BASATA iwashugulikie wasanii "wakorofi "kivingine



Na Evance Ng'ingo
LICHA ya juhudi za serikali pamoja na wadau kadhaa binafsi kujikita katika kuendeleza tasnia ya sanaa ya muziki lakini bado kuna baadhi ya wasanii wenyewe wanakwamisha harakati hizo.

Wapo wasanii ambao bado wanataka kuendeleza dhana iliyokuwapo zamani kwa jamii kuhusiana na sekta ya sanaa kuwa ni uhuni ambayo kwa sasa imeshaanza kufutika.

Wasanii wengi kwa sasa wameiwekea heshima kazi ya sanaa kuwa ni kazi kama kazi nyingine na wamekuwa wakionesha wazi mafanikio yao kupitia kazi hiyo.

Ila wapo ambao wamekuwa wakiendeleza uhuni au kufanya mambo ambayo sio tu kinyume na sheria bali hata miiko inayosimamia sanaa husika.

Ni hivi karibuni Baraza la Sanaa laTaifa (BASATA) liliamua kuzuia kuchezwa radioni wimbo wa msanii wa muziki wa kizazi kipya Emanuel Elibariki, Nay wa Mitego.

Uamuzi huo unatokana na maudhui ya wimbo wenyewe ambao unaonekana dhahiri kuwa hauzingatii maadili ya sanaa.

Ni wimbo ambao umedharirisha utu wa watu na pia umetia dosari tasnia hiyo ya muziki wa kizazi kipya hasa ikingatiwa kuwa wimbo huo umechochea chuki kati ya wasanii husika.

Kutokana na mashahiri ya wimbo huo kuwa yanalenga kudharirishaji lakini pia tayari waliolengwa nao wameshaanza kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa kwenye wimbo.

Kuna baadhi ya maneno ambayo yamesikika katika wimbo huo akiwataja wasanii kama vile Ommy Dimpoz akimsema kuwa anashangaza hadi sasa hajulikani mwanamke wake ni nani.

Huku akiwajeli wasanii wengine Raymond Kigosi, Wema Sepetu na Jacline Wolper huku akiwasema wasanii wengine mambo yao binafasi ya kimaisha ambapo yanadalili za udharirishaji na yamechukuliwa ni kama kejeli na wanajamii.

Binafsi naona kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia ya mawasiliano bado BASATA hata kuufungia wimbo huo lakini bado haisaidii kitu.

Kwa sasa tayari wimbo huo licha ya kufungiwa kwenye radio lakini unasikika katika mitandao kadhaa ya kijamii kama vile WhatsApp  au mitandao mingine ya kijamii na watu wanausikiliza.

Mbali na kulipongeza Baraza hio lenye dhamana ya kusimamia sanaa nchini lakini ni vema kwa  BASATA kuangalia upya namna ya kuwashugulikia wasanii.

Kwa kuwa msanii anakuwa akijua kuwa wimbo utafungiwa lakini anaimba na kisha hata ukifungiwa basi ndio kwanza unakuwa umemtangaza zaidi kwa kuwa wapo watu ambao watataka kuusikiliza kwa njia ya mitandao.

Hapo bado msanii anaendelea kuwa juu kimuziki na ndio kwanza hata mapromota wanakuwa tayari kumwalika na watu wengi watahudhuria onesho lake.

Kinachotakiwa ni kuwaambi wasanii kuwa iwapo wakiimba nyimbo zisizofaa licha ya kufungiwa nyimbo husika na msanii pia ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni za baraza kwa wasanii husika.

Hii itasaidia wasanii kuepuka kutunga nyimbo mbaya zenye upotoshwaji wa maadili katika jamii, kama kuna uwezekano wa kutozwa faini au hata kuzuiwa kufanya maonesho inaweza kusaidia kwa kiasi fulani kurejesha maadili.

Lakini ni vema kwa watayarishaji wa muziki kuangalia namna bora ya kuepuke kurekodi nyimbo zenye upotoshwaji wa maadili.

BASATA ifike wakati iwazuie hata wamiliki wa studio za kurekodia muziki kuepuka kurekodi nyimbo kama hizo ili kupunguza uwezekano wa watu kurekodi nyimbo zisizokuwa na maadili.
=================

Related

Technology 8629488276872207114

Post a Comment

emo-but-icon

item