua ya kuwa ni kifaa kinachotumiwa kwa ajili ya kufanyia miamala ya kifedha ikiwa ni pamoja na teknolojia nyingine mbalimbali.
Hiyo inatokana na mawazo mbalimbali ya kibunifu ambayo yameingizwa na kutumiwa kwenye simu hizo kwa ajili ya kukuza wigo wa matumizi ya simu.
Ubunifu huo wa kiteknolojia umewanufaisha watu wengi zaidi nchini hasa ikizingatia kuwa idadi ya watumiaji wa simu wamekuwa wakiongezeka kila kukicha. Tanzania ni nchi ambayo imeunganishwa kidigitali zaidi na hasa kwa njia ya simu za mkononi zaidi ya mfumo wa kikompyuta.
Kwa mujibu wa takwimu kutokea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), watumiaji wa simu za mkononi wameongezeka kutoka Milioni 2.96 kwa mwaka 2005 na kufikia milioni 36.01 Juni 2016.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa sekta ya mawasiliano inakua kwa kasi nchi na kusaidia kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 21 katika kipindi cha miaka mitano na kuchangia pato la taifa kwa asilimia 1.2 mwaka 1999.
Ikaja kusaidia kwa asilimia 1.7 mwaka 2005 huku mwaka 2009 ikiongeza kwa asilimia 2.7 na mwaka 2012 iliongeza pato kwa asilimia 3.5.
Mambo makubwa yaliyopelekea kuwapo kwa hamasa hiyo kwenye matumizi ya simu na hivyo kupelekea ongezeko la pato kutokea nyanja hiyo ni matumizi mbadala ya simu ambayo yanachagizwa na teknolojia na kupelekea simu kuwa kifaa zaidi ya kifaa cha mawasiliano tu.
Kijana Justine Kashaigili ni moja kati ya vijana ambao wametumia teknolojia katika kuja na mbinu mbadala zenye kulenga kutatua kero ya usafiri kwa hapa nchini.
Kashaigili anasema kuwa kwa sasa sehemu mbalimbali za hapa nchini kumekuwa na changamoto kadhaa katika suala zima la usalama wa watumiaji wa huduma za usafiri. Anasema kuwa huku usafiri mkuba ukiwa ni wa Taksi, Bajaji na Pikipiki maarufu kama bodaboda bado aina hiyo ya usafiri inakabiliwa na changamoto kadhaa.
Anasema amebuni mbinu ya kiteknolojia, App iitwayo Twende ambayo inamkutanisha abiria na dereva wa usafiri kirahisi zaidi ambapo abiria akitumia simu yake ya kisasa za aina ya Smartphone anaweza kupakua huduma hiyo kwenye Google play store na kisha kujisajili ili kutumia huduma hiyo.
Anasema "Chini ya msaada wa Tume ya Sayansi na Teknolojia pamoja na kampuni ya simu za mkonouni ya Tigo, huduma hii inawakutanisha kirahisi zaidi madereva wa taksi, bajaji au bodaboda na wateja wao, ambao waanakuwa karibu na eneo alipo na kisha anaweza kuwasiliana nae kirahisi na kukubaliana bei".
Kutokana na ubunifu huo, Kashaigili ameajiri wafanyakazi sita wanaoshirikiana nae katika kutoa huduma hiyo anasema, baada ya kubaini ukubwa wa tatizo hilo ambalo aliliona tangia akiwa chuoni aliumiza kichwa katika kutafuta njia mbadala zenye kulenga kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa madereva wa Bajaji eneo la Mwenge, Jonathan Henry anasema kuwa, App hiyo imemkutanisha na wateja wengi kirahisi zaidi kwa kuwa anawaona kwenye simu yake ya Smartphone na kisha kupanga nao bei.
Anasema, kwa sasa madereva wenzake wa bodaboda wanafurahia huduma hiyo kwa kuwa inawahakikishia usalama zaidi dhidi ya wateja wasiokuwa waaminifu wenye kudhuru madereva.
"Najua inakuwa ni rahisi zaidi kumkamata mteja ambae amemkodisha dereva wa bajaji na kisha kumdhuru au hata kumuibia bajaji kwa kuwa taarifa za kila mteja zinarekodiwa kwenye teknolojia hii ya Twende" anasema Henry.
Nae Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Bajaji wa Feri. Juma Bilal anaweka wazi kuwa kwa kuwa wanafanya kazi kwenye maeneo ya mijini hasa hapo Posta na Feri, kunakuwa na wateja ambao wanataka kwenda nje ya Posta na Feri ambapo kupitia huduma hiyo.
"Binafsi nikiwasha simu na kwa kuwa nimeshapakua App hii basi ninawaona wateja wote ambao nao wanakuwa Online na kuna wateja ambao wananipigia simu kwa kuwa wanakuwa wameniona kwenye simu zao nikiwa Online basi wananipigia simu, wapo wanaosema wanataka kwenda Masaki na tunajadiliana bei kisha kazi inafanyika" alisema kijana huyo.
Akizungumzia zaidi kuhusiana na teknolojia yake hiyo, Kashaigili ambae ni mhitimu shahada ya Computer Science, DT 228 kutokea Chuo cha Utawala wa Fedha, IFM anasema, kuwa tangia akiwa mwaka wa kwanza chuoni hapo huo ukiwa mwaka 2011 alikuwa akikerwa na changamoto za usafiri unaowakumba wakazi wa jiji.
Anasema hali hiyo ilikuwa ikimkera na hasa zaidi wakati akiona wananchi wakiwa wanasumbuliwa kujadiliana bei na wato huduma za usafiri.
"Najua ilikuwa ni kuwa mtu anaweza kusimamisha taksi au bajaji na hapo ndipo anaanza kujadiliana bei wakati huo huo ni muda unakuwa unapotezwa hapo wakati wakijadiliana bei, lakini pia kama mtoa huduma akikataa kuafiki bei iliyopendekezwa basi mteja anakuwa hana jinsi nyingine zaidi ya kuendelea kungojea usafiri mwengine" anasema kijana huyo.
Anasema kuwa wakati akiwa chuoni hapo akiendelea na masomo yake alianza kutafuta mbinu mbadala ya kutatua kero hiyo na kwenye andiko la mradi wake kabla ya kutunukiwa shahada aliamua kubuni mradi unaolenga kujibu kero hiyo.
Anasema kuwa tayari bajaji 1500, taksii 1000 pamoja na bodaboda 50 zimeshajiunga na huduma hiyo huku kwa upande wake akishirikiana na wafanyakazi wake wamejipanga kuhakikisha kuwa huduma hiyo inawawezesha watanzania.
Anasema kuwa abiria hatolazimika kumpatia fedha mtoa huduma ya usafiri iwe bajaji, taksi na daladala ila atafanya malipo yake moja kwa moja kwenda kwenye akaunti maalum ya Twende ambao ndio wanajukumu la kumlipa mtoa huduma.
Anasema kuwa hiyo inasaidia zaidi kudumisha huduma kwa kwa kama iwapo wangekuwa wanalipwa moja kwa moja huenda ikawa na shida.
Anasema kuwa ofisi ya Twende ndio itakayopokea fedha hizo na kisha kuzilipa kwa mtoa huduma, lakini hata hivyo anasema kwa kwa mteja ikifikia elfu 50 anaweza kupewa fedha yote.
Twende App hivi sasa inatoa mbadala sahihi wa malipo kupitia Tigo Pesa kwa namba binafsi za Tigo Pesa kwa madereva na inapatikana katika mfumo wa Android na hivi karibuni itapatikana kwa watumiaji wa simu zilizo na mfumo wa iOs.
“Nimesukumwa na kasi ya maendeleo ya miundo mbinu na nguvu ya ujasiriamali hapa nchini. Ninategemea kuwapatia wakaazi wa jiji la Dar es Salaam chaguo wanalolimudu, rahisi na linalofaa kwa ajili ya usafiri salama.”
Anasema kuwa malipo hayo yanafanywa kwa njia ya Tigo Pesa na mteja anaweza kutumia simu yake hiyo katika kutoa maksi kuhusiana na mwenendo mzima wa mtoa huduma huyo na kwa wale ambao watalalamikiwa kampuni yake itawaondoa usajili wao kwenye huduma hiyo ya Twende.
Mkuu wa Zana za Kidijitali wa Tigo Tawonga Mpore anasema, “Huduma hii ni kielelezo cha Tigo kujikita katika mageuzi ya mtindo wa maisha ya kidijitali kwa kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili watumiaji wa usafiri wa nchi kavu".
==========