Jaji Mkuu kusikiliza rufani ya Seya februali 12
http://habari5.blogspot.com/2014/01/jaji-mkuu-kusikiliza-rufani-ya-seya.html
JOPO la majaji watatu limependekeza rufaa tatu ikiwemo ya mwanamuziki maarufu nchini mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanawe zizingatiwe wakati wa kutafsiri vifungu vya sheria katika rufaa ya mfanyabiashara Kibute Otienyeri anayepinga kifungo cha maisha jela.
Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Mkuu Othman Chande, jaji Benard Luanda na Bethuel Mmila wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya Otienyeri aliyehukumiwa baada ya kupatika na hatia ya kunajisi.
Katika uamuzi wao majaji hao walipendekeza rufaa hiyo isikilizwe mbele ya majaji watano ili kupata tafsiri sahihi ya vifungu vya sheria vinavyotumika wakati watoto wadogo wanatoa ushahidi mahakamani.
Katika kutafsiri vifungu hivyo, majaji hao walielekeza rufaa tatu zitiliwe maanani ikiwemo rufaa namba 56/2005 ya Babu Seya na mwanawe Johnson ‘Papii Kocha’ wanaotumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi watoto, Rufaa nyingine ni za Herman Hanjewele na Hammis Shaban.
Jopo hilo litalosikiliza rufaa hiyo Februari 12 mwaka huu litaongozwa na Jaji Mkuu Chande, Ibrahim Juma, Bethuel Mmila, Kipenka Mussa na Engela Kileo.
Katika rufaa hiyo, inadaiwa Agosti 23 mwaka 2008 saa 4 asubuhi Katika kijiji cha Manyiri, Arumero mkoani Arusha, Otienyeri alimnajisi mtoto wa miaka 11.
Ilidaiwa siku hiyo, mtoto huyo alitumwa na dada yake aende sokoni akanunue nyanya, akiwa njiani alikutana na mshitakiwa ambaye alimuita na kumuingiza kwenye kibanda na kumnajisi.
Baada yakupitia ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa jamhuri na utetezi wa mshitakiwa ambaye hakuwa na shahidi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimtia hatiani mshitakiwa na kumuhu kifungo cha maisha jela.
Mshitakiwa hakuridhika na uamuzi huo na kukata rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ambapo Jaji Kakusulo Sambo alisema ameamini ushahidi uliotolewa n mtoto kuwa ni wakweli na hukumu iliyotolewa ilikuwa sahihi.
Hata hivyo Otienyeri alikata rufaa Mahakama ya Rufani mbele ya jopo la majaji watatu ambao walipendekeza isikilizwe mbele ya jopo la majaji watano.
Mwisho.