Safari njema Lowassa
http://habari5.blogspot.com/2014/01/safari-njema-lowassa.html
Na John Mhala, Monduli
MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa amesema ameanza safari yake jana yenye matumaini makubwa kwa Watanzania, lakini yenye vikwazo vingi, ingawa anasema ana uhakika wa kufika na kushinda.
Lowassa alisema hayo jana katika Ibada ya shukurani yake na familia yake, kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Monduli mkoani Arusha.
Ibadala hiyo ilikwenda sanjari na harambee ya ujenzi wa hosteli na zilipatikana zaidi ya Sh milioni 89. Lowassa alisema safari aliyoianza jana, ana uhakika wa kufika salama na kushinda; Ina matumaini makubwa kwa Watanzania kwa kuwa itakuwa na elimu bure, maji safi na salama, huduma za afya zenye uhakika lakini safari hiyo ina vikwazo.
Alisema atakapofika salama na kushinda katika safari hiyo, huduma hizo zitapatikana bila shaka yoyote.
Alisema pamoja na miiba, mabonde na makorongo makubwa na milima, Bwana Yesu ni kiongozi katika safari hiyo, hivyo ana uhakika wa kufika na kushinda.
Alisema kila binadamu ana malengo katika maisha na hakuna asiyejua malengo yake katika maisha na ndoto zake.
‘’Nina malengo ya maisha yangu na malengo hayo hakuna asiyejua na nina faraja kubwa na malengo na ndoto zangu, nina uhakika wa kufika katika safari ninayoanza na kushinda kwa kuwa mbele ya safari hiyo anaiongoza Bwana Yesu Kristo,’’ alisema bila ya kufafanua.
Akizungumzia Rasimu ya Katiba, Lowassa aliliomba Kanisa kuiombea ijadiliwe kwa amani na upendo.
Kaimu Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Mchungaji Solomon Massangwa aliomba Serikali kutoa ruzuku kwa shule za dini, kwa kuwa zina mchango mkubwa kwa jamii.
Mchungaji Massangwa alizungumzia pia suala la Serikali, kutoa dawa katika hospitali za dini kuwa utoaji unacheleshwa na kufanya hospitali hizo kukosa dawa kwa muda fulani.
Maoni ya Mhariri
Nakupongeza Lowasa kwanza kwa kumtanguliza Mungu mbele katika kila jambo na inatakiwa kuhakikisha kuwa unazidi kujitaidi ili kufikia katika hiyo safari yako ndefu na yenye mafanio.
Lakini pia ambavyo unaendelea kujihusisha na masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi ikiwa pamoja na kuendeleza harakati za kuhakikisha kuwa maendeleo yanapatikana.