Jamaa nusura ajirushe kutoka juu ya nguzo


SUALA la matatizo ya kimaisha ni changamoto ambayo inamkuta karibia kila mtu maishani lakini kwa huyu mkazi wa Kipera Mkoani Morogoro Hassan Kibwana limeonekana kuwa la kufunga mwaka.
Jamaa huyu alipanda juu ya mnara wa simu na kutishia kujirusha chini akishinikiza kutaka kuonana na Rais Kikwete ili afikishe madai aliyonayo.
Tukio hilo lililodumu  kuanzia saa 5.10 hadi saa 6.50 asubuhi lilitokea eneo la Ubungo ndani ya eneo la Shirika la Viwango Tanzania (TBS) mahali ulipo mnara huo na kusababisha maelfu ya wananchi kuacha shughuli ili kushuhudia kihoja hicho.
Kwa mujibu wa mmoja wa wafanyakazi wa Kampuni ya ulinzi inayolinda eneo la TBS ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake, alisema awali mtu huyo alionekana akirandaranda katika eneo hilo huku akiwa na ngazi yake fupi mkononi.
Alisema ghafla alimuona mtu huyo akiweka ngazi hiyo pembeni ya uzio uliozunguka nguzo hiyo na kuanza kupanda ambapo hata hivyo alifanikiwa kumfukuza.
“Lakini wakati naendelea na shughuli zingine ghafla alipanda ngazi kwa haraka na kurukia ndani ya uzio na kuanza kuupanda mnara huo kwa kasi huku tukimpigia kelele za bila mafanikio tukimtaka ashuke” alisema mlinzi huyo.
Hatua hiyo ilisababisha wananchi walioko eneo hilo wakiwemo wasafiri waliokuwemo ndani ya mabasi kupigwa na butwaa kutokana na kitendo cha mtu huyo huku baadhi wakionekana kuwa na hofu ya pengine mtu huyo angetimiza ahadi yake ya kujirusha kama mamlaka za usalama zingechelewa kufika eneo hilo.
Hata hivyo askari wa kikosi cha zima moto na uokoaji cha Halmashauri la Jiji la Dar es salaam wakiwa na gari No. SM 9484 walifika katika eneo hilo na kupanda juu ya mnara huo na kufanikiwa kumshusha chini huku akiwa amefungwa kamba mikononi na kumwingiza katika gari ya Polisi  na baadae gari hiyo kuondoka naye katika eneo hilo .
Iliwalazimu askari hao wa kikosi cha zimamoto na uokoji kutumia nguvu za ziada ili kumdhibiti mtu huyo aliyeamua kuanzisha mapambano dhidi ya askari hao huku akiwa juu ya mnara huo kabla ya kuzidiwa nguvu na kushushwa.
Akielezea sababu za kufanya tukio hilo Kibwana alisema kusudi la yeye kupanda juu ya mnara huo ni kumtaka Rais Kikwete afike hapo ili aweze kusikia kilio chake.
“Polisi walinisingizia kesi ya kuua na kusababisha nifungwe jela miaka sita huko Morogoro, nimekwenda kumuona Mkuu wa Mkoa Kalembo hajanipa msaada wowote zaidi ya kunitaka nifikishe malalamiko yangu kwa rais sasa mtu kama mimi ningewezaje kumuona rais ndiyo maana nimeamua kufanya hivi ili aje” alisema Kbwana.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Camilius Wambura alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa bado wanaendelea kumuhoji mtuhumiwa huyo na baadae watamfikisha mahakamani kujibu tuhuma na kupanda juu ya mnara huo na kutishia kujiua.

Mtazamo wanguNi vema kukawa na vituo kadhaa kwa ajili ya kusaidia ushauri nasaha kwa watu ambao wanakumbwa na msongo wa mawazo  ili kuepuka kadhia kama hizi.
ends

Related

Jamii 453769926525090125

Post a Comment

emo-but-icon

item