Clouds FM yatoa msaada kwa Hospitali Temeke na waathirika wa dawa za kulevya
http://habari5.blogspot.com/2014/01/clouds-fm-yatoa-msaada-kwa-hospitali.html
Mmoja kati ya waathirika wa dawa za kulevya akitoa ushuhuda wake mbele ya wafanyakazi wa kituo cha Clouds Fm |
Wakiwa katika hospitali ya Temeke pamoja na wagonjwa |
Walipewa zawadi ya Kuku kutoka kiituo cha kusaidia waathirika wa dawa za kulevya kilichopo Keko |
Millard Ayo akiwa amebeba mtoto katika wodi ya watoto Temeke |
Kituo cha Redio namba moja hapa nchini, Clouds FM leo kimefikia kilele cha mwezi wa maadhimisho ya miaka 14 toka kimeanzishwa.
Maadhimisho hayo ambayo yamefanyika kwa mwezi mzima sasa, yalianza na watangazaji wa vipindi tofauti kwenda mikoa mbalimbali ili kuweza kusherekea miaka hii 14 pamoja na wasikilizaji wao sehemu walipo.
Leo ikiwa ndio siku ya kilele cha maadhimisho hayo, Clouds FM imetembelea hospitali ya Temeke na kituo cha kuhudumia vijana wanaotumia madawa ya kulevya cha Keko Youth, ambapo misaada mbalimbali imetolewa.
Wakiwa katika hospital ya Temeke, Clouds FM imetoa vifaa mbalimbali vya hospitali katika wodi ya wanawake na watoto, huku Keko Youth wakipewa vitendea kazi ambavyo vitawezesha vijana kujiajiri baada ya kumaliza matibabu.
Akizungumzia maadhimisho hayo ya Clouds FM, Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga alisema sherehe hizi kwa mwaka huu ni za kipekee kwa Clouds FM hasa kwa kuwa wameweza kufanikisha mambo mengi makubwa toka walipoanza.
‘Maadhimisho haya ya miaka 14 kwa mwaka huu yana lengo moja kubwa, kuwashukuru wasikilizaji wetu kwa kutufikisha hapa tulipo, na ndio maana tumeanza kwa kuwapa misaada wanaohitaji, halafu tunamalizia kwa burudani’’ alisema Kusaga.
Akielezea zaidi mafanikio ya Clouds FM kwa kipindi cha miaka 14, Kusaga alisema redio imefanikiwa kuwafikia watu wengi zaidi, imeongeza ubunifu lakini pia kumekuwa na uboreshaji wa hali ya juu wa mitambo ya kutangazia pamoja na maudhui.
‘Kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo tumefanikiwa kushinda tuzo ya Super Brand, na kwa mwaka huu pekee radio imefanikiwa kuanza kusikika mikoa ya Njombe, Songea, Njombe, Sumbawanga, Katavi na Geita, kupitia mitandao kwa wasikilizaji wetu nje ya nchi lakini pia tumefanikiwa kufanya tamasha la Fiesta kwa mafanikio zaidi’ alisema Kusaga.
Kusaga pia aligusia mchango wa Clouds FM katika kuhamasisha maendeleo na uzalendo hapa nchini akitoa mfano wa semina za Fursa ambazo zilifanikiwa kwenda nchi nzima zikizungumza na vijana kuamka na kuchangamkia fursa katika sehemu wanazoishi.
‘Semina za Fursa zimekuwa mfano mkubwa namna Clouds FM ilivoweza kutumia nguvu yake kama radio inayosikilizwa zaidi katika kuchagiza maendeleo, na kwa hakika mafanikio ya semina yamekuwa ni makubwa sana’ alisisitiza Kusaga.
Kusaga pia alitoa shukrani za pekee kwa watanzania kwa kuinga mkono Clouds FM sio kwa kusikiliza tu bali hata katika kuhudhuria matamasha na shughuli nyingize za Clouds.
Kilele cha maadhimisho ya miaka 14 ya Clouds FM kitamalizika kwa burudani kubwa ambayo itafanyika katika viwanja vya Mwembeyanga ambayo itajumuisha wasanii na watu wengine maarufu.
‘Kumekuwa na mafanikio makubwa katika redio yetu kwa kipindi cha miaka 14, na naomba niseme, bila ninyi wasikilizaji wetu tusingeweza kufika hapa’ alimaliza Kusaga