Zari All White Party ilivyofana
http://habari5.blogspot.com/2015/05/zari-all-white-party-ilivyofana.html
Na Evance Ng'ingo
MOJA kati ya matukio makubwa ya burudani ambayo yemetokea hivi karibuni ni hafla ya Zari's White Party ambayo ilihusisha vazi jeupe na iliandaliwa na mwanadada Mganda aishie hapa nchini Zari Hassan
Mwanadada huyo ambae kwa sasa ana mahusiano ya kimapenzi na gwiji wa muziki wa Bongo Fleva, Nasib Abdul, Diamond aliandaa hafla hiyo kwa lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali wa fani tofauti tofauti
Hafla za White Party zilianzishwa nchini Marekani na mwanamuziki wa muziki wa Hip Hop wa nchini humo Sean Combs maarufu kama Puffy Daddy ambapo ilikuwa ikiwakutanisha watu mbalimbali wakiwa kwenye vazi hilo
Kwa hapa nchini mwanamitindo Frank Mgoyo maarufu kama Frank Gonga alianzisha hafla kama hizo za White Party ingawaje alikuwa akiandaa kwa watanzania waishio nje ya nchi.
Aliandaa zaidi nchini Sweden na kisha mwaka juzi aliandaa moja hapa nchini ambapo mwanadaa Zari Hassan alikuja kama mwalikwa.
Kwa Zari mwaka jana aliandaa hafla hiyo nchini Uganda ambapo Diamond alihudhuria na kisha kwa mwaka huu amekuja kuandaa hafla hiyo hapa nchini.
Zari ambae ni Mjasiriamali, Mdau wa Mitindo na Muziki hafla yake hiyo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa mwenyewe akikiri kuwa ni zaidi ya hata ilivyokuwa nchini kwake Uganda.
Anasema kuwa hakutegemea kama kwa hapa nchini angeweza kupendwa na watanzania kwa kiasi kikubwa namna hiyo na kisha kuungwa mkono kwenye hafla yake hiyo
Anasema kuwa alikuwa akifikiria kuwa hafla yake hiyo ambayo ameamua kuifanyia hapa nchini ingekuwa ni kama hafla nyingine za kawaida na sio kama ambavyo ilikuja kupokewa kwa namna hiyo.
Moja kati ya vitu ambavyo huenda vilimchanganya mwanadada huyo ni pamoja na namna ambavyo alikuta maandalizi pamoja na wingi wa watu katika Ukumbi wa Mlimani City ambapo hafla hiyo ilifanyika
Wakati akiwa anazungumza kuwashukuru watanzania waliohudhuria ukumbini hapo anasema kuwa watanzania wameonesha upendo kwake kama ambavyo wanamuonesha upendo msanii Diamond.
Kabla ya kupanda jukwaani kuanza kutoa shukrani zake alikaribishwa kwa kuimbiwa nyimbo huku watu waliohudhuria ukumbini hapo wakipiga kelele za kumkaribisha jukwaani
Mwanadada huyo ambae kwa sasa ni mjamzito alipowasili jukwaani kabla yote alianza kutokwa machozi na kushindwa kuongea kwa dakika kadhaa.
Alipoanza kuzungumza moja kati yavitu ambavyo viliwavutia watu wengine ukumbini hapo ni aliposema kuwa yeye ni kama mtanzania kwa kuwa amebeba mtoto wa Mtanzania akiwa ana maana kuwa anamimba ya Diamond
Mbali kushukuru alioondoka jukwaani hapo na ikaanza rasmi burudani ambapo msanii Sheta alianza kwa kuimba nyimbo zake kadhaa ukiwamo wa Shikorobo. Burudani huyo iliendelea kwa muda na kisha akapanda msanii Diamond tena kwa kuimba.
Lakini kabla ya hapo alikuwa jukwaani msanii Rubby ambae aliimba wimbo wake mmoja wa Maumivu Yangu na alizikonga nyongo za wapenzi wa burudani ukumbini hapo.
Ilikuwa ni burudani safi huku asilimia kubwa ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo walikuwa wamevalia nguo nyeupe kuanzia juu mpaka chini.
Burudani haikuanzia hapo bali nje ya ukumbi kulikuwa na jukwaa ambapo kuna baadhi ya wasanii walilitumia kuimba
Pia kulikwa na Red Carpet ambapo wanamuziki, waigizaji na wageni mbalimbali walipata nafasi ya kupiga picha
Kwa ndani kulikuwa na mahala pa watu waliokata tiketi za Milioni tatu, Milioni Moja na kisha pa watu wa elfu hamsini
Ili kuhakikisha kuwa kila mmoja anafurahishwa na sherehe hiyo kulikuwa na huduma za baada za aina mbili ambapo moja ilikuwa ni ya watu wote huku pia kukiwa na nyingine sehemu ya watu waliolipa milioni tatu
Jukwaa la milioni tatu lilikua ni kama lipo juu kidogo kwa kuwa lilifungwa na kuwekewa ngazi kwa ajili awatu kukaa, lakini pia kulikuwa na ulinzi wa kuwazuia watu waliolipa kiingilio cha chini kwenda kuona raha za VIP
Burudani ilikuwa ni ya kipeke zaidi hasa pale ambapo Diamond alianza kupigana vijembe na msanii Nay wa Mitego hasa baada ya kuimba wimbo wao wa muziki.
Wimbo huo walianza kubishana kuhusiana na suala zima la ni nini muhimu katika mapenzi hasa Diamond akisema kuwa Mapenzi ni ujuzi na uwezo wa kumtuliza mwanamke na Naye wa Mitego akisema kuwa mapenzi ni fedha
Wakiwa wanaendelea kupigana vijembe Diamond alitetea hoja yake kwa kumchukulia mfano dansa wake kuwa amempa ujauzito Aunt Ezekiel huku watu wenye fedha zao wakiwa wameshindwa hata kupata nafasi hiyo.
Nay alitolea mfano kwa Jackline Wolper kuwa alimtoroka mpenzi wake baada ya mpenzi wake huyo kufilisika wakati wakiendelea kurumbana huko jukwaani watu walikuwa wakishangilia kwa shangwe kila msanii alipokuwa akitoa kijembe.
Diamond aliposema kuwa "mbona wewe Nay umeachwa na mwanamke licha ya kumuonga kila kitu na lakini kakukimbia na kwenda kuolewa na mwanamme mwengine" watu walishangilia kwa shangwe.
Wasanii wakati wakiingia ukumbini hapo walikuwa kwenye magari tofauti ya kukodiwa na kifahari ambayo hutumika kwenye hafla mbalimbali kubwa.
Katika magari hayo ya milango sita la kwanza kulikuwa na wasanii kama vile TID, Bob Junior, Dito, Makomandoo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda.
Pia siku hiyo kulikuwa na burudani kutoka kwa msanii wa Afrika Kusini maarufu kama AKA ambae aliimba nyimbo zake za Hip Hop.
Akizungumza na gazeti hili baada ya kumalizika kwa onesho hilo, Meneja wa Diamond, Babu Tale anasema kuwa idadi ya watu waliohudhuria shoo hiyo ni kubwa ikilinganishwa na party yoyote ya kiingilio cha juu kuwahi kutokea hapa nchini.
Anasema kuwa kila kitu kilienda sawa na watanzania wameonekana kufurahishwa na kila kitu katika hafla hiyo kuanzia muziki, burudani, ratiba na mipangilio yote muhimu.
Kabla ya kuanza kwa onesho hilo saa mbili usiku gazeti hili kuanzia mida ya saa 12 ilitembelea baadhi ya maduka ya Sinza, Kinondoni na Mwenge kuona ni kwa kiasi gani nguo nyeupe zimenunuliwa.
Maeneo hayo ni maarufu kwa mavazi ya vijana wengi ambao wamekuwa wakienda kununua nguo katika maduka makubwa ya mavazi ya vijana
Asilimia kubwa ya maduka hayo nguo nyeupe zilikuwa zimeisha hasa suruali aina ya jeans na makoti, wengi walisema kuwa mavazi hayo yamenunuliwa zaidi siku kadhaa kabla ya shoo hiyo na wengi walikuwa wakisema kuwa ni kwa sababu ya Zari White Party
" Yani ningeshtukia ningehakikisha kuwa ninaagiza mzigo mkubwa kwa ajili ya watu wanaotaka nguo kwa ajili ya hafla hiyo kwa kuwa inaonekana kuwa ni watu wengi wamejitokeza kununua zote nilizokuwa nazo hapa" anasema mmoja ya wauzaji wa nguo Mwenge.
Kwa upande wake Zari anasema kuwa anapenda kufanya shoo hiyo kila mwaka na amevutiwa na hamasa ya Watanzania katika kusherehekea.
================