Sheria Ngowi na Edna wawafunda wanamitindo
http://habari5.blogspot.com/2015/06/sheria-ngowi-na-edna-wawafunda.html
Wakiwa kwenye picha ya pamoja |
Sheria Ngowi akiwafunda somo wanamitindo |
Wakapata nafasi ya kupiga nae picha |
Na Evance Ng'ingo
WANAMITINDO wanaochipukia nchini wametakiwa kujitambua pamoja na kuwa na mikakati ya kujitangaza zaidi ili kupata soko la ndani na nje ya nchi.
Wito huo ulitolewa jana na Mwanamitindo mahiri wa mavazi nchini Sheria Ngowi wakati akizungumza na Wanamitindo kutoka kampuni ya Black Fox Model Africa.
Ngowi pamoja na mtaalamu wa urembaji Edna Ndibarema wa kampuni ya Ndiba Style walialikwa na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, ya Black Fox Model Africa, Aj Mynah kuzungumzia fursa zilizopo katika tasnia hiyo.
Ngowi aliwataka wanamitindo kuichukulia kazi hiyo kuwa ni sawa na kama kazi nyingine zenye kipato licha ya kuwa kwa hapa nchini ni fani ambayo inazidi kukua kwa kasi.
Alisema kuwa akiwa kama mwanamitindo ametembea nchi mbalimbali kuonesha mavazi na amekutana na wanamitindo mbalimbali wa kimataifa ambao walianza kufanya kazi hiyo wakiwa kama wanamitindo wa kawaida.
Alisema kuwa ili wanamitindo wa Tanzania nao kufikia hatua kama hiyo wanatakiwa kuwa na mikakati mingi ya kujitangaza ambapo aliwataka kutumia zaidi vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kujitangaza.
Alisema kwa kwa kutumia mitandao kama Twiter, Facebook, Instagram pamoja na tovuti nyingine mbalimbali kubwa wanamitindo wanaweza kujijengea jina na kutumiwa na makampuni mbalimbali kutangaza biashara zao.
Aliongeza kuwa pia wanatakiwa kuwa na kitabu maalumu chenye picha na nakala zao mbalimbali zinazoelezea kuhusiana na urefu wao, urefu wa kiuno, urefu wa nywele na mengineo muhimu ili wazitumie kujitangaza kirahisi zaidi katika mitandao ya kijamii au hata kuwa nayo wenyewe.
" Kikubwa ni kujua namna ya kujitangaza hasa zaidi kujionesha utoafuti wako wewe na wanamitindo wengine na kinachotakiwa ni kujitangaza na ili kufanikisha hilo yapo mambo mengi ya kuzingatiwa ili kutimiza ndoto hizo" aliongeza mwanamitindo huyo.
Kwa upande wake Edna Ndibarema aliwataka wanamitindo kuzingatia suala zima la usafi hasa katika kujiandaa wakati wa shoo, usafi wa mwili pamoja na kuimarisha haiba ya sura zao.
Alisema kuwa wanamitindo wengi wanashindwa kujitambua thamani yao na kujikuta wakitumiwa vibaya na watu mbalimbali kwa matamanio ya mwili na mengineo.
=====================