Yanga yamchukua Juma Pondamali kuwanoa makipa wake
http://habari5.blogspot.com/2014/01/yanga-yamchukua-juma-pondamali-kuwanoa.html
Pondamali akitoa mafunzo ya kudaka |
Huyu ndo Juma Pondamali |
KLABU ya Yanga katika kuendelea na harakati zake za kuriimarisha benchi la ufundi la klabu hiyo, imemchukua kocha wa makipa wa timu ya Taifa Stars Juma Pondamali kuwa kocha wa makipa wa timu hiyo.
Kocha huyo anaungana na Kocha Msaidizi wa timu hiyo Boniface Mkwasa katika kuwanoa wachezaji wa Yanga ambapo leo hii wanatokea hadharani kwa mara ya kwanza katika uwanja wa Bora Kijitonyama.
Yanga ililazimika kuwatimu kazi kocha wake mkuu Ernest Brandits pamoja na kocha msaidizi Felix Minziro kufuatiwa kufungwa 3-1 na Simba katika mechi yake dhidi ya Simba katika kuwania taji la Nani Mtani Jembe.
Kufuatia hali hiyo Yanga ilijikuta ikilazimika kutopeleka timu yake katika michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyoanza wiki hii kisiwani Zanzibar.
Akizungumzia kuchaguliwa huko kufundisha makipa wa Yanga, Pondamali alisema kuwa kwake ni hatua muhimu kuwanoa makipa wa timu hiyo.
Alisema kuwa akiwa kama kocha wa makipa aliebobea anaenda Yanga kuleta mapinduzi na sio kufanya mzaha.
"Mimi kwanza nataka hao makipa pale wajue kuwa naenda pale kufanya kazi na sio lelemama sitaki mzaha kwanza sitaki kabisa kufanya kazi za kimzahamzaha nataka kwenda pale kupiga mzigo".alisema Pondamali.
Alisema kuwa akiwa kama kocha wa makipa atahakikisha kuwa anaimarisha nafasi hiyo muhimu na kuona kuwa hakuna kufungwa kimzahamzaha.
Aliongeza kuwa leo anaungana na Mkwasa katika kuanza kazi ya kunoa kikosi hicho ambacho ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Leo kazi ni pale pale Bora na naomba sana kuhakikisha kuwa kitakachoendelea hapo ni mazoezi ya kufa mtu"alisema Pondamali.
Kwa sasa Yanga inaendelea kutafita nafasi nyingine kama vile hiyo ya Kocha Mkuu ambayo ipo wazi na inasemekana kuwa inatafuta kocha mzungu wa kufanya kazi hiyo.
Mkwasa aliwahi kuionoa timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars pamoja na Ruvu Shooting na kuwa pamoja na Pondamali katika timu hiyo huenda ikawa mwanzo mzuri wa kuimarisha Yanga ambayo inaonekana kupoteza mwelekeo.
Mbali na Pondamali kukubali kuteuliwa kukinoa kikosi hicho hata hivyo msemaji wa Yanga Baraka Kiziguto alionekana kukwepa kulizungumzia hilo hasa akisisitiza kuwa hizo ni habari za mitaani tu na zisizokuwa na ukweli.
Maoni ya Mhariri
Haya naipongeza Yanga kwa kumchukua Pondamali na Mkwasa lakini je kufukuza ndio suluhisho la tatizo? manake naona kwanza imemfukuza kocha Mzungu Brandits huku Minziro nae akipewa mkono wa kwaheri.
Pia Yanga imeshindwa kuhudhuria michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kukosekana kwa benchi la Ufundi Imara na sijui kama wachezaji wameipokea hiyo vema au je ni kwa nini hawakuiandaa timu B vema ili ishiriki.
Mimi naona kuwa Yanga inatakiwa kujipanga na kuwa na mikakati muda mrefu ya kusaka mafanikio na hivyo iondokane na uchukuaji wa hatua za harakaharaka kama hizo za kufukuza makocha.
Lakini hata hivyo nawatakiwa maandalizi mema waliochaguliwa kuchukua nafasi za akina Brandits na Minziro ambao ni Mkwasa na Pondamali