Kuchapiwa siri ya ndani msiielewe vibaya - Mavoko
http://habari5.blogspot.com/2014/01/kuchapiwa-siri-ya-ndani-msiielewe.html
Kijana Rich Mavoko akifanya vitu vyake jukwaani |
Rich Mavoko akiwa na mama yake Sharo Milionea |
Na Mwandishi wa Sanaa
KWA sasa moja kati ya
nyimbo ambazo zinatamba sehemu mbalimbali katika baa, kumbi za sherehe na hasa
katika klabu za usiku ni wimbo wa Roho Yangu.
Wimbo huo ulioimbwa
na msanii Rich Mavoko ni wimbo unavuma kwa sasa huku ukiwa unapendwa zaidi
kutokana na maneno yaliyogusiwa kwenye wimbo huo.
Ni wimbo ambao
unahusiana na masuala ya mapenzi huku ukiwa umekuja na mtazamo tofauti kuanzia
ujumbe na hata mtiririko wa wimbo wenyewe.
Mavoko ni kijana
ambaye amekuwa akifanya vema kwenye medani ya muziki ambapo anazo nyimbo nyingi
kwa sasa.
Ana nyimbo kadhaa,
lakini kwa wafuatiliaji wa muziki, wimbo wa Marry Me ndio hasa uliomtambulisha
kwenye soko la muziki kwani ndio uliovuma kuanzia mwishoni mwa mwaka juzi mpaka
mwaka jana, baadhi ya nyimbo zake nyingine ni
Silali na One Time.
Katika mahojiano hayo
maalum, Mavoko anazungumzia wimbo wa
Roho Yangu na kusema kuwa hakutarajia kama wimbo huo ungepokelewa kwa
shangwe na mashabiki wa muziki.
Anasema kuwa aliamua
kuuimba wimbo huo kutokana na kugundua kuwa wapo watu wengi wanaotatizwa kwenye
mapenzi na wanashindwa kujitoa katika mahusiano hayo.
Anasema kuwa wapo
ambao wanakumbwa na visa vingi ikiwamo kudanganywa na mengineo lakini bado tu
wanaendeleza masuala ya mahusiano.
Anasema kuwa hiyo
ndio moja ya sababu zilizofanya kuutunga wimbo huo wa Roho Yangu.
Anasema kuwa ni wimbo
ambao una maana kubwa ingawaje kuna watu ambao wamekuwa wakiuchukulia kwa maana
tofauti au wakizingatia kipengele kimoja zaidi.
Katika wimbo huo kuna
maneno ambayo ndio hayo ambayo Mavoko anasema kuwa yanachukuliwa tofauti.
Maneno kama vile
mjini msingi kiuno, kuchapiwa siri ya ndani na maneno kama vile Ujanja kunywa
supu ya pweza.
Anasema kuwa ni
maneno ambayo yalikuwa kwa muda mrefu yakitumiwa lakini hayakuwahi kupewa
kipaumbele kwa kuonekana kuwa ni maneno yenye maana gani zaidi.
Anasema kuwa msemo
kama vile mjini msingi kiuno ni hakuwa na maana kuwa anawaelekeza watu
kujiingiza kwenye ngono kibiashara kwa maana ya kutumia mwili wao kujiletea
maendeleo.
Ila anafafanua kuwa
maana yake ni kuwaelezea baadhi ya vijana tena wakiume ambao wanatumia miili
yao kama ndio msingi.
Akiwa na maana kuwa
wanalelewa na kutunzwa na wanawake huku wao mtaji wao ukiwa ni viuno vyao.
"Najua nikisema
Roho Yangu ndani yake kunakuwa na ujumbe wa aina mbalimbali, kama vile kuwaasa
mengi vijana na watu katika suala zima la mapenzi hapa nikiwa na maana kuwa
yale ambayo nimeyagusia humu yanatakiwa kueleweka kiumakini zaidi,"anasema
Mavoko.
Anaendelea kufafanua
kuwa hata akisema kuwa ujanja ni kunywa supu ya pweza anawalenga kuwasaidia
wale vijana ambao hawana uwezo mkubwa wa masuala ya mapenzi.
Anasema kuwa kwa
kuhakikisha kuwa wanalinda heshima zao ni kuhakikisha kuwa wanakunywa supu ya
pweza na ndio maana amesema kuwa ujanja ni kunywa supu ya pweza.
Mavoko pia anautetea
ujumbe usemao kuchapiwa ni siri ya ndani, ambao kwa sasa unaonekana kutajwa
tajwa sehemu mbalimbali na watu wanaonekana kuuchukulia ni kama ujumbe muhimu
katika maisha ya mahusiano.
Mavoko anaongeza kuwa
iwapo kama mtu akijikuta anakutana na masahibu kama hayo anachotakiwa kufanya
ni kutambua kuwa hiyo ni kama suala jingine na kulitatua kwa ndani ya mazingira
husika.
Anasema kuwa wapo watu
ambao wanayachukulia masuala kama hayo ya kukuta mpenzi, mchumba au mke
kutembea nje ya ndoa na wanaanza kuyangumza kwa marafiki au watu wengine badala
ya kuifanya siri ya ndani.
Anasema kuwa akisema
kuwa kuchapiwa ni siri ya ndani hana maana kuwa wanatakiwa wakae kimya na
kuyachukulia masuala hayo kama ya kawaida, bali iwe siri ya ndani na itatuliwe
kwenye misingi ya kifamilia zaidi.
Akizungumzia maisha
yake anasema kuwa kwa sasa ana mchumba wake ambaye sio mdau wa mziki kabisa.
"Mimi natarajia
kuoa na kwa sasa nina mtu wangu ambae ndio ninapanga nae maisha huyu ni
mwanadada ambae kwanza haendekezi haya masuala ya muziki na sio mdau sana wa
shughuli hizi,"anasema Mavoko.
Anaongeza kuwa yeye
ni msanii ambaye analenga kuwa na familia bora atakayemheshimu mkewe na familia
yake kwa ujumla.
Gazeti hili
lilipotaka kufahamu upande wa pili wa
maisha yake binafsi kama msanii anapenda kitu gani na kipi hatumii kabisa
Mavoko 'alifunguka'…
"Sipendi kunywa
pombe wala kuvuta sigara mimi ni msanii ninayetumia muda wangu mwingi kukaa
ndani kujifunza zaidi muziki".
Anaongeza kuwa hiyo
inamsaidia zaidi kujiweka karibu na watu mbalimbali na kupata mawazo ya nyimbo
mpya za kuimba.
Anaongeza kuwa kwa
sasa amejenga nyumba kubwa kwa wazazi wake mkoani Morogoro na pia amenunua gari
ambalo analitumia kwa maisha yake.
"Muziki
umenisaidia kununua gari, kupata shoo nyingi nje ya nchi hasa kwa mwaka huu wa
2014 tayari nimeshaweka kwenye ratiba hiyo ya kwenda nje ya nchi kama Uingereza
na kwengineko,"anasema Mavoko.
Anatumia fedha zake
nyingi katika kuvaa na kuhakikisha kuwa anakuwa na mwonekano wa kisanii kila
mara.
Anaongeza kuwa yeye
anajitambua kama msanii makini na mwenye nia ya kufika mbali na ndio maana hata
wimbo wake wa Roho Yangu ameutengenezea video yenye umakini wa hali ya juu.
Anasema kuwa
alilazimika hata kurekodi kwa kutumia Kamera ya kisasa zaidi kutoka Kenya huku
akiwa na mwongozaji wa utengenezaji wa video ya wimbo wake huo kutoka Uganda.
Anaamini kuwa umakini
ndio kitu ambacho kinaweza kumsaidia msanii kufika mbali kikazi zaidi.
Aidha Mavoko kwa
upande mwingine alimkumbuka msanii marehemu Khamis Mkiety, 'Sharomilionea'.
Anasema kuwa msanii
huyo alikuwa rafiki yake mkubwa na mtu
wake wa karibu zaidi na kuongeza kuwa kifo chake kinaendelea kumuuma hadi sasa.
Mwisho./fm
I LOVE THAT SONG..... KUDOS RICH MAVOKO.....AND I DIDNT KNOW U LOOK SO HOTT!!!
ReplyDelete