Yanga yashushwa kileleni
http://habari5.blogspot.com/2014/01/yanga-yashushwa-kileleni.html
MATOKEO ya 1-0 iliyopata timu ya Azam FC yameiwezesha timu hiyo kuitoa Yanga kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Azam ilipata ushindi huo dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora katika mchezo uliochezwa katika uwanja wake wa nyumbani, Chamazi.
Bao la Azam lilifungwa kupitia mchezaji wake Kipre Tcheche dakika 26 ya mchezo.
Mchezaji huyo alifunga bao hilo kwa shuti kali kufuatia mpira uliowagonga mabeki wa Rhino na kutua miguu mwa Tchetche.
Kufuatia matokeo hayo Azam kwa sasa ina pointi 33 huku Yanga ikifuatia kwa pointi 32.
Hali ilikuwa mbaya kwa Yanga baada ya kumalizika kwa mchezo wake dhidi ya Coastal Union ya Tanga bila ya kufungana.
Katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga uligubikwa na kero mbalimbali kama vile washabiki wa Yanga kurusha chupa uwanjani pamoja na tiketi za electroniki kushindwa kufungua milango.
Yanga ilibanwa zaidi na Coastal hasa katika ushambuliaji ambapo washambuliaji wa Yanga walionekana kushindwa kufurukuta.
Timu hizo mbili ambazo zote zilikuwa nje ya nchi zikijandaa na mzunguko huu wa pili wa Ligi, Yanga ilikuwa Uturuki huku Coastal Union ilikuwa Oman zikijiandaa na ligii hii zilishindwa kuoneshana ubabe katika mchezo huo wa jana.
Kwa upande wake Mbeya City imetoka kwa sare ya 1-1 na Ruvu Shooting mchezo uliochezwa katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Kwa sasa Mbeya City inakuwa na pointi 31.
Katika mchezo kati ya Mtibwa Sugar na Kagera Sugar uliochezwa katika Uwanja wa Kaitaba timu hizo zilitoka bila ya kufungana.