yanga yaomba radhi zanzibar kwa kukacha kombe mapinduzi.



 Uongozi wa Klabu ya  Yanga ya Dar-es-Salaam umeomba radhi kwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwa kushindwa kushiriki katika mashindano ya kombe la Mapinduzi kwa
ajili ya kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa na Makamo Mwenyekiti wa timu hiyo Clement Sanga wakati
alipokabidhi jumla ya sh.Milioni 10 kwa ajili ya kusaidia mchango wa Mapinduzi na
kufanikisha mashindano hayo.

Alisema Yanga ni miongoni mwa klabu zenye historia kubwa ya Zanzibar ambapo
aliyekuwa rais wa kwanza wa Zanzibar hayati Abeid Amani Karume alitoa mchango mkubwa
wa kuanzishwa kwa klabu hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo lake.

'Kwa niaba ya uongozi wa klabu ya Yanga na Mwenyekiti mwenyewe tunaomba radhi kwa
kushindwa kuhudhuria mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambapo sisi ni sehemu ya wadau
wakubwa.......tumetingwa na harakati za maandalizi ya mashindano ya klabu Bingwa ya
Afrika'alisema.

Alisema klabu hiyo imeshindwa kushiriki katika kombe la Mapinduzi baada ya kamati
yake ya ufundi kuvunjwa na hivyo kukosa mwalimu ambaye ataongoza timu hiyo kwa ajili
ya kombe la Mapinduzi.

'Sababu moja kubwa iliyopelekea kushindwa kuhudhuria kombe la Mapinduzi ni kuvunjwa
kwa kamati ya ufundi ambapo walimu wote walifukuzwa kwa hivyo ilikuwa vigumu sana
kuja Zanzibar bila ya mwalimu'alisema.

Mapema akipokea fedha hizo,Makamo wa pili wa rais ambaye ni mlezi wa kombe la
Mapinduzi balozi Seif Ali Iddi amevitaka vilabu vya soka nchini kuepuka migogoro
isiyokuwa na lazima kwa ajili ya kuendeleza mchezo wa soka nchini.

Alisema migogoro na mivutano katika soka ni sawa sawa na migogoro katika vyama vya
siasa ambayo itavuruga maendeleo na kuimarisha vyama hivyo katika kuelekea kwenye
uchaguzi.

'Naishauri klabu ya soka ya Yanga kuepuka migogoro katika soka ambayo daima kazi
yake kubwa kurudisha maendeleo ya soka'alisema.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haikufurahishwa na kitendo cha Yanga
kukacha mashindano hayo zaidi kutokana na timu hiyo pamoja na Simba kuwa na
mashabiki wengi na mvuto katika maendeleo ya soka nchini.

'Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea ombi lenu la kuomba radhi kutokana na
sababu mbali mbali ikiwemo migogoro iliyoibuka hivi karibuni'alisema balozi.

Sanga alisema klabu ya Yanga inaondoka nchini kuelekea Uturuki kwa ajili ya kupiga
kambi maandali ya mashindano ya kimataifa.

Alisema timu hiyo imekubaliana na uongozi wa kombe la Mapinduzi kwamba itakuja
Zanzibar na kucheza mechi tatu za kirafiki ambapo mapato yatakayoingia yatakwenda
moja kwa moja katika mfuko wa kombe la Mapinduzi.

mwisho.




Related

Michezo 6275712582314347874

Post a Comment

emo-but-icon

item